Hazard awaponza Chelsea kinoma

Muktasari:

 

  • Matatizo ya Chelsea yanatokana na timu hiyo kukosa mizani sawa katika kiungo kilichoundwa na Jorginho, Ross Barkley na N'Golo Kante

London, England. Chelsea inaponzwa na kumtegemea Eden Hazard kupita kiasi na ndiyo chanzo cha matokeo mabaya ya klabu hiyo ya London, kwa mujibu wa kiungo wa zamani wa Liverpool, Graeme Souness.

Kukosolewa huko kumefuatia kipigo cha 2-0 walichopata Chelsea kutoka kwa Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park, licha ya kutawala kipindi cha kwanza cha mechi yao hiyo ya Ligi Kuu England.

Straika Richarlison alifunga kwa kichwa na Gylfi Sigurdsson akamalizia vyema penalti yake iliyopanguliwa na Kepa Arrizabalaga na kuwapa Everton ushindi wao wa kwanza dhidi ya Chelsea kwa zaidi ya miaka miwili.

Ushindi uliwainua Everton hadi katika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu England na kuifanya Chelsea kupoteza mechi yao ya saba EPL msimu huu.

Souness amesema matatizo ya Chelsea yanatokana na timu hiyo kukosa mizani sawa katika kiungo kilichoundwa na Jorginho, Ross Barkley na N'Golo Kante – ambao msimu huu wamefunga jumla ya magoli nane tu msimu huu.

"Kumtegemea Hazard afanye makubwa kila siku ni ngumu sana kwake. Mnapaswa kushirikiana kutegeneza magoli kutoka pande zote za uwanja," alisema Souness.