Hiki ndicho kinachowarudisha nyumbani wazawa

NI ndoto ya idadi kubwa ya nchi duniani kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi mbalimbali kubwa na zenye umaarufu duniani.

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho nyota wanaocheza katika ligi hizo hukipata kutokana na mishahara, bonasi, posho na hata mikataba binafsi ya kampuni mbalimbali kutokana na matangazo ya biashara, ni sababu ambazo hushawishi idadi kubwa ya wachezaji kutamani kucheza katika ligi hizo.

Mfano wa ligi hizo ni ile ya England (EPL), Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligi Kuu ya Italia, Ligi Kuu ya Ujerumani, Ligi Kuu ya Uholanzi na Ligi Kuu ya Ubelgiji.

Hata hivyo kwa bahati mbaya, mambo yamekuwa tofauti kwa kundi kubwa la wanasoka hapa nchini ambao kwa muda mrefu wengi vipaji vyao vimekuwa vikiishia katika Ligi Kuu ya hapa nyumbani.

Ni wachache waliofanikiwa kupiga hatua na kati yao ni Mbwana Samatta pekee aliyeweza kupenya hadi kufika katika Ligi Kuu ya England akiitumikia Aston Villa lakini pia aliwahi kutamba katika Ligi Kuu ya Ubelgiji ambako alikuwa akiichezea KRC Genk.

Wengine ambao angalau wameweza kukucheza nje ya Tanzania kwa mafanikio, wapo katika ligi za ndani ya Bara la Afrika kama vile Saimon Msuva anayechezea Difaa Jadida ya Morocco, Ally Msengi (Stellensboch, Afrika Kusini) na Abdi Banda aliyepo Highlands Park ya Afrika Kusini.

Hata wengi waliopata fursa ya kucheza soka nje ya nchi, walishindwa kudumu na kuishia kurejea nyumbani ambako baadhi yao, wamepotea kwenye ramani ya soka kwa sasa.

Kuna orodha ndefu ya wachezaji waliopata fursa hiyo na wakarejea nchini lakini kiuhalisia wanaoshindwa kucheza nje ni wengi kuliko wanaobakia.

Mfano wa wachezaji waliowahi kwenda nje na kurejea nchini ndani ya muda mfupi ni Jerry Tegete, Mrisho Ngassa, Uhuru Selemani, Farid Musa, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Shiza Kichuya, Hassan Kessy, Adam Salamba, Haruna Moshi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Abdi Kassim, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Yusuf Soka, Shaaban Iddi, Danny Mrwanda na wengineo.

Kumekuwa na sababu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na wachezaji hao pindi wanaporudi nchini lakini kubwa zaidi ambayo huwa imekuwa ikijirudia ni maslahi wanayopata kuwa kidogo kulinganisha na mahitaji yao kama wachezaji wa kigeni huko.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa zipo sababu nyingine kubwa zaidi ya hiyo ambazo zinapelekea kukwamisha wachezaji wetu na hiyo ya maslahi imekuwa haina uzito sana ingawa haikosekani.

Sababu hizo ni kiwango duni, kushindwa kuhimili mazingira mapya, maslahi na kutokuwa na nidhamu na msingi mzuri wa soka tangu utotoni.

UGENI WA

MAZINGIRA

Baadhi ya wachezaji wa Kitanzania hurejea nyumbani kutokana na kukosa uvumilivu na subira katika nchi ambazo huelekea yale ya ndani na ya nje ya uwanja, hujikuta wakikosa uvumilivu na kulazimika kuamua kutoendelea kucheza huko.

Ndani ya uwanja hujikuta wakilazimika kutumia muda mwingi katika kufanya mazoezi hasa yale ya ufiti na utimamu wa mwili ambayo huku kwetu yamekuwa yakitolewa kwa kiwango cha chini.

Lakini nje ya uwanja hukutana na changamoto ya chakula, lugha na mtindo tofauti wa maisha hali inayopelekea waamue kurejea nyumbani.

