Hazard arejesha mzuka Madrid

MADRID, HISPANIA. Kocha wa  Real Madrid, Zinedine Zidane amesema nyota wake  Eden Hazard anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha timu yake kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach, leo Jumanne Oktoba 27, 2020.

Hazard amekuwa akikumbana na majeraha ya mara kwa mara tangu atue Santiago Bernabeu akitokea Chelsea 2019 amecheza michezo 22 tu chini ya Zidane msimu uliopita na kufunga bao moja.

"Hazard kuwa nasi ni kwa sababu yupo sawa na hiyo ni taarifa njema kwetu. Tunafuraha kumwona  yupo nasi," amesema Zidane.

"Nadhani tutaona vile ambavyo atatumika. Natambua kuwa msimu mrefu hivyo nitahitaji mchango wa kila mmoja, huo ni ukweli na nimekuwa nikilisema hilo," amesema na kuongeza

"Ipo wazi kuwa tumekuwa na tatizo upande wa mawinga lakini wapo wachezaji ambao wanaweza kuonyesha kwetu sio tatizo kubwa."

Borussia M'gladbach  ambao ni wapinzani wa Real Madrid kwenye mchezo wa leo, hawajapoteza mchezo hata mmoja kati ya michezo mitano ya mwisho kucheza kwenye mashindano yote.

Katika mchezo wao wa mwisho walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Inter Milan kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Upande wake  Zidane ataingia kwenye mchezo huo huku vijana wake wakiwa na morali ya ushindi wa mchezo wao uliopita  kwenye  El Clasico, licha ya kwamba waolianza kwa kupoteza kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk.

MECHI ZA UEFA-JUMANNE

Kundi  A
Lokomotiv Moscow vs Bayern Munich
Atletico Madrid vs  Salzburg

Kundi  B
Shakhtar Donetsk vs Inter
Borussia Moenchengladbach vs Real Madrid

Kundi C
FC Porto vs Olympiacos
Marseille vs Manchester City

Kundi  D
Atalanta vs Ajax
Liverpool vs FC Midtjylland