Hitimana kutua kesho

Muktasari:

  • Timu ya Namungo FC inatarajia kuanza mazoezi kesho Jumanne, huku kocha Mkuu wa timu hiyo, Hitimana Thierry naye akitarajia kuwasili kesho hiyohiyo kutoka Rwanda.

Kocha mkuu wa Namungo FC, Hitimana Thierry anatarajia kutua kesho Jumanne, Mkoani Lindi akitoka kwao Rwanda kwa ajili ya kuendelea na kazi.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Ally Seleman alisema asilimia kubwa ya wachezaji tayari wamewasili kambini na kesho wanatarajia kuanza mazoezi.
"Kocha wetu alikuwa Rwanda nyumbani kwao, hivyo kesho atakaporejea atakuta wachezaji wameanza mazoezi chini ya msaidizi wake, (Godefroid Okoko)," anasema Seleman.
Anaongeza pamoja na kocha kutua kesho, nyota wawili wa timu hiyo, Bigirimana Blaise na Styve Nzigamasabo raia wa Burundi nao watawasili Jumatano.
Hitimana kabla ya kutua Namungo FC aliwahi kuifundisha Biashara United (Tanzania), Musanze FC, AS Kigali, Rayon Sports zote za Rwanda na pia amewahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Rwanda.
Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 50 kwenye msimamo wa ligi.
Uongozi wa timu hiyo umeeleza lengo lao ni kuhakikisha wanamaliza ligi wakiwa nafasi za juu kuanzia ya nne.