Hazard ni shida Stamford Bridge

Sunday May 12 2019

 

By LONDON, ENGLAND

CHELSEA wanafanya kila njia kumfurahisha supastaa wao Eden Hazard ili abaki kwenye kikosi chao baada ya usiku wa juzi Ijumaa kumpa tuzo mbili za ubora kikosini hapo.
Staa huyo wa Ubelgiji amekuwa akihusishwa na mpango wa kutimkia Real Madrid katika dili linaloweza kutimia kwa ada ya Pauni 100 milioni. Lakini, Hazard baada ya kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa timu hiyo pamoja na ile ya bao bora la msimu, aliulizwa kama atasaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Stamford Bridge.
Hazard alijibu: "Iko wapi peni?".
Mashabiki wa Chelsea wameripotiwa kufurahishwa na jambo hilo, lakini walitumia kurasa zao za siku kuhoji kwanini hakupewa peni haraka asaini ili waondokane na presha ya kumpoteza staa wao. Hata hivyo, shabiki mwingine alikuwa na mtazamo tofauti akisema maneno hayo ya Hazard ni ya kuwanyanyasa tu.
Mkataba wa Hazard utafika tamati mwishoni mwa msimu wa 2020, lakini kutokana na Chelsea kutumikia adhabu ya kuzuiwa kusajili kwa kipindi cha mwaka mmoja, jambo hilo linawafanya kuweka nguvu katika kumwaachia staa huyo aondoke kwa sababu hawatakuwa na nafasi ya kusajili nyota mpya wa kuja kuziba pengo lake.
Baadhi ya mashabiki waaamini kwamba Hazard hatasaini dili jipya kwenye timu yao, isipokuwa ataendelea kubaki hapo Stamford Bridge ili kuokoa Pauni 100 milioni za Real Madrid, ambapo atakapokwenda kujiunga nao bure mwishoni mwa msimu ujao atakwenda kulipwa mshahara mara mbili ya kiwango anachovuna kwa sasa kwenye kikosi cha The Blues. Kama Hazard akibaki Chelsea atakuwa na ruhusa ya kusaini mkataba wa awali na Real Madrid itakapofika Januari mwakani.

Advertisement