Haya ya Azam FC hata Yanga yaliwakuta

Muktasari:

Katika mechi 30 za msimu mzima, Azam FC ilishinda mechi 14, ikapoteza 6 na kuambulia sare mara 10. Jumla walimaliza ligi wakiwa na alama 52. Msimu uliofuata baada ya kuondoka kwao, Azam FC ilimaliza katika nafasi ya pili, ikishinda michezo 16 na kupoteza miwili. Ikatoka sare mara 10 na kuvuna pointi 58.

Azam FC ilipoamua kuanchana na nyota wake watano muhimu; Aishi Manula,  Shomary Kapombe, Gadiel Micheal, Erasto Nyoni na John Bocco, watu wengi waliibeza timu hiyo na kuona wamefanya uamuzi wa hovyo zaidi kuwahi kufanyika kwenye mpira.
Kiwango ambacho wachezaji hao walikionesha kwenye timu zao mpya, kiliongeza ukubwa wa sauti za wakosoaji wa uamuzi ule wa Azam FC.
Lakini Azam FC wenyewe hawakuwa na maneno mengi kutetea uamuzi ule zaidi ya kuacha wakati uamue kwa sababu hakuna hakimu mtenda haki duniani kama wakati.
Msimu wa 2016/17 ambao ulikuwa wa mwisho kwa wachezaji hao wakiwa pale Chamazi, klabu yao ilimaliza ligi ikiwa katika nafasi ya nne, nafasi mbaya zaidi kwao tangu msimu wao wa kwanza kwenye Ligi Kuu, 2008/09 walipomaliza katika nafasