He! Nuksi ya Drake inazidi kutesa vigogo Ulaya

Muktasari:

  • Usiku wa juzi Jumapili sasa ndio ilikuwa balaa ambapo Kurzawa akiwa na Drake ilianza kuwatisha mashabiki wa timu yake kabla ya kwenda kukumbana na kipigo hicho kizito kwenye ligi. Mara ya mwisho PSG kupokea kipigo kizito hivyo kwenye ligi ilikuwa mwaka 2000 waliporuhusu wavu wao kuguswa mara tano na Sedan.

PARIS, UFARANSA.NAKWAMBIA usipige picha na mwanamuziki Drake utajuta kujifahamu. Kama huamini, tena kawaulize Paris Saint-Germain ndio wahanga wa siku za karibuni kabisa na nuksi ya Drake baada ya juzi Jumapili kukumbana na kipigo kizito kwa mara ya kwanza kwenye ligi ndani ya miaka 19.

Vinara hao wa Ligi Kuu Ufaransa walichapwa 5-1 na Lille ikiwa ni muda mfupi tu tangu beki wao Layvin Kurzawa alipotuma picha yake kwenye mtandao wa kijamii ambayo alipiga na rapa huyo wa Canada mapema wiki iliyopita.

Drake ametajwa kuwa na nuksi baada ya hivi karibuni timu za Arsenal na Manchester City kukumbana na vipigo baada ya mastaa wao kuposti picha kwenye mitandao ya kijamii zilizowaonyesha wakiwa wamepozi na rapa huyo.

Arsenal walikumbwa na pigo kwenye mchakamchaka wao wa Top Four baada ya kuchapwa na Everton 1-0 siku chache baada ya straika wao Pierre-Emerick Aubameyang kupiga picha akionekana na Drake.

Man City wao walichapwa 1-0 na Tottenham kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya huku wakikosa penalti baada ya staa wao Sergio Aguero akiwa ameposti selfie aliyopiga na rapa huyo.

Usiku wa juzi Jumapili sasa ndio ilikuwa balaa ambapo Kurzawa akiwa na Drake ilianza kuwatisha mashabiki wa timu yake kabla ya kwenda kukumbana na kipigo hicho kizito kwenye ligi. Mara ya mwisho PSG kupokea kipigo kizito hivyo kwenye ligi ilikuwa mwaka 2000 waliporuhusu wavu wao kuguswa mara tano na Sedan.

Ulikuwa usiku mzito kwa PSG ambapo walianza kwa bao la kujifunga la Thomas Meunier ndani ya dakika ya saba tu ya mchezo, kabla ya kusawazisha kupitia kwa Juan Bernat dakika nne baadaye kabla ya kucheza pungufu mchezaji wao mmoja akionyeshwa kadi nyekundu na kilichofuatia baada ya hapo ni mvua ya mabao, Nicolas Pepe na Jose Fonte wakiwa miongoni mwa waliotikisa nyavu.

Drake atafanya shoo huko Amsterdam, Aprili hivyo mastaa wa Ajax wanaonywa kupiga picha na staa huyo la sivyo itakuwa kwao.