Hili la Morrison, atafungwa mtu

HABARI ya mjini kwa sasa kwenye vilinge vya soka ni sakata la winga Mghana Bernard Morrison. Mashabiki wa Yanga wanatokwa povu kusikia winga huyo ametua kwa watani wao Simba, huku wenzao wakichekelea baada ya kuona picha zikimuonyesha akisaini akiwa na uzi wa Msimbazi.

Pia mashabiki wa timu zote hizo mbili wamegawanyika, wapo wachache wa Yanga wanaoona ni bora aende zake tu Simba, huku wengine wakipinga na kulaumu uongozi wakiamini labda wamepigwa changa la macho walipoambiwa kwa msisitizo kuwa, jamaa aliongeza mkataba wa miaka miwili.

Upande mwingine mashabiki wengine wa Simba wanapinga usajili wa winga huyo wakidai jamaa ni mtukutu na ataenda kuiharibu timu yao iliyotulia kwa misimu mitatu ikibeba mataji wakatavyo, lakini wengine ambao ndio wengi wanashangilia pigo hilo walilopigwa watani wao. Wanadai sasa ni zamu yao kuumia kama walivyoumia walipocharazwa 1-0 kwenye Ligi Kuu Bara kwa mkwaju wa friikiki iliyopigwa na winga huyo huyo na kuwapa kelele nyingi mashabiki wa Yanga.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba sakata la usajili Mghana huyo, Bernard Morrison bado linasumbua vichwa vya mashabiki na sio hao tu hata wanasheria nao wamekuwa na maoni yao huku tahadhari kubwa ikiibuka juu yake.

Ipo hivi. Juzi mchana Simba kupitia mitandao yake ya kijamii ilimtambulishaMorrison kuwa staa wao mpya baada ya uvumi wa muda mrefu, huku wakianza na ujumbe siku moja kabla wakiwataka mashabiki wa soka wajiandae kushtuka kwa kile watakachokifanya saa 8 ya siku ya Nanenane ambayo kwa kawaida huwa ni Simba Day, ambayo imeshindikana mwaka huu kwa sababu ya corona.

Ndipo mchana buana wakaziachia picha hizo na kusisimua mashabiki wa pande zote, lakini mapema Yanga nao walishafanya tukio kama hilo wakidai mchezaji huyo alishasaini mkataba wa kuongeza wa miaka miwili kuendelea kuitumikia klabu hiyo na hivyo kusubiri kuona nini kitatokea leo Jumatatu.

Ndio, leo inaelezwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokuwa inashughulikia sakata la mchezo huo na viongozi wake, itatoa uamuzi wa kesi hiyo, lakini ikiwa tayari Simba wakiwa wameshamtambulisha kabla kesi haijafikia tamati na mabosi wa Jangwani wakaapa ‘Tutawakomesha’.

Hata hivyo, Yanga ikisisitiza Morrison ni mali yao, jamaa alishawakataa kitambo akisisitiza mkataba wake ule wa miezi sita ulishamalizika tangu Julai na kudai hakusaini mkataba huo mpya hatua ambayo ni wazi iliwapa nafasi Simba kumalizana naye fasta.

UTATA ULIPO

Kupitia utata huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (enzi za FAT), Ismail Aden Rage ameiambia Mwanaspoti kuwa sakata hilo linaweza kuleta athari kwa klabu zote mbili endapo moja itagundulika imedanganya katika suala la kuingia mkataba huo.

“Unajua Yanga wanasema waliingia mkataba na Morrison, lakini hakuna aliyeuona, Simba pia wanasema wameingia mkataba na Morrison hakuna aliyeuona sasa kwa mawazo yangu ya kisheria hili lina utata,” alisema Rage.

“Athari inaweza kuwa klabu moja wapo itakayogundulika kudanganya adhabu yake kwa FIFA ni kubwa sana wakisalimika labda ni kufungiwa maisha kujihusisha na soka sijajua sheria za TFF.

“Kama Yanga wanadanganya kwamba waliingia mkataba na Morrison ikaja ikagundulika kuwa saini ya mchezaji sio yenyewe najua kwamba TFF hawana mamlaka ya kugundua saini vipo vyombo vinavyoweza kuamua hilo basi ikiwa hivyo hilo ni kosa la jinai na adhabu yake ni kubwa,” alisema Rage na kuongeza;

“Simba nao kwa kuwa mchezaji huyu alikuwa hapa ndani tena alishacheza hapa kama itagundulika kuwa waliingia mkataba na mchezaji ambaye alikuwa na mkataba na klabu yake hilo nalo ni kosa baya ndio maana nasema linaweza kusababisha viongozi wengi waliohusika kufungiwa.”

