Hii ndo Yanga yenyewe, huyo Morrison anajua hadi aibu

Muktasari:

Kabla ya kusafiri kwenda Singida kuvaana na wenyeji kwenye Uwanja wa Liti, Eymael alilieleza Mwanaspoti kuwa yeye ni kocha wa kimataifa na mwenye viwango hivyo, kupoteza mechi mbili za kwanza halikuwa jambo zuri na kwamba, akiendelea kupoteza zaidi atalazimika kufikiria hatima yake.

LICHA ya kucheza kwenye uwanja ambao eneo lake la kuchezea sio rafiki kwa soka la burudani, lakini kiungo winga wa Yanga, Bernard Morrison jana amewapa mashabiki jeuri ya kutamba huko mitaani.

Winga huyo Mghana aliyenaswa kwenye dirisha dogo la usajili, jana aliwanyanyasa anavyotaka walinzi wa Singida United wakati Yanga ikipata ushindi wake wa kwanza ikiwa chini ya Mbelgiji, Luc Eymael.

Mbali na Morrison, mastraika mwili jumba David Molinga ‘Falcao’ na Yikpe Gnamien na kiungo Haruna Niyonzima na waliwasahaulisha mashabiki wa Jangwani vipigo viwili mfululizo wakati walipoiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Chini ya Eymael, ambaye jana amepewa onyo kali na Bodi ya Ligi, Yanga imepoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC na jana iliingia uwanjani kusaka ushindi na dalili zilianza mapema tu kutokana na kupiga mpira mwingi huku mastaa wake wakicheza soka la kuvutia licha ya uwanja kuwatibulia.

Kabla ya kusafiri kwenda Singida kuvaana na wenyeji kwenye Uwanja wa Liti, Eymael alilieleza Mwanaspoti kuwa yeye ni kocha wa kimataifa na mwenye viwango hivyo, kupoteza mechi mbili za kwanza halikuwa jambo zuri na kwamba, akiendelea kupoteza zaidi atalazimika kufikiria hatima yake.

Hata hivyo, kwa ushindi huo Mbelgiji huyo ameanza kupumua na kuiweka ajira yake kwenye sehemu salama.

Kwa ushindi huo, Yanga imepanda nafasi nne ikiwa na alama 28 katika michezo yake 15 huku Singida United ikiendelea kuanguka katika nafasi ya 19. Azam FC ambayo jana imeichapa Mwadui FC kwa bao 1-0 imejiimarisha katika nafasi ya pili ya msimamo ikiwa na pointi 35, sita nyuma ya vinara Simba wenye pointi 41.

Yanga ilianza mchezo huo kwa kasi na kutawala zaidi eneo la kati ikiwatumia vyema Niyonzima na Papy Tshishimbi ambao, waliwazidi ujanja na maarifa viungo wa Singida United wakiongozwa na Athuman Iddi (Chuji), Haruna Moshi Boban na Six Mwakasega.

Hata hivyo, Singida United walikosa utulivu katika dakika 45 za kwanza ambapo, hata mashambulizi waliyotengeneza yalikuwa yakipotea kwa walinzi wa Yanga, Lamine Moro na Said Makapu ambao walicheza kwa kuelewana.

Iliwachukua Yanga dakika 12 tu, kutangulia kupitia kwa Molinga, ambaye aliusukumiza mpira wavuni wakati kipa wa Singida United, alipotokea mpira baada ya shuti la Mapinduzi Balama kumgonga beki. Molinga, ambaye jana alionyesha uwezo mkubwa kupambana kusaka mabao kwa timu yake, aliuwahi na kuuchop mpira huo na kumuacha Chaima mikono mitupu.

Kama kawaida Yanga walikuwa wakiingia ndani ya eneo la hatari la Singida United, wakitumia mabeki wa pembeni hasa Juma Abdul kusukuma mipira kwa Kaseke na Morrison, ambaye kila anapogusa mpira mashabiki wa Yanga walikuwa wakimsha shangwe.

Licha ya kusumbua ngome ya Singida United, staili ya Morrison kuchezea mpira kadri anavyojisikia, iliongeza mzuka kwa mashabiki wa Yanga.

Kocha wa Singida United, Ramadhan Nswanzurwino alifanya mabadiliko dakika ya 27 kwa kumtoa Kazuru Mashauri na kuingia Steven Opopu kusaidia kuimarisha eneo la kiungo ambako, Niyonzima na Tshishimbi walifunika kabisa.

Hata hivyo, kama Molinga angekuwa makini jana basi angeweza kuipatia Yanga hata mabao matatu kutokana na kupata nafasi nyingi za mabao.

Ndani ya dakika 45 za kwanza, Molinga alikosa bao lingine baada ya Morrison kupiga pasi ndani ya boksi na Balama alipiga shuti hilo lililounganishwa na Molinga, lakini lilipanguliwa Chaima na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Dakika 56, Haji Mwinyi nusura aisawazishie Singida United baada ya kupiga krosi ya moja kwa moja akipokea pasi ya Stephen Opopo, lakini ikatoka pembeni kidogo mwa lango.

Dakika 58 Yanga ilijihakikishia ushindi kwa kuandika bao la pili kupitia Niyonzima, akiunganisha kwa shuti kali krosi ya Morrison ambaye aliwakusanya walinzi wawili wa Singida United na kupiga krosi iliyounganishwa kwa shuti kali.

Dakika 62 kiungo wa Yanga, Tshishimbi alionyeshewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Opopo aliyekuwa anakimbia na mpira huku Niyonzima naye akazawadiwa kadi kwa kumkwatua Boban.

Yanga walifanya mabadiliko ya kumtoa Molinga na kuingia Yikpe, Kaseke na kuingia Abdulaziz Makame huku Singida wakimtoa Elynyesia Sumbi na kuingia Athuman Idd ‘Chuji’.

Dakika 76, Yikpe aliifungia Yanga goli la tatu kwa kichwa baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa wapinzani wao ambapo, Balama alipiga mpira wa kichwa uliokutana na Yikpe aliyeweka wavuni.

Singida walicharuka na kupata bao la kufutia machozi katika dakika ya 83 kupitia Mwakasega aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Opopo.