Hazard achefuliwa na majeraha

MADRID, HISPANIA. KOCHA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema mchezaji wake  Eden Hazard amepoteza furaha kutokana na majeraha ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yanamuandama tangu ajiunge na miamba hiyo mwaka 2019.

Hazard ambaye alijiunga na Real akitokea Chelsea kwa dau la Euro 130 milioni, ameshindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa ambapo msimu uliopita alifunga bao moja kabla ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu.

Mbelgiji huyo alianza kuonyesha kiwango kikubwa katika maandalizi ya msimu na mechi mbili za mwanzo za La Liga kabla ya kupata majeraha ya misuli wakati wa maandalizi ya mchezo dhidi ya Real Valladolid, juzi Jumatano.

Madrid ilicheza mechi hiyo bila Hazard kuwepo uwanjani na ikashinda bao 1-0. Baada ya mchezo  Zidane alisema hajajua ni kwa muda gani mchezaji huyo atakaa nje na kuongeza kwamba Hazard amekuwa akikerekwa sana na majeraha hayo ya mara kwa mara.

“Siwezi kusema ni muda gani itamchukua hadi kupona, alipata maumivu katika mazoezi ya maandalizi ya mchezo huu,” alisema.

“Amekuwa anakaa sana nje kutokana na majeraha ya mara kwa mara, ingawa sio majeraha ambayo yanaweza kumuweka nje kwa muda mrefu, lakini amechukizwa sana na jambo hili kwa sababu alishapona kabisa kutoka kwenye majeraha yake ya hapo awali,” aliongeza.

Ripoti kutoka tovuti ya ESPN zinadai majeraha hayo yanaweza kuchukua muda wa wiki tatu hadi nne kupona, jambo ambalo litamfanya kukosa mechi mbili za La Liga dhidi ya Levante na Cadiz CF, lakini anaweza kucheza El Classico dhidi ya Barcelona.