Rage ambaye amewahi kuwa pia Makamu wa Rais wa TFF alisisitiza; “Yanga anaweza kufungiwa kiongozi wao yeyote aliyehusika pale kwa klabu yangu (Simba) bahati mbaya hatujajua inaongozwaje lakini kwa haraka anaweza kufungiwa Mtendaji Mkuu wa klabu au Mwenyekiti wa Bodi.”

TFF LAWAMANI

Rage aliongeza katika sakata hili, pia TFF nao hawatakwepa lawama kutokana na muda ambao wamekuwa wakilifanyia kazi sakata hilo tangu liibuke.

“Tumeambiwa Agosti 10 (yaani leo) watatoa uamuzi lakini binafsi naona wamechukua muda mrefu sana kutoa maamuzi na wakati mwingine shida nyingine zilianzia hapo kama wangetoa uamuzi mapema haya mengine yasingetokea,” alisema Rage.

TFF ilikuwa ikilishughulikia suala hilo kupitia Kamati yake ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji na tangu wakutane hawajawahi kutoa uamuzi wowote kabla ya hivi karibuni kuelezwa sakata hilo limepelekwa kwenye vyombo vya dola kutokana na kubaini utata kupitia ushahidi wa pande zote.

“Yanga wametoa vielelezo vyao na Morrison naye amekuwa akisisitiza hajasaini, hapo kuna utata hivyo tumelipeleka jambo hilo polisi ili kufanya uchunguzi wa nyaraka kubaini nani mkweli,” aliwahi kunukuliwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya TFF, Elias Mwanjala.

KISASI MBUYU TWITE

Aidha, Rage alisema kama ikigundulika Simba walimsajili Morrison kihalali sakata hilo litakuwa limemrejeshea furaha kubwa na kulipa kiasi cha sakata la beki Mbuyu Twite ambaye Yanga waliwazidi kete 2012 kwa kumsainisha wakitangulia kumalizana na klabu yake.

WASIKIE WADAU SASA

Mbali na Rage, baadhi ya wadau wakiwamo Mwanasheria wa zamani wa TFF, Emmanuel Muga nao walikuwa na maoni tofauti, huku wakisema suala hili linaweza kumfunga mtu kama itabaini kuwepo kwa udanganyifu.

Muga alisema, shirikisho hilo ndilo lenye mamlaka ya kuuthibitishia umma kama Morrison ni mchezaji halali wa klabu ipi kati ya Simba na Yanga kulingana na uhalali wa mikataba iliyonayo.

“Anayetunza na kuhalalisha mkataba ni TFF ambao pia ndio wanaohalalisha usahihi wa mkataba na baadaye kufika mpaka Fifa sasa hapa kuna madai ya mkataba kughushiwa,” alisema Muga.

Muga akiangalia upande wa TFF alisema Shirikisho hilo mara baada ya mkataba wa Morrison na Yanga wa miezi sita kumalizika kisha kuupokea mkataba mwingine wenye utata walipaswa kuzuia makubaliano yoyote mengine kati ya mchezaji husika na klabu nyingine.

Naye mchambuzi Ally Mayay TFF ndio wenye mamlaka ya kutoa usahihi wa mkataba kupitia mkataba au mikataba waliyonayo.

“Siku hizi sio kama miaka ya nyuma kwamba mikataba inahalalishwa kwa makaratasi siku hizi kuna mfumo wa kisasa wa Usajili wa Kimataifa (TMS) kila klabu inapewa namba yake na kuingiza taarifa za usajili kwa wachezaji wake sasa TFF itaingia huko na kutoa usahihi wa upi ni mkataba halali na kibaya zaidi mfumo huo hauwezi kuziruhusu klabu mbili tofauti kuingiza taarifa za mchezaji mmoja,” alisema Mayay.

KAULI YA YANGA

Yanga kupitia katibu Mkuu wake wa sasa, aliye Mwanasheria pia, Simon Patrick imesisitiza mashabiki wa Yanga hawapaswi kuwa na presha kwani wanaenda kutoa fundisho kwa waliohusika na sakata la Morrison, ili kuhakikisha haki inapatikana na kukomesha mambo ya kihuni katika soka la Tanzania.

Katika akaunti yake binafsi katibu huyo wa Yanga aliandika; “Wananchi msikubali kuyumbishwa, hili sakata ndio litakaloleta mageuzi ya mpira wa Tanzania, kuanzia kwenye mfumo wa haki mpaka taasisi za soka. Serikali ya JPM husimama upande wa wenye haki, CAS pia husimama upande wa wenye haki.

“Nawaomba Wanayanga msiwe na wasiwasi wa aina yoyote zama za ujanja ujanja zimeisha. The series is on, vaa miwani ya 3D, agiza kahawa weka bundle. Nawatakia mapumziko mema ya Sikukuu ya Nane Nane.”

Kwa upande wa Simba mpaka sasa hawajasema lolote zaidi ya ujumbe wao wa ‘Morrison is Red’.