He! Bayern wanafanya magumashi kwa Sane

Saturday June 8 2019

 

MUNICH, UJERUMANI.BAYERN Munich inafanya ujanja ujanja kwenye mpango wao wa kumsajili winga wa Manchester City, Leroy Sane kwa kuwatumia wachezaji wenzake wa Ujerumani.

Sane kwa sasa yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani, ambako amejumuika na mastaa kibao wa kutoka Bayern Munich, ambapo mmoja wao, staa Joshua Kimmich alidai kwamba winga huyo wa Man City atafiti vizuri sana akihamia Allianz Arena.

Staa huyo anafikiria maisha yake ya sasa huko Man City baada ya kuwekwa sana benchi msimu uliopita na jambo hilo limemfanya aweke ngumu kidogo kwenye mpango wa kusaini mkataba mpya.

Beki wa Bayern, Kimmich alisema Sane atakwenda kuwa usajili mzuri kwenye kikosi hicho cha Bundesliga hasa ukizingatia kwamba kinataka kujijenga upya kufuatia kuondoka kwa masupastaa Franck Ribery na Arjen Robben.

“Ningependa sana tuwe na Leroy pale Bayern, hilo litakuwa limetuma ujumbe mwafaka,” alisema beki huyo wa kulia na kuongeza

“Ni mchezaji atakayefiti Bayern. Ni mchezaji mzuri sana. Lakini, nashangaa kwani hata hakupewa nafasi ya kutosha kuichezea Man City msimu uliopita. Kama ningekuwa bosi wa klabu, basi ningefanikisha usajili wake.”

Advertisement

Bayern walidai kwamba hawatapeleka ofa ya kumnasa Sane mwenye mkataba wa miaka miwili huko Man City, labda kama tu mchezaji mwenyewe atawaambia wafanye hivyo.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola hayupo tayari kumpoteza Sane kirahisi licha ya kwamba kwenye kikosi chake kuna mawinga wengine moto kama Raheem Sterling, Riyad Mahrez na Bernardo Silva. Mabosi wa Man City bado wanawasikilizia wale wa Bayern Munich kuhusu dili hilo la Sane.

Advertisement