He! Guardiola apigwa vijembe

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA Felix Magath ameanzisha bifu na Pep Guardiola akimwambia kwamba si lolote hata mataji aliyobeba kwenye kikosi cha Barcelona ni ya Lionel Messi sio yake.

Guardiola ameshinda mataji matatu ya La Liga kwa misimu minne aliyokuwa Nou Camp kati ya 2008 na 2012.

Kutokana na hilo, Guardiola alisifiwa sana na kuitwa ‘genius’ kutokana na staili ya soka la kupiga pasi nyingi tiki-taka lililokuwa na uwezo wa kupenya ngome yoyote ile ya mabeki.

Lakini, Magath, 67, ameamua kumgeukia Guardiola na kumwambia kwamba mafanikio yale aliyopata akiwa kocha wa Barcelona hayakusababishwa na yeye, bali ni Messi.

Magath alisema: Messi ndiye aliyebeba mataji, sio Guardiola.

“Bila ya Messi, mfumo huu usingefanya kazi na kufanyikiwa chini ya Guardiola.

“Kama hilo sio, basi angebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Bayern Munich au Manchester City.

“Tiki-taka inafanya kazi kama tu una wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kupenya wapinzani. Kwa mtazamo wangu, Guardiola ameshapoteza makali yake na sasa anasuasua tu.”

Guardiola, 49, alishinda mataji ya Bundesliga kwa miaka yote mitatu aliyokuwa kwenye kikosi cha Bayern Munich.

Alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England akiwa na Man City, ambayo alitua mwaka 2016 huku ubingwa huo alinyakua kwenye misimu ya 2017-18 na 2018-19.

Msimu huu, baada ya mechi tatu - Man City ipo kwenye nafasi ya 14 ikiwa imeshinda mechi moja tu.

Kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, Man City ya Guardiola ilipambana sana kusaka huduma ya Messi kabla ya kubaki Nou Camp. Wamepanga kumsajili 2021.