Hee! Kumbe Kagere achomoki Msimbazi kwa Sh1.2 Bilioni

Muktasari:

Wakala wa Meddie Kagere, Patrick Gakumba ameibuka na kukanusha taarifa zinazozagaa mitandaoni kuwa mchezaji wake amemalizana na Zamalek ya Misri kwa dau Sh1.2Bilioni.

Dar es Salaam.Pamoja kusambaa kwa tetesi kuwa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere amemalizana na Zamalek kwa dau la Sh1.2 Bilioni, Wakala wa nyota huyo Patrick Gakumba amesisitiza kuwa MK14 hachomoki Msimbazi.

Nyota huyo aliyejiunga na Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu ulioisha baada ya kutikisa nyavu mara 23 pia aliisaidia timu yake kufika robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akifunga mabao sita.

Wakala Gakumba alisema taarifa hizo zinazo zagaa mitandaoni kuwa mteja wake amemalizana na Zamalek ya Misri ili ajiunge nayo msimu ujao ni uzushi na hakuna ukweli wowote juu ya jambo hilo.

"Ni kweli nimepokea ofa kutoka Zamalek, lakini sijaikubali kwa sababu Kagere bado ni mchezaji halali wa Simba, timu yoyote inaruhusiwa kutangaza dau haijalishi amemaliza mkataba au laah, lakini kwa Kagere bado hajamalizana na Simba hivyo bado yupoyupo sana," alisema Gakumba.

Alisema sio Zamalek tu wanaohitaji huduma ya mshambuliaji huyo, pia TP Mazembe, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Raja Casablanca ya Morocco.

Alisema hana shaka na uwezo wa Mteja wake kwa sababu anajituma uwanjani na anauchu na mabao hivyo msimu ujao thamani yake itapanda mara dufu na bila shaka timu zote kubwa barani Afrika zitahitaji huduma yake.

Aliwataka Mashabiki wa Simba kuondoa hofu na kuendelea kumpa ushirikiano nyota huyo Mnyarwanda ili ajione kama yupo nyumbani kwa sababu sapoti yao itamfanya aongeze nguvu ya kuipambania zaidi timu yao.

"Mashabiki wa Simba waendelee kuchekelea tu kwa sababu Kagere bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba pia aliniambia anaipenda  timu hiyo kwasababu ana furaha sana kuchezea pale  hivyo msimu ujao atakuwepo na atakuja na moto wa hatari zaidi," alisema Wakala huyo.