Henderson: Luis Suarez? Yule mtu hakika ningemuua

Muktasari:

Henderson, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 20 tu na alikuwa amecheza mechi moja tu kwenye Timu ya Taifa ya England, amefichua malumbano yake na Suarez, ambayo yalimfanya kuwa na hasira kutokana na kusimangwa sana mazoezini.

LIVERPOOL, ENGLAND . KIUNGO Jordan Henderson amefichua alikuwa yupo tayari kumuua Luis Suarez katika miaka yake ya mwanzoni Liverpool kwa sababu mshambuliaji huyo alikuwa akimwona mzigo tu mazoezini.

Henderson alitua Anfield kwa ada ya Pauni 20 milioni akitokea Sunderland kuelekea msimu wa 2011/12, lakini kwa wakati huo Suarez tayari alikuwa ameshatua Liverpool miezi sita kabla, aliponaswa akitokea Ajax kwenye dirisha la Januari 2011 na alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Kocha Kenny Dalglish.

Henderson, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 20 tu na alikuwa amecheza mechi moja tu kwenye Timu ya Taifa ya England, amefichua malumbano yake na Suarez, ambayo yalimfanya kuwa na hasira kutokana na kusimangwa sana mazoezini.

Henderson alisema: “Nilijaribu kujitahidi kwa kadiri nilivyoweza. Lakini ukiwa mwanasoka suala la kulaumiwa na watu ni jambo la kawaida. Kipindi kile, nilikuwa mchezaji mdogo na kuna jambo moja au mawili Luis aliyafanya mazoezini, sikuyapenda kabisa.

“Alinifanya nijione sifai kwamba sikustahili kufanya mazoezi pamoja naye. Alikuwa akirusharusha tu mikono kwamba hakupenda jinsi nilivyokuwa nacheza, kwamba sikustahili kuwapo kwenye timu hiyo. Iliniuma sana.

Alifanya hivyo mara tatu nilikasirika sana na nilikuwa tayari kumuua.” Henderson alisema uhusiano wake na Suarez ulikuja kuwa mzuri baada ya kumpigia pasi ya bao straika huyo. Wawili hao walibaki kuwa marafiki wazuri hadi Suarez alipoenda Barcelona mwaka 2014.