Hii Madrid yakufikirika we tema mate chini

Thursday March 14 2019

 

MADRID,HISPANIA. HII ina maana Toni Kroos nje. Casemiro naye nje. Karim Benzema atasubiri huko kwenye benchi na Gareth Bale pia habari ndo hiyo hiyo.

Isco, Thibaut Courtois na Luka Modric itabidi tu wasubiri. Hicho ndicho watu wanachokifikiria baada ya Zinedine Zidane kurudi Real Madrid.

Lisemwalo ni kwamba Zidane atapewa nguvu ya kusajili mchezaji anayemtaka, jambo hilo linawafanya mashabiki wa timu hiyo kuanza kutengeneza kikosi chao cha kufikirika kwa vile atakavyorudisha Galacticos huko Bernabeu.

Mpango huo wa Zidane utawezeshwa na rais Florentino Perez. Kocha Zidane amewashtua watu baada ya kuamua kurejea Real Madrid ikiwa ni miezi isiyofika kumi tangu alipoamua kuachia ngazi mwishoni wa msimu uliopita baada ya kubeba Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo.

Real Madrid imekuwa timu ya kawaida sana kwa siku za karibuni tangu Zidane alipoachia ngazi, imetupwa nje kwenye kila michuano na suala la ubingwa limekuwa gumu kwao msimu huu. Hali mbayo imewafanya watimue makocha wawili ndani ya msimu mmoja. Walianza kwa kumfuta kazi Julen Lopetegui kabla ya kufanya hivyo tena kwa Santiago Scolari, aliyekuja kurithi mikoba na kudumu hapo kwa miezi minne.

Zidane sasa amerudishwa kwenye timu hiyo na Perez amekubaliana na matakwa yake ya kutaka kufanya matumizi makubwa kwenye kukifumua kikosi chote na kukifanya kuwa moto kabisa kwa ajili ya msimu ujao. Perez aligoma kufanya usajili wa wachezaji aliokuwa akiwataka Zidane mwishoni mwa msimu uliopita na ndio maana Mfaransa huyo aliamua kutimka zake.

Zidane amehakikishiwa pesa ya kusajili itakuwepo na Real Madrid ipo tayari kutumia pesa kwenye kusajili masupastaa wenye majina makubwa kwenye soka duniani.

Pesa haionekani kuwa tatizo kwa klabu hiyo ya Hispania hasa inapoamua kufanya mambo yake hasa kwa kipindi hiki inapokuwa na mpango wa kumtengenezea Zidane kikosi chenye vichwa matata kabisa vya mastaa wa soka duniani ili kumfanya Zidane kuwa na kila kitu anachokihitaji uwanjani.

Saa chache tu baada ya Zidane kurudi Bernabeu, tayari kumeanza kuvumishwa majina mbalimbali ya mastaa wa maana kabisa kwamba wameingia kwenye rada za Real Madrid na mwisho wa msimu huu kazi itakuwa moja tu, kunasa kichwa kimoja baada ya kingine.

Licha ya kwamba wamemsajili kipa Thibaut Courtois kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana tu hapo, staa huyo wa zamani wa Chelsea ameshindwa kuonyesha makali sana na hivyo, David De Gea amerudishwa tena kwenye orodha ya makipa wanaosakwa na Los Blancos.

De Gea bado hajasaini mkataba mpya huko Manchester United na hakuna ubishi Zidane ni shabiki mkubwa wa kipa huyo wa Hispania.

Safu ya mabeki kinachoonekana itabaki kuwa ilivyo na kutakuwa na mabadiliko kidogo tu, lakini pesa nyingi itatumika kwenye sehemu ya kiungo na washambuliaji.

N’Golo Kante anatajwa kuwa kiungo mkabaji bora kabisa duniani licha ya kocha Maurizio Sarri kumchezesha kwenye namba aliyoimudu huko Chelsea. Ni wazi atakuwa kwenye mpango wa Zidane, hasa ukizingatia Mfaransa huyo anataka kufanya mabadiliko makubwa kwenye sehemu ya kiungo, ambapo wakali kama Casemiro, Toni Kroos na Luka Modric wamechoka na wanapaswa kukaa nje.

Ukimweka kando Kante kwenye kiungo mpya ya Zidane, viungo wengine wanaotajwa huenda wakaja kuungana naye hapo Bernabeu ni Christian Eriksen wa Tottenham Hotspur na Paul Pogba wa Man United. Kumbuka Pogba alisema suala la kubaki au kuondoka Old Trafford atalifanya mwishoni mwa msimu huu.

Kurudi kwa Zidane huko Real Madrid kunaongeza uwezekano wa supastaa wa Stamford Bridge, Eden Hazard kwenda kujiunga na wababe hao wa Bernabeu, hasa ukizingatia yupo kwenye mpango wa kunaswa na timu hiyo na huko Chelsea anawagomea kusaini mkataba mpya.

Real Madrid imeweka wazi dhamira yao ya dhati ya kuwanasa mastaa wawili wa Paris Saint-Germain, Neymar na Kylian Mbappe na huenda ikafanya mchakato wa kuwanasa wawili hao wote kuhakikisha wanakwenda kurudisha nguvu kwenye kikosi cha Los Blancos na kutamba tena kwenye soka la Ulaya. Perez hajafuta mpango wa kuwanasa mastaa hao na hilo likifanikiwa basi kwenye ile fowadi yao kutakuwa na Hazard, Neymar na Mbappe – fowadi ambayo itakuwa sumu kwa beki yoyote ile duniani.

Hapo ina maana kwenye benchi lao kutakuwa na mastaa kama Vinicius, Casemiro, Kroos na Bale, ambapo ukikabiliana na Real Madrid itakuwa ndani moto, nje moto.

Advertisement