NYUMA YA PAZIA: Henderson wanatamani angekuwa Steven Gerrard

Tuna kila kitu ambacho maisha ya mwanadamu yanahitaji”. Aliwahi kusema Mwingereza mmoja mshairi akiisifu nchi yake, hasa Jiji la London. Sahau kuhusu New York, Hongkong, Paris, Milan na kwingineko. Waingereza wana ufahari huu.

Baada ya Liverpool kuukosa ubingwa wa England kwa miaka 30, hatimaye sasa wameupata, Waingereza wametamani watuchomekee mtu wao ambaye wanalazimisha aonekane alikuwa mtu muhimu kweli kweli katika kikosi cha Liverpool msimu huu.

Jordan Henderson. Waingereza wanajaribu kumweka katika bwawa moja la kuogelea na mastaa wengine wa Liverpool waliotwaa taji hili. Kina Sadio Mane, Mohamed Salah, Virgil van Dijk, Fabinho, Alisson Becker na wengineo.

Katika hao niliowataja, Henderson haogelei nao katika bwawa moja. Lakini Waingereza wanajaribu kumwingiza bwawani kwa sababu wanataka miaka kadhaa ijayo iingizwe katika kumbukumbu katika kikosi cha Liverpool kilichovunja mwisho wa miaka 30 bila ya kutwaa ubingwa, Jordan Henderson alikuwa staa wao.

Majuzi BBC wamemchagua kuwa mchezaji bora wa ms imu. Unajiuliza, kama Lionel Messi mwenyewe alimpigia kura Sadio Mane kuwa mwanasoka bora wa dunia, inakuaje Mane anakosa kuwa mwanasoka bora wa msimu?

Katika dunia nyingine ya nje, wanatambua Virgil van Dijk ni mwanasoka bora wa Ulaya. Katika dunia ya Waingereza wanadhani Henderson ndiye mwanasoka bora wa Ulaya na wa dunia. Katika hali ilivyo sasa Liverpool itashangaza kama Henderson anachaguliwa kuwa mwanasoka bora wa msimu wakati mwisho wa msimu Mane au Salah au VVD wanakwenda kuwania tuzo za mwanasoka bora wa dunia.

Unahodha wa Henderson unakuzwa zaidi lakini ukweli unabakia pale pale Waingereza wangetamani zaidi kama Steven Gerard angekuwa mchezaji wa Liverpool katika kikosi hiki. Wangepata uhalali kutoka katika dunia hii alikuwepo staa wao ndani ya kikosi cha mastaa.

Bahati mbaya Henderson hajawahi kufikia umuhimu wa Gerrard katika vikosi ambavyo Gerrard aliviongoza katika michuano mbalimbali enzi zake. Gerrard alizungukwa na mastaa wengi kutoka katika mataifa mbalimbali lakini bado alikuwa mchezaji staa zaidi.

Henderson amezungukwa na mastaa mbalimbali kutoka katika mataifa mbalimbali lakini wengi wao wamemfunika. Licha ya unahodha wake, bado anaweza kubakia kuwa mchezaji wa tatu wa Kiingereza kuwa na umuhimu katika kikosi hiki nyuma ya Trent Alexander Anorld na Andy Robertson.

Waingereza wanajua Gerrard ndiye aliyestahili hiki kinachotokea kuliko Henderson. Kama wangeweza kubadilishana nyakati basi Waingereza wengi wangenda kuona ikitokea Gerrard akicheza na kina Sadio Mane na kutwaa taji hili.

Kuna Waingereza wengi tunaona umuhimu wao au uhalali wao wa kupelekwa juu na vyombo vya habari vya Kiingereza pindi timu kubwa inapochukua ubingwa fulani. Achana na habari za Gerrard lakini vipi kuhusu John Terry na Chelsea yake?

Chelsea ilijaa mastaa wengi waliokuwa na umuhimu mkubwa. Hata mastaa wa Kiingereza kina Lampard walikuwepo. Lakini lilipokuja suala la John Terry kulikuwa hakuna ubishi wowote. Alikuwa nahodha halisi. Beki halisi. Kiongozi halisi.

Zipo nyakati ambazo tungeweza kuulizana licha ya umuhimu wa Didier Drogba kule mbele, maisha ya Chelsea yangekuwa vipi kama Terry asingeongoza safu ya ulinzi? Hiki ndicho ambacho kilitakiwa kizungumzwe kwa Henderson kwa sasa.

Sir Alex Ferguson aliwahi kuwa na Waingereza wa namna hii. Kina Roy Keane, Paul Scholes, David Beckham na wengineo. Tuliwaelewa licha ya ukweli vikosi vyake viliwahi kusheheni mastaa kibao wa kigeni. Hawa pia walikuwa nguzo.

Arsene Wenger aliwahi kuishi na mtu anayeitwa Tony Adams ‘Mr Arsenal’. Umuhimu wake ulikuwa wazi mbele ya mastaa wengi kama vile kina Dennis Bergkamp, Thierry Henry, Patrick Vieira na wengineo wengi.

Tottenham kama ilivyo, kama ingekuwa inatwaa mataji ni wazi nahodha, Harry Kane angekuwa katika sifa ambazo anastahili licha ya kuzungukwa na mastaa wengi wa kigeni katika klabu yake. Ana umuhimu pengine kuliko mchezaji yeyote kikosini kando ya Son.

Huu ustaa wa kulazimisha wa Henderson hauna uhalali. Nadhani kina Mane kama wangecheza chini ya Gerrard wenyewe wangehisi wamecheza chini ya mwanaume ambaye anastahili kuvaa kitambaa cha unahodha na anastahili kuwaongoza.

Kwa sasa unabakia kuwaonea huruma kina Mane. Kama Mane angekuwa Muingereza sasa hivi angekuwa anaimbwa vilivyo. Bahati mbaya kwake ni kijana aliyezaliwa Sedhiou pale Senegal na analazimika kuishi katika kivuli cha kina Henderson.

Hivyo hivyo, kwa mlingoti VVD. Naye analazimishwa kuishi katika kivuli cha Henderson ingawa ni wazi kama angekuwa ni Muingereza kwa sasa angekuwa anaimbwa katika hadhi za kina John Terry wa wakati ule.

Kama Liverpool na Manchester City wakitengeneza kikosi cha pamoja sioni kama kuna mchambuzi asiye wa Kiingereza ambaye anaweza kumpanga Henderson katika kikosi cha pamoja. Labda wale wachambuzi wa Kiingereza akina Jamie Carragher, Paul Merson, Gry Neville na wachache wengineo.

Kama ungetengeneza kikosi hicho huku Steven Gerrard akiwa katika ubora wake, basi ni wazi kwamba angecheza hilo la katikati na akina Kevin De Bruyne. Huu ndio ukweli halisi.