Hazard, Mourinho hatihati kukutana Madrid

Muktasari:

Maneno ya Hazard kuhusu Mourinho yameibua vuguvugu la kwamba huenda wawili hao wakakutana na kufanya kazi pamoja huko Bernabeu na si Old Trafford.

WACHUNGUZI wa fitina za soka Barani Ulaya wamekaa kikao na kuichunguza kauli ya staa wa Chelsea, Eden Hazard kwamba yupo tayari kufanya kazi tena na kocha, Jose Mourinho na wamegundua kitu.
Mtu mmoja mtundu amedai kauli ya Hazard inaashiria kwamba amejiandaa kufanya kazi tena na kocha huyo wa Manchester United kwa sababu anahisi wanaweza kukutana Real Madrid miezi michache ijayo.
Shaun Custis, Bosi wa michezo wa gazeti la The Sun la Uingereza amedai, Hazard amejiandaa kufanya kazi na Mourinho ndani Santiago Bernabeu kwa sababu anaona kuna mwelekeo wa wawili hao kukutana Hispania.
Wakati Real Madrid wakijiandaa kumchukua Hazard katika dirisha kubwa la majira ya joto, inasemekana kwamba klabu hiyo pia imekuwa ikimfikiria Mourinho endapo wataamua kuachana na kocha wao wa sasa, Julen Lopetegui ambaye amekuwa akiwapatia matokeo mabovu.
“Inavutia jinsi ambavyo jambo lenyewe lilivyo. Hazard  Amesema angependa kucheza chini ya Jose tena, lakini muda si mrefu kutakuwa na nafasi ya kazi pale Real Madrid. Na kama Manchester United haitafanya vizuri kutakuwa na nafasi ya kazi pale. Rais wa Madrid na Jose ni watu wa karibu.”
“Kulikuwa hakuna uadui wakati Mourinho alipoondoka na siku zote alimtaka abakie. Ni Mourinho ndiye aliyeamua kuondoka, hivyo kuna uwezekano Mourinho akarudi Madrid na Hazard akajiunga naye.” Alisema Curtis.
Hazard alikuwa mmoja kati ya wachezaji ambao walishutumiwa kucheza ovyo katika msimu wa mwisho wa Mourinho pale Chelsea 2015/16 ikiwa ni miezi michache baada ya timu hiyo kuchukua ubingwa huku Hazard akifunga mabao 19 kuelekea katika taji.
Curtis amehoji ni kwanini kwa sasa Hazard anaonekana kuwa tayari kufanya kazi tena na mtu ambaye kwa kiasi kikubwa aliondoka na hisia Stamford Bridge kwamba yeye ndiye ambaye amechangia kumfukuzisha kazi
“Sielewi kwanini Hazard anasema hivyo. Walichokifanya kilikuwa wazi sana. moja kati ya sababu ambazo, Hazard anakosolewa kwamba hafikii kiwango cha akina Messi ni kwa sababu hafanyi mambo makubwa kila msimu. Kulikuwa na misimu miwili pale hakuonyesha juhudi zozote na anahitaji mwendelezo wa ubora. Je sasa hivi anafanya vema kwa sababu anaandaa mazingira ya kufanya kazi kwingine?” alihoji Curtis.
Hazard anatajwa kuwa mrithi wa kudumu wa staa wa zamani wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo ambaye aliondoka kwenye klabu hiyo katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto kwenda Juventus kwa dau la pauni 88 milioni na kuanzia hapo wamekuwa hawafanyi vema katika mechi zao mbalimbali.
Hazard ambaye ni staa wa kimataifa wa Ubelgiji amekiri kwamba anavutika na mpango wa kwenda Bernabeu ingawa hatafanya hivyo katika dirisha la Januari na mpaka sasa ameshindwa kukubali ofa ya kusaini mkataba mpya Stamford Brigde.
Kwa upande wa Mourinho, kocha huyo alikaribia kufukuzwa wikiendi iliyopita lakini kibarua chake kilisalimika baada ya timu yake kucheza kishujaa katika pambano dhidi ya Newcaste ambalo walishinda kwa mabao 3.
Hata hivyo hatima ya kocha huyo bado ipo shakani endapo United itaendelea kuyumba kuanzia katika pambano kali dhidi ya Chelsea wanalotazamiwa kucheza Jumamosi mchana ugenini katika Uwanja wa Stamford Bridge ambapo Mourinho anatazamiwa kukumbana na makali ya Hazard.
Mpaka sasa United imeachwa pointi saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya England na viongozi wa Ligi hiyo watani zao Manchester City ambao wana pointi 20 huku wao wakiwa na pointi 13 wakishika nafasi ya nane.

SUMMARY
Maneno ya Hazard kuhusu Mourinho yameibua vuguvugu la kwamba huenda wawili hao wakakutana na kufanya kazi pamoja huko Bernabeu na si Old Trafford.

...