Hesabu za Ubingwa

Muktasari:

Zipo sababu kadhaa ambazo zinatoa taswira ya wazi kuwa Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa na namna ugumu ulivyo kwa timu nyingine ingawa katika soka lolote linaweza kutokea.

USHINDI wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi Jumanne katika Uwanja wa Taifa jijini, umeifanya Simba ifikishe pointi 59 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Ni matokeo ambayo yanaifanya Simba iwe na kibarua cha kusaka ushindi katika michezo 12 tu ili itwaye ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo.

Ushindi katika michezo hiyo 12 kati ya 15, utaifanya Simba ifikishe jumla ya pointi 95 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote inayoshiriki ligi hiyo.

Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 44 kabla ya mechi ya jana, ikiwa itapata ushindi michezo yake yote iliyosalia itamaliza na pointi 92.

Yanga yenyewe kwa sasa ina pointi 40 na ikiwa itapata ushindi katika mechi zote 17 zilizosalia, itakusanya jumla ya pointi 51 na hivyo itamaliza msimu ikiwa na pointi 91 . Kwa sasa sio muda sahihi kuitaja timu gani itatwaa ubingwa wa ligi kwani yoyote inaweza kuondoka na taji hilo.

Hata hivyo, kiuhalisia Simba ndio yenye nafasi kubwa ya kuibuka mabingwa wa msimu na ikiwa watashindwa kufanya hivyo itabidi ijilaumu yenyewe.

Zipo sababu kadhaa ambazo zinatoa taswira ya wazi kuwa Simba ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa na namna ugumu ulivyo kwa timu nyingine ingawa katika soka lolote linaweza kutokea.

Ratiba mteremko

Hesabu ya ubingwa ni mechi 12 lakini upo uwezekano kwa Simba kufanikisha lengo hilo bila hata kucheza idadi hiyo ya mechi.

Ikiwa itapa ushindi katika mechi mbili dhidi ya Yanga na Azam FC, maana yake itazidi kuziweka katika wakati mgumu timu hizo kwani wapinzani wake hao hawataweza kumaliza wakiwa na zaidi ya pointi 90 hivyo mlima unaweza kuwa mfupi kwa Simba.

Ukiondoa mechi hizo dhidi ya wapinzani wake katika mbio za ubingwa, Simba pia ina mechi chache ngumu ambazo bado ina nafasi ya kushinda ikiwa itatumia vyema udhaifu wa timu hizo ambazo ni Namungo, Prisons, Coastal Union na Polisi Tanzania.

Ni tofauti na Yanga ambao licha ya kuwa na mechi mbili ngumu dhidi ya Simba na Azam, pia ina kibarua mbele ya za Coastal Union, Namungo, Biashara United, Kagera Sugar, Lipuli na Mtibwa Sugar ambazo baadhi zilipata matokeo mazuri dhidi yake ugenini na nyingine zimekuwa na kiwango bora msimu huu. Na hata Azam ambayo ukiondoa kibarua cha kucheza na Ndanda ugenini jana na mbali na mechi mbili za Simba na Yanga pia itakuwa na mechi ngumu ugenini ambazo ni dhidi ya JKT Tanzania, Namungo, Biashara United, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Lipuli FC pamoja na Prisons.

Udhaifu wa Yanga, Azam

Azam na Yanga ndizo zinatafsiriwa kama washindani halisi wa Simba katika mbio za ubingwa wa ligi msimu huu tofauti na klabu nyingine kutokana na hali ya kiuchumi na maandalizi.

Hata hivyo, washindani hao wa Simba wameonekana kukosa mwendelezo wa kupata matokeo mazuri katika mechi zao tofauti na Simba ambayo imeonyesha uwezo wa kupata ushindi katika idadi kubwa ya michezo mfululizo. Yanga na Azam zimekuwa zikiangusha pointi muhimu hata katika viwanja vyao vya nyumbani tena dhidi ya timu zinazoonekana dhaifu jambo ambalo limekuwa likiziongezea ugumu katika mbio za ubingwa.

