Hazard kaogopa namba ya Ronaldo hapo Real Madrid

Muktasari:

Huko Bernabeu, namba 7 kwa sasa inavaliwa na mchezaji Mariano Diaz, ambaye tangu atue kwenye kikosi hicho ameshindwa kabisa kucheza soka kwa kiwango cha juu na kuonekana kuwa mzigo tu.

MADRID, HISPANIA.SUPASTAA, Eden Hazard ameonywa asithubutu kuchukua jezi namba 7 iliyokuwa ikivaliwa na Cristiano Ronaldo huko Real Madrid kukwepa majanga.

Badala yake, winga huyo matata kabisa anapokuwa uwanjani, ameamua kuchagua kuvaa jezi namba 23, ambayo iliwahi kutumiwa na Mwingereza, David Beckham alipokuwa kwenye kikosi hicho.

Hazard, anataka kutengeneza utawala wake tofauti na ule wa Ronaldo huko Bernabeu, lakini uamuzi wa kuachana na jezi yenye namba 7 ni jambo la kuogopa tu kukumbana na mzimu wa namba hiyo iliyokuwa ikitumika na mchezaji aliyefanya mambo mengi mazuri katika timu hiyo.

Huko Bernabeu, namba 7 kwa sasa inavaliwa na mchezaji Mariano Diaz, ambaye tangu atue kwenye kikosi hicho ameshindwa kabisa kucheza soka kwa kiwango cha juu na kuonekana kuwa mzigo tu.

Kwa mujibu wa Marca, staa huyo wa zamani wa Chelsea ni mpenzi mkubwa wa NBA, hivyo ameamua kuchukua namba 23 kwa sababu ilikuwa ikivaliwa na mastaa wa maana kwenye ligi hiyo ya mpira wa kikapu huko Marekani kama vile Michael Jordan, huku staa LeBron James naye anavaa namba 23 huko LA Lakers.

David Beckham alipotua Madrid alichaguliwa namba hiyo kwa ajili ya Jordan. Hazard alipokuwa Stamford Bridge alikuwa akivaa jezi namba 10, lakini huko Madrid, amekuta inavaliwa na Mwanasoka Bora duniani kwa sasa, Luka Modric.

Real Madrid wao hawajali kuhusu namba ya mgongoni atakayovaa staa wao waliyemnasa kwa pesa nyingi, wanachojali ni namba za mabao na nafasi atakazotengeneza atakapokuwa uwanjani.