Hii ndio team mataji Afrika

LONDON, ENGLAND. WANASOKA wa Kiafrika wanafanya vizuri sana huko Ulaya. Waafrika wana wachezaji kibao wakifanya vyema kwenye ligi hizo za Ulaya, ikiwamo Ligi Kuu England, kwa mashabiki wa soka la Kenya, huwakosi kwenye televisheni zao kumtazama kiungo wao matata, Victor Wanyama pindi anapokuwa na kazi ya kuitumikia timu yake ya Tottenham Hotspur kwenye ligi hiyo. Hata hivyo, Wanyama hajafurahia kubeba taji lolote kwenye Ligi Kuu England.

Makala haya yanahusu wanasoka wa Kiafrika waliobeba mataji mengi, akiwamo beki Kolo Toure, ambaye rekodi zake zinaonyesha kwamba amenyakua mataji 10 tofauti kwa nyakati zake alizodumu kwenye soka hilo la Ulaya, akipita kwenye vikosi vya Arsenal, Manchester City na Celtic alikobeba mataji, wakati kwa wakati wake wa Liverpool haukuwa na majaabu. Hawa ndio mastaa wa Kiafrika wenye mataji mengi zaidi.

5.Nwankwo Kanu- mataji 12

Gwiji wa Kinigeria, Nwankwo Kanu ni staa mwennye mataji kibao aliyowahi kubeba katika maisha yake ya soka. Mshambuliaji huyo alifanya vizuri sana akiwa na Ajax kabla ya kwenda Inter Milan, Arsenal na Portsmouth. Rekodi zake zinaonyesha, Kanu amebeba mataji 12, lakini nyakati zake alizokuwa Ulaya, alikuwa kwenye timu zenye mastaa wa maana wakiwamo kina De Boer, Ronald Koeman, Clarence Seedorf, Patrick Kluivert na Edwin Van Der Sar kwa kuwataja kwa uchache tu. Mchezaji mwingine aliyetwaa mataji 12 ni John Obi Mikel.

4.Michael Essien- mataji 12

Kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ghana, Michael Essien huduma yake ya ndani ya uwanja ilikuwa si ya mchezo. Essien nni mmoja kati ya viungo mahiri kabisa kuwahi kutokea kwenye soka la Kiafrika. Essien alicheza klabu nyinngi za Ulaya, lakini mafanikio makubwa aliyapata kwenye vikosi vya Olympique Lyon na Chelsea. Rekodi zake zinaonyesha kwamba amebeba mataji 12, huku akiwahi kuzichezea pia Real Madrid na AC Milan. Akiwa Lyonn alibeba ubingwa wa ligi mara mbili sawa na huko Chelsea pia, ambako pia alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

3.Yaya Toure- mataji 17

Kiungo Yaya Toure ni mmoja kati ya wanasoka wa Kiafrika waliobeba mataji mengi baada ya kunyakua mataji 17 tofauti kwenye soka la ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Kwenye ngazi ya klabu, Yaya Toure alipata mafanikio zaidi akiwa na kikosi cha Barcelona na Manchester City ambako alibeba mataji ya kutosha.

Alikuwapo pia Olympiacos ambako alibeba mataji mawili. Kwa sasa amerudi kwenye klabu yake hiyo ya zamani ya huko Ugiriki.

2.Didier Drogba- mataji 17

Supastaa Muivory Coast, Didier Drogba ni mmoja wanasoka wa Kiafrika waliopata mafanikio makubwa uwanjani. Fowadi huyo alikuwa sumu kubwa kwa mabeki wa timu pinzani akiwatesa kwa muongo mzima, akitamba sambamba na Samuel Eto’o wa Cameroon. Straika huyo wa zamani wa Chelsea alishinda mataji yote kwenye ngazi ya klabu ikiwamo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012. Kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Phoenix Rising FC akiwa mchezaji mmiliki. Drogba aliwahi kucheza pia Galatasaray.

1.Samuel Etoo- mataji 18

Staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon, Eto’o ndiye mwanasoka wa Kiafrika aliyebeba mataji mengi zaidi katika maisha yake ya kisoka. Amebeba mataji yote kwennye klabu yake na timu ya taifa isipokuwa Kombe la Dunia tu. Amecheza soka England, Hispania, Italia, Russia na Uturuki na kote huko amebeba mataji. Nyakati zake nzuri zaidi zilikuwa Barcelona na Inter Milan ambako alibeba mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili mfululizo.