He! Abramovich alivyolipa pesa kibao kwa makocha

Muktasari:

  • Makocha wengine waliolipwa pesa zinazokaribia na hizo ni Claudio Ranieri, ambaye alilipwa Pauni 6 milioni mwaka 2004 sawa na ilivyokuwa kwa Carlo Ancelotti alipotimuliwa mwaka 2011, ambapo alipewa mkwanja wa Pauni 6 milioni.

LONDON, ENGLAND . MAURIZIO Sarri. Kitu ambacho anaweza kukifanya kwa sasa ni kukusanya tu mabegi yake kujiweka tayari kwa ajili ya kusubiri kufukuzwa tu. Kichapo kingine chochote kitakachofuatia, hasa kwenye ile mechi ya fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Manchester City, haiwezi kukiacha salama kibarua chake huko Stamford Bridge.

Bilionea Roman Abramovich hatazamwi kama ataendelea kuwa na uvumivu baada ya hapo. Kitu kingine ni kwamba hata gharama za Sarri kufukuzwa kazi ni ndogo kuliko za makocha wengine wote waliowahi kufanya kazi kwenye kikosi cha Chelsea na kufukuzwa. Kinachoelezwa ni kwamba Sarri akifukuzwa, fidia atakayolipwa ni Pauni 5 milioni tu.

Hiyo ni fidia ndogo zaidi kuwahi kulipwa kwa makocha wote waliowahi kufanya kazi kwenye kikosi cha Chelsea chini ya bilionea huyo wa Russia. Sarri atalipwa fidia ndogo kuliko hata aliyolipwa Avram Grant, wakati alipofukuzwa 2008, ambapo alilipwa Pauni 5.5 milioni.

Makocha wengine waliolipwa pesa zinazokaribia na hizo ni Claudio Ranieri, ambaye alilipwa Pauni 6 milioni mwaka 2004 sawa na ilivyokuwa kwa Carlo Ancelotti alipotimuliwa mwaka 2011, ambapo alipewa mkwanja wa Pauni 6 milioni.

Hizi hapa fidia kubwa zaidi Abramovich aliwalipa makocha waliokuja kuinoa Chelsea baada ya kuwafuta kazi. Kwa ujumla wake, Abramovich ametumia Pauni 89.3 milioni kulipa makocha aliowafukuza kazi.

6. Antonio Conte – (2018, Pauni 9 milioni)

Mtaliano, Antonio Conte ndiye wa mwisho kufutwa kazi huko Chelsea baada ya mambo kwenda kombo. Kocha huyo alifukuzwa Julai 2018 na nafasi yake kuja kuchukuliwa na Sarri. Wakati Conte anafungasha virago vyake na kuondoka Stamford Bridge alilipwa fidia ya Pauni 9 milioni.

5. Jose Mourinho – (2015,Pauni 9.5 milioni)

Mreno, Jose Mourinho kwa sasa anahusishwa tena na mpango wa kurudi Chelsea na hiyo itakuwa mara ya tatu. Mara mbili alizokuwa kwenye timu hiyo, zote alifukuzwa kazi. Awamu yake ya pili, alifukuzwa kazi Novemba 2015 baada ya timu kufanya hovyo. Hata hivyo, jambo hilo limemwingizia pesa Mourinho, kwani alilipwa Pauni 9.5 milioni fidia.

4. Roberto Di Matteo – (2012, Pauni 10.7 milioni)

Staa wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Matteo alirudi kuinoa timu hiyo Machi 2012, lakini hadi kufika Novemba 2012 akafutwa kazi. Miezi yake minane aliyokuwa kwenye timu hiyo, Di Matteo aliisaidia timu kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Di Matteo alianza kama kocha wa muda, kabla ya kupewa mkataba wa kudumu na alipofukuzwa kazi, alilipwa fidia ya Pauni 10.7 milioni.

3. Andre Villas-Boas – (2012,Pauni 12 milioni)

Mreno mwingine huyo aliyepata nafasi ya kunoa Chelsea. Baada ya kunaswa na mabingwa hao wa Stamford Bridge, maisha ya AVB kwenye timu hiyo yalikwenda kuishia Machi 2012, ambapo alifutwa kazi baada ya mambo kwenda hovyo. Hata hivyo, AVB hakuondoka Chelsea mikono mitupu, kwani amekuwa mmoja wa makocha waliolipwa fidia kubwa, aliondoka akilipwa Pauni 12 milioni na bilionea Abramovich.

2. Luiz Felipe Scolari – (2009, Pauni 12.6 milioni)

Akiwa na rekodi tamu kabisa ya kutoka kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2002 akiwa na kikosi cha Brazil, bilionea Abramovich alimwona Mbrazili Luiz Felipe Scolari anafaa kwenye kuinoa timu yake, akampa kazi na bahati mbaya mambo yakamshinda. Scolari hakudumu muda mrefu kwenye timu hiyo na Februari 2009 akafutwa kazi. Hata hivyo, haikuwa aibu ya bure, kwa kitendo hicho cha kufutwa kazi, Scolari alilipwa fidia ya Pauni 12.6 milioni na bilionea huyo wa Stamford Bridge.

1. Jose Mour inho – (2007, Pauni 18 milioni)

Katika awamu yake ya kwanza Jose Mourinho huko Chelsea alipata mafanikio makubwa kabla ya kukumbana na rungu la kutimuliwa. Mourinho alitua Stamford Bridge 2004, akawapa ubingwa wa Ligi Kuu England mara mbili mfululizo kabla ya mambo kutibuka 2007 na ilipofika Septemba tu mwaka huo, alifutwa kazi. Kupoteza ajira hakujakuwa pigo sana kwa Mourinho, kwani alilipwa fidia ya Pauni 18 milioni kama fidia ya mkataba wake kuvunjwa kabla ya kufika mwisho.