Hitimana, Namungo wavutiana pumzi

Muktasari:

Hivi karibuni, Yanga ilimtimua kocha wake, Luc Eymael huku kocha msaidizi, Charles Mkwasa nae akiamua kukaa pembeni na Hitimana akitajwa kuwa mrithi wake.

Dar es Salaam. Kocha wa Namungo FC, Hitimana Thierry amesema kwa sasa anaandaa ripoti baada ya ligi kumalizika ili apate muda mfupi wa mapumziko na kujua hatma yake ndani ya kikosi hicho.

Hitimana amekuwa akihusishwa kutakiwa na Yanga kwa muda mrefu japo mwenyewe alikanusha kufuatwa kiofisi zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari.

Kocha huyo raia wa Burundi amekuwa kwenye msimu mzuri licha ya kumaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu Tanzania, pia ameiwezesha Namungo kucheza fainali ya Kombe la FA (ASFC) na kupata uwakilishi kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Aidha, Hitimana alisema, kwa sasa ataendelea kubaki nchini baada ya uongozi wake kumtaka wafanye mazungumzo kwa ajili ya msimu ujao unaotarajiwa kuanza Septemba 6 mwaka huu.

“Endapo nitaendelea kuwepo ndani ya Namungo, dirisha dogo la usajili sitaongeza nyota wa kimataifa kutokana na muda.

“Ripoti yangu itasema na kutoa mwongozo wa mchezaji gani na mahitaji katika kikosi, ila kwa sasa sitaweka wazi hadi viongozi waone na wafanyie kazi,” alisema.

Lengo kubwa la kusajili nyota wazawa pekee ni kutokana na kukosa muda wa kuwaangalia zaidi wachezaji wa kimataifa kabla ya kumridhisha kwa viwango vyao.

Hivi karibuni, Yanga ilimtimua kocha wake, Luc Eymael huku kocha msaidizi, Charles Mkwasa nae akiamua kukaa pembeni na Hitimana akitajwa kuwa mrithi wake.

Lakini hadi sasa, bado Yanga haijakuwa wazi juu ya kocha gani anayepewa nafasi ya kutwaa mikoba ya kocha wa Ubelgiji, Eymael.