Hesabu za Amunike kwa Samatta

Muktasari:

Alisema anafahamu ndoto ya Watanzania ni kufuzu Fainali za Afcon, hivyo yeye na wachezaji wake wanajipanga vizuri kuhakikisha wanaitimiza kupitia mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

KOCHA wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amefichua mbinu atakayoitumia kuimaliza Uganda keshokutwa Jumapili huku akitamba uwepo wa kundi kubwa la nyota wa kigeni chini ya nahodha Mbwana Samatta utamrahisishia kazi.

Alisema anafahamu ndoto ya Watanzania ni kufuzu Fainali za Afcon, hivyo yeye na wachezaji wake wanajipanga vizuri kuhakikisha wanaitimiza kupitia mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tunafahamu Uganda ni timu nzuri na imara lakini sio tishio kwetu. Wachezaji wangu wanajiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na wako sawa kiakili na kisaikolojia na kila wakati ninapozungumza nao wamekuwa wakionyesha furaha na hamasa.

Kimsingi siwezi kusema tutaingia kwa mbinu ya kujilinda au kushambulia. Tutakachokifanya ni kucheza kwa uwiano ulio sawa katika kutimiza majukumu hayo mawili na niwakumbushe kwenye mechi kunakuwa na nyakati ambazo mnakuwa juu, pia zile ambazo mnakuwa chini.

Kwa wachezaji morali ipo juu na ukizingatia nyota wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamefika kwa wakati na kuwa na mwitikio chanya naamini watakuwa chachu kwa wengins kikosini,” alisema.

Alisema anafahamu ubora wa Uganda hivyo mbinu pekee ya kupata ushindi dhidi yao ni kuwanyima uhuru wachezaji wao kwa kutowapa nafasi ya kumiliki sana mpira.

Nyota hao 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wanaongozwa na nahodha Mbwana Samatta anayecheza Genk ya Ubelgiji.

Wengine ni Rashid Mandawa (BDF XI), Hassan Kessy (Nkana), Saimon Msuva (Difaa el Jadida), Thomas Ulimwengu (JS Saoura), Farid Musa (CD Tenerife), Shaban Chilunda (CD Izarra), Himid Mao (Petrojet), Shiza Kichuya (ENPPI) na Yahya Zayd (Ismaily).