Hili la Morrison bado Simba na Yanga hazijaingia kwenye mabadiliko

Tanzania ni nchi ambayo anaweza kuishi mtu wa aina yoyote hata kama ana upungufu wa aina gani ilimradi asitembee mtupu.

Kitakachokuvutia ni jinsi watu hasa wenyeji watakavyoweza kukuabudu kwa utajiri wako (kama unao), lakini pia hata kama ukiwa fukara pia watakuvumilia

Usijali sana hata kama akili yako ikiwa na upungufu nalo pia watatafuta namna ya kuishi na wewe - hilo haliwasumbui.

Mataifa mengine hali ya namna hiyo itategemea na uvumilivu wao hasa kwa lile watakaloona haliendani na maisha yao.

Ni vigumu sana kuamua kuishi na uongo, hapa kwetu wasio wakweli wanaishi na wewe, hawana shida kabisa.

Kwa sasa Taifa hasa medani ya michezo kuna sakata la mchezaji Bernard Morrison ambalo sitaki kuangalia hukumu yake iliyotakiwa kutolewa jana mchana kwani linakera kwa jinsi lilivyoendeshwa.

Medani ya soka imekuwa ikisimama tangu mwanzo wa wiki ikisubiri kujua hukumu ya sakata la mchezaji huyo na klabu yake ya Yanga litamalizwa vipi na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Kesi yake imechukua siku kadhaa ikipigwa danadana kutoa uamuzi wa kipi kiamuliwe kati ya mchezaji na klabu, na ndani yake pia ikaongezeka Simba ambayo hapa ilikuwa kama ndege inayosubiri mzoga uanguke ili ijichukulie.

Maisha ya Morrison na Yanga yalitosha kugundua kwamba klabu hiyo kongwe ilikosea kumsajili kwani licha ya kipaji chake hakuwa mchezaji mwenye rekodi bora ya nidhamu kuanzia maisha ya nje ya uwanja mpaka ndani ya uwanja.

Hilo linathibitika kuanzia huko alikopita lakini pia hata hapa ndani ya nchi akiwa hapohapo Yanga kwa kuwa na matukio tofauti ya kukosa nidhamu.

Yanga wanajua walipokosea, hawakufanya uchunguzi ni mchezaji gani wanayemsajili na bahati mbaya zaidi hata walipokuwa wakitafakari kumuongezea mkataba hawakutaka kujiuliza mara mbili ilikuwaje mchezaji mwenye kipaji kama chake akawa huru bila kuwa na timu huko alikokuwa.

Angalau swali hili lingewaongoza katika kujua uhalisia wa maisha yake halisi.

Wakati Morrison akisumbuana na Yanga, Simba nao wakaingia na ubora wao katika kumtaka mchezaji huyohuyo - tena wakipambana zaidi wakiona mchezaji husika anaishi maisha ambayo hatakiwi kuishi na kwao atakuwa sawa na atacheza mpira mkubwa.

Unaweza kujiuliza hivi maisha ya Simba yamebadilika kwa kiasi hicho kuyazidi hata ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambayo Morrison aliitumikia na baadaye kuachana naye?

Jibu utakalopata hapa utagundua kwamba wakati tunatamani kuzibadilisha klabu zetu kwenda kuishi maisha ya kisasa na weledi, kumbe bado kuna viongozi wanatuthibitishia kwamba uwezo wao wa kutafakari ni mbali katika maisha ya kuishi kwa weledi.

Nilitegemea Simba wangejifunza uhalisia hata wa yanayotokea Yanga kati ya Morrison na klabu yake kujitosheleza kwamba licha ya kipaji cha mchezaji, lakini hana hadhi ya kuitumikia klabu hiyo, kama kweli tuliambiwa kwa usahihi kwamba wapo wachezaji ambao walilazimika kutopewa mikataba mipya msimu uliopita kutokana na kukosa nidhamu.

Nakumbuka vizuri kwamba kuna wakati mkurugenzi mmoja wa Bodi ya Wadhamini ya Simba aliwahi kuja mbele ya vyombo vya habari na kusema kwamba, wataachana na baadhi ya wachezaji kutokana na suala la nidhamu na wengi waliunga mkono hatua hiyo na kudhani kwamba kweli klabu hiyo imeamua kuishi katika njia ya mabadiliko.

Kilichonisikitisha Simba hiyohiyo tena inataka kumsajili mchezaji anayedaiwa kuwa aliwahi kuwatishia watu, lakini pia akionyesha matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu huko alikopita na hata alipo sasa.

Kusikia haya na utambulisho wa Simba kwa Morrison ukanishtua na kuanza kujiuliza hivi klabu hii ya Msimbazi bado inaongozwa na MO Dewji ambaye aliamua kuwaondoa wachezaji kwa kukosa nidhamu na sasa ameamua kuwarudisha?

Hapa kuna haja ya kujitathimini kwa viongozi wa klabu hizi kubwa mbili kwamba, wanatakiwa kutambua wapo ambao wana akili zaidi yao na wanatafakari aina ya maisha wanavyoziendesha na hasa wanafuatilia jinsi wanavyokimbizana na hili sakata la Morrison.