He! Diego Costa kaliamsha dude

Muktasari:

Mshambuliaji huyo mwenye asili ya Brazil aliondoka Chelsea baada ya kutofautiana na kocha wake Antonino Conte, tangu ametua Atletico Madrid amekuwa na mafanikio makubwa

MADRID, HISPANIA.STRAIKA, Diego Costa ametishia kung'atuka Atletico Madrid na kutimkia zake China baada ya kushindwa kukubaliana na klabu yake juu ya mkataba mpya, akitaka alipwe mshahara sawa na mshambuliaji mwenzake, Antoine Griezmann.

Costa ameripotiwa kuwaambia Atletico kwamba kama mambo yatashindwa kwenda sawa basi ni heri achukue ofa za pesa ndefu za kwenda kufanya mambo yake huko Mashariki ya Mbali. Straika huyo wa Kihispaniola anaripotiwa kulipwa Pauni 7 milioni kwa mwaka huko Atleti.

Griezmann, ambaye alisaini mkataba mpya Juni mwaka huu ambapo utakwenda na kufika tamati 2023, anaweka kibindoni Pauni 17.5 milioni kwa mwaka.

Wachambuzi wa mambo wakaanza kuwachambua washambuliaji hao wawili na kuangalia ni haki Costa kuhitaji mshahara kama anaolipwa Griezmann.

Kwenye kikosi cha Atletico, Costa amecheza mechi 116 na kufunga mabao 46, wakati Griezmann amecheza mechi 151 na kufunga mabao 81.

Kwa rekodi hizo, ina maana Costa amecheza mechi 34 pungufu na amezidiwa mabao 35. Rekodi hizo hazikuachana, lakini takwimu za kimalipo zinaonekana Griezmann amemfunika Costa kwa Pauni 10.7 milioni kwenye mshahara wa mwaka. Mkataba wa Costa, aliyewahi kuichezea Chelsea utafika tamati 2021.