Hazard, Eriksen hao Madrid mtawakoma!

Monday January 14 2019

 

MADRID, HISPANIA.REAL Madrid imeweka mkakati kabambe kabisa wa kuvamia kwenye Ligi Kuu England na kuchota viungo wawili matata wa kushambulia ili kukifanya kikosi chake kuwa tishio huko Santiago Bernabeu.

Ripoti kutoka England zinadai, Los Blancos wanapiga hesabu za kumnasa staa wa Chelsea, Eden Hazard na supastaa wa Tottenham Hotspur, Christian Eriksen.

Mastaa hao wawili matata kabisa kwenye Ligi Kuu England wamewekwa kwenye rada za Real Madrid ili kwenda kuifanya kuwa tishio kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mpango wote wa kuwanasa wachezaji hao utafanywa mwishoni mwa msimu.

Ofa yake kwa kila mchezaji itaanzia Pauni 50 milioni, huku mabingwa hao wa Ulaya wakiamini kuwa lazima tu ofa zao za kwanza zitagomewa, lakini wataendelea na mchakato wao wa kuwanasa wakali hao.

Wachezaji wote hao mikataba yao itafika tamati mwishoni mwa msimu ujao, hivyo Spurs na Chelsea zipo kwenye hatari ya kuwapoteza mastaa wao kwa pesa kiduchu kama watashindwa kuwasainisha mikataba mipya.

Real Madrid jana Jumapili ilitarajia kuifuata Real Betis kwenye mchezo wa La Liga, huku mabingwa hao mara 13 wa Ulaya wakiwa wameachwa pointi kibao na mahasimu wao vinara, Barcelona.

Advertisement