Nyota wa zamani wa Simba, Danny Mrwanda amefichua kuwa mazoea ya maisha ambayo wachezaji wa Kitanzania wamekuwa wakiishi hapa nchini, yamekuwa yakiwagjarimu pindi wanapoenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.

“Maisha ya wenzetu kule ni tofauti na yetu na muda wote mchezaji amekuwa akiishi kwa kufuata ratiba na hata muda ambao wa mapumziko, kila mtu anakuwa kwake,” anasema Mrwanda na kuongeza;

“Sasa kwa sisi ambao tumeshazoea huku kwetu, ambako ni rahisi kukutana na ndugu, marafiki na mashabiki mara kwa mara inakuwa ni vigumu kwa mtu kuendelea kubaki huko na kuamua kurejea nchini.”

Staa huyo aliyewahi kukipiga pia Yanga na Polisi Morogoro anaongeza; “Lakini kingine ni kwamba wanakutana na maisha mapya ambayo ni tofauti na huku nyumbani hasa katika masuala ya lugha, chakula na hata aina ya mazoezi na mbinu hivyo wanaona badala ya kujitesa huko wanaona bora warudi.”

Naye Kocha na mchambuzi wa soka nchini, Kennedy Mwaisabula anasema kufeli kwa baadhi ya wachezaji kucheza soka la kulipwa ni kutokana na malezi waliyopata kwenye soka lao.

“Tumeondoka kwenye misingi ya mpira na maisha ya mchezo huo, walio wengi hawajapita kwenye akademi ukiachana na baadhi yao kama akina Simon Msuva na Mbwana Samatta.

“Wachezaji wengi hawajui kuishi maisha ya ‘uprofesheno’ hawajazoea upweke, lugha kwao ni shida ukiachana na masuala ya kukatwa kodi kwenye mishahara yao, haya mambo wengi yanawashinda wamezoea wakitoka mazoezini ama kwenye mechi waingia mtaani wajichanganye.

TATIZO KIWANGO

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kundi kubwa pia hufelishwa na viwango duni ndani ya uwanja ambavyo huonyesha mazoezini na hata katika baadhi ya mechi.

Wengi wao huonyesha kiwango cha chini mazoezini na katika baadhi ya mechi jambo ambalo hupelekea watupiwe virago

Mfano wa hilo ni kwa winga aliyerejea nchini na kujiunga na Yanga, Farid Musa ambaye katika kipindi chote cha miaka mitatu (3) alichokuwepo Hispania akiitumikia CD Tenerife, hakuwa kucheza hata mchezo mmoja wa kimashindano akiwa na timu hiyo na muda mwingi aliutumia akiwa katika kikosi cha vijana cha Tenerife.

Winga wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Uhuru Seleman alisema kuwa ni vigumu kwa mchezaji mwenye kiwango duni kucheza nje ya nchi.

“Kwa bahati nzuri mimi nimecheza soka la kulipwa nje. Hiyo nafasi haikuja kwa bahati mbaya bali kiwango na uwezo wangu ndio uliwashawishi.

Lakini kama kiwango chako kiko chini, huko nje hawana uvumilivu,” anasema Uhuru.

MASILAHI KIDUCHU

Urahisi wa wachezaji kupata fedha hapa nchini kinyume na zile za mishahara au ada ya usajili, ushawishi baadhi ya wachezaji kurudi nchini na kuendelea na soka la hapa kutokana na wakihisi wanaweza kuvuna kiasi kikubwa cha fedha ambayo matumizi yake sio makubwa tofauti na nje ambako mchezaji anapata kile alichokisaini katika mkataba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mrwanda alisema kuwa fedha ambazo wachezaji huzipata siku za mwanzoni pindi wanapoenda kucheza soka la kulipwa, wengi wao huziona ndogo na kufikiria kurejea nyumbani.

“Inawezekana mchezaji akawa analipwa Dola 300 huko nje ambako hajapazoea halafu anaambiwa atalipwa Dola 200 hapa wengi ndio huangukia kwani wanaona kuna uwezekano wa kupata hela nyingi na isiwe na matumizi makubwa ikiwa watacheza hapa tofauti na wakiwa Ulaya.