Mfano, Yanga ilipoteza pointi nne katika michezo miwili mfululizo nyumbani dhidi ya Mbeya City na Prisons baada ya kutoka nazo sare kama ilivyo kwa Azam FC ambayo imekuwa ikitoka sare nyumbani na hata kupoteza katika mazingira isiyotarajia kama ilivyofungwa mabao 2-1 na Coastal Union.

safu ya washambuliaji

Moja ya mambo yanayoibeba Simba msimu huu ni uwezo wa wachezaji wake katika kufumania nyavu wakitumia vyema nafasi ambazo wanatengeneza kulinganisha na Yanga na Azam.

Ushahidi wa hilo ni idadi ya mabao ambayo timu hizo zimefunga ambapo hadi sasa imepachika mabao 46, Azam ikifunga mabao 30 na Yanga ikifunga mabao 25.

Kocha wa zamani wa Yanga, Hans Pluijm amekuwa akisisitiza kuwa timu haistahili kuwa bingwa kama haifungi mabao mengi.

Ukuta mgumu

Simba ndio timu yenye safu imara zaidi ya ulinzi hadi sasa, kwani imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11 na inayofuatia ni Azam FC ambayo imefungwa mabao 14.

Safu imara ya ushambuliaji inakuwezesha kushinda mechi lakini safu imara ya ulinzi inakupa ubingwa.

Kikosi kipana

Simba imepita katika kipindi kigumu miezi ya hivi karibuni kwa kucheza ikiwa na kikosi kidogo kutokana na kuwa na kundi kubwa la wachezaji majeruhi.

Hata hivyo, imevuka vizuri kipindi hicho na ikaweza kuongoza msimamo wa ligi kwa tofauti kubwa ya pointi dhidi ya washindani wake ambao hawajakumbana na changamoto ya kuwakosa idadi kubwa ya nyota wao.

Kwa sasa Simba inaongoza huku idadi kubwa ya majeruhi wake wakiwa wanarejea uwanjani. Hiyo itaipa faida kwani itakuwa na fursa ya wachezaji wengine kupumzika na kujiimarisha vizuri zaidi katika kipindi ambacho timu zitalazimika kucheza idadi kubwa ya mechi ndani ya muda mfupi huku washindani wake wakinyemelewa na changamoto ya uchovu na majeraha.

Wasemavyo makocha wa Simba, Azam FC

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema kwa sasa hesabu yao kuu ni kupata ushindi katika kila mechi iliyo mbele yao.

“Ni jambo zuri tunaendelea kuongoza ligi na wachezaji wanafanya kile ambaco tunatakiwa kufanya. Hata hivyo, bado tunatakiwa tuendelee kufanya hivi katika mechi zinazokuja ili tuweze kutimiza lengo letu.”

Kocha msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche alisema bado timu yake inautolea macho ubingwa huo.

“Bado tunaamini nafasi ipo na ukiangalia pointi tulizonazo, uwezekano wa kuwafikia na kuwapita hao wanaoongoza ligi bado upo, hivyo jambo la msingi kwa sasa ni kupata ushindi katika mechi zetu halafu tuone mwishoni itakuaje,” alisema Cheche.

Senzo afafanua ubingwa

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ameelezea juu ya mipango yao ya ubingwa; “Tumepanga kila mechi iliyopo mbele yetu kuibuka na ushindi, ndiyo maana hata bonasi tunatoa kila timu inapofanya vizuri, hatuwezi kuweka wazi ni kiasi gani kinatolewa ila hii ipo tangu msimu uanze kwamba viongozi tuna wajibu wa kuwapa bonasi wachezaji wetu.

“Tunahitaji kuweka malengo na kushinda jambo ambalo tunaweza, tuna ratiba ngumu lakini tunaangalia jinsi gani tuweze kuwasafirisha wachezaji wetu pasipo kuchoka sana maana tuna mechi za ugenini Mbeya na Shinyanga ambako tunatacheza mechi ya Kombe la FA na Stand United.

“Yote haya tunayofanya huwa tunashirikiana na benchi la ufundi kuona ni namna gani tunaweza kuwasaidia wachezaji wetu maana lengo ni kutwaa ubingwa wa ligi na FA maana tunataka kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Senzo ambaye mi raia wa Afrika Kusini.