Hesabu za Sven ni Dodoma

Dar es Salaam. Kocha wa Simba SC, Sven Vandenbroeck amesema ushindi walioupata dhidi ya Gwambina wa mabao 3-0 unawaongezea morali katika mchezo wao ujao dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Sven alisema anataka kukiona kikosi chake kikiwa katika kiwamgo kikubwa zaidi katika mchezo wao ujao zaidi ya walivyocheza kwenye michezo miwili iliyopita.

“Wachezaji wote wamefanya vizuri na nina furaha katika hilo, lakini itakuwa vizuri tukiwa katika kiwango kikubwa zaidi kwenye mechi inayofuata kuhakikisha tunatoka na ushindi tena.

“Tutabadilika katika mbinu hatutoweza kucheza kama hivi lakini kuna nguvu ambayo nadhani tutaiongeza zaidi ya sasa,” alisema.

Sven alisema katika mchezo wao dhidi ya Gwambina walikutana na timu ngumu, ambayo ina ubora wa kutosha, lakini wachezaji wake walipambana.

“Walicheza vizuri, baadaye tukaamua kufunguka zaidi kwa kutumia mawinga na tulimiliki mpira hadi dakika 75 na hata zile 15 za mwisho,” alisema.

Kocha huyo alionyesha kufurahishwa na bao la mkwaju wa adhabu lililofungwa na Pascal Wawa katika mchezo huo

“Tulipata faulo na tuliitumia vizuri, ni jambo zuri hili baada ya muda mrefu kutofunga kupitia mipira ya adhabu,” alisema.

Akizungumzia viwango vya washambuliaji wake, Chris Mugalu na Meddie Kagere ambao wote walifunga katika mchezo huo, alisema hilo ni jambo zuri katika kikosi chake.

“Hili ni suala zuri linalonipa wakati wa kufanya uamuzi, hata ukiangalia kwenye bao la mwisho, Morrison alikuwa yupo na beki, lakini aliamua kumuangalia mwenzake,” alisema.

Mchezo ujao wa Simba utakuwa dhidi ya JKT Tanzania, ambao wanacheza leo dhidi ya Coastal Union ya Tanga.