Lakini wanasahau kwamba wakiwa wavumilivu, wanaweza kupata fedha nyingi ambayo pengine hata hawajawahi kuiota, ikiwa watapiga hatua kisoka,” alisema Mrwanda.

Beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alieleza sababu ya kuvunja mkataba wake na timu MFK Vyskv ya nchini Czech kuwa ni timu hiyo kushindwa kumlipa.

“Kule ni nchi za watu, isitoshe ugonjwa wa covid 19 ndio ulikuwa umepamba moto, halafu unaona timu haikulipi, hivyo nikawa nimeshindwa kujikimu,”anasema Ninja.

Kwa upande wake kocha Mwaisabula alisema urahisi wa kupata fedha hapa nchini unawapumbaza wachezaji.

“wanashindwa kufanya vizuri, nchi hizo kwa sababu mchezaji anaishi na pesa anayoipata tu na sio nje ya mishahara yao kama ilivyo hapa wakimaliza mechi mashabiki wanawapa hela,” anasema Mwaisabula

UDAHIFU KIUTAWALA

Changamoto nyingine ambayo imekuwa ikiwaangusha wachezaji nje ya nchi ni ukosefu wa usimamizi mzuri lakini pia matatizo ya kiutawala kwa klabu wanazotoka au wanazokwenda kuzichezea

Mfano wa wachezaji ambao walikwamishwa na changamoto hiyo ni Shomary Kapombe.

Kapombe ni miongoni mwa wachezaji waliopita kwenye kituo cha Moro Kids kilichopo Morogoro ambako ndiko nyumbani kwao.

Simba ilimsajili Kapombe akitokea Polisi Moro ambao walimchukua kwenye kituo hicho cha kulea na kukuza vipaji vya soka kwa vijana, usajili wa Kapombe kwenda Simba ulifanywa msimu wa 2011 ambapo alidumu kikosini hapo hadi mwaka 2013.

Baadaye Kapombe alitimkia timu ya Cannes ya nchini Ufaransa ambako alikaa kwa msimu mmoja pekee wa 2013/14 na kuamua kurudi nyumbani kutokana na sababu mbalimbali. Kapombe alipotoka Ufaransa hakurudi Simba kwani walishindwa kumsaidia kutatua matatizo yake ya kisoka akiwa Ufaransa hivyo kuamua kujiunga Azam FC msimu wa

2014/17.

Ilielezwa kuwa baada ya kukwama kurudi Ufaransa, Kapombe alianza kutengenezewa zengwe na timu yake hiyo ya Cannes iliyomsajili kwa mkataba wa miaka minne.

Kapombe wakati anavutana na Cannes alianza kufanya mazoezi na Azam FC kitendo hicho kilionekana kuwakwaza

Cannes ambao baadaye walianza kumletea figisu za kutaka kumfungia endapo angesaini timu hiyo.

Wakati huo Shirikisho la Soka nchini (TFF) chini ya Jamal Malinzi, inadaiwa lilipokea barua kutoka Cannes ya kulalamikia mchezaji huyo kujiunga Azam ambapo Malinzi aliingilia kati kutatua Kapombe asifungiwe kwani pia ni tegemeo timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

Cannes walitaka Kapombe arudi Simba na walipe Euro 33,000 lakini kwenda Azam walitaka walipwe Euro 70,000 jambo ambalo kwa matajiri hao wa ligi nchini halikuwa gumu, walilipa kiasi hicho cha pesa.

Inadaiwa Kapombe kushindwa kurudi kwake pia kulichangiwa na wakala wake ambaye aliufahamu mchongo mzima unavyoendelea na ndiyo maana mchezaji huyo alikwama Uwanja wa Ndege wa Kenya baada ya Visa yake kumsumbua maana alitafuta Visa ya muda.

Na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa safari yake ya Ufaransa kwani hata akaunti zake za benki zilifungwa na timu hiyo ambapo pesa yake iliyokuwa kwenye akaunti hiyo zilizuiwa. Corona nayo imewanyima fursa.

Baadhi ya wachezaji waliorejea nchini wameliambia gazeti hili kuwa mlipuko na kusambaa kwa virusi vya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid19 kumechangia kuwafanya warejee nyumbani

ADAM SALAMBA

Baada ya klabu ya Simba, kumuondoa kwenye mpango wao 2019 alikwenda kujiunga na Al-Jahra ya nchini Kuweit, ambako alisaini miaka mitano.

Ugonjwa wa covid 19, ulikuwa unatishia amani katika nchi ya Kuwaiti, hivyo uongozi wake ukavunja mkataba na kuwalipa pesa wachezaji wote wa kigeni katika timu hiyo.

“Yaani kurejea nchini kwangu Tanzania nikiwa salama ni jambo la kumshukuru Mungu,kilichoniondoa ni ugonjwa huo sio kitu kingine, ligi kule ilifutwa kabisa,” anasema.

hassan kessy

Pamoja na kukiri mkataba wake ulimalizika katika klabu ya Nkana ya Zambia, kikichomfanya arejee Tanzania na kushindwa kupambana mbele kwa mbele na ugongwa wa covid 19. “Nasubiri hali ya ugonjwa huo itengamae kwani ndipo nianze kutafuta timu nje kwani nina mawasiliano ya timu nyingi, Ila kwa sasa nipo na Mtibwa Sugar,” anasema.

DAVID KISU

Kipa mpya wa Azam FC, David Kisu yeye alitoa sababu ya kuvunja mkataba na Gor Mahia ya Kenya kwamba ni baadhi ya mambo hayakuenda sawa na uongozi wake.

“Siwezi kuweka wazi ni kitu gani hasa, lakini tayari nimemalizana nao mpaka najiunga na Azam FC, ambayo kwangu ni sahihi sioni kama nimepotea njia,”anasema.

DAVID NAFTAR

Alikuwa anacheza Tusker ya Kenya, lakini ugonjwa wa covid 19 ndio uliomkimbiza na akarejea Tanzania kujiunga na Mbeya Kwanza.

“Sina sababu nyingine ni huo ugonjwa, licha ya mkataba wangu ulimalizika bado Tusker ilikuwa inahitaji niendelee na huduma yangu,”anasema.

MAONI YA WADAU

Henry Shindika ni miongoni mwa wachezaji waliocheza kwa muda mrefu nje ya Tanzania ambapo anasema haikuwa rahisi kwake lakini alivumilia changamoto zote alizokutana nazo huko kwani malengo yake aliamini yangetimia tu.

“Sio rahisi kujuwa kwa nini wachezaji wengine wanashindwa kucheza nje wanapopata nafasi, nadhani wanarudi kwa sababu kila mtu anajua changamoto anazokutana nazo huko, mimi nilivumilia sio na mwingine ataweza, labda mazingira yake aliokutana nayo magumu kwenye timu, hivyo anachoka na anataka kucheza halafu mwelekeo hamna anaamua kurudi.

“Niliamua kuvumilia mpaka mwisho wa mkataba wangu, changamoto ya namba na jinsi ya kuishi wenzetu lakini ilifikia wakati nikazoea nikaendelea kupambana mpaka mkataba wangu ulipomalizika,” anasema Shindika.

TFF YAFUNGUKA

Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Oscar Mirambo alisema maandalizi ya wachezaji ndio yanayowakwamisha. “Wachezaji wetu wengi wanaibuka tu na hawapati msingi mzuri tangu wakiwa na umri mdogo hivyo kuna vitu huwa wanavikosa ambavyo baadaye vinawagharimu pale wanapoenda nje.

“Lakini suluhisho la hili ni kuwa na mfumo mzuri ambao utajumuisha mtaala kwa makocha na falsafa ya pamoja kama nchi ili wachezaji wapate maandalizi mazuri kuanzia katika umri mdogo,” anasema Mirambo.

Imeandikwa na Olipa Assa, Charles Abel na Mwanahiba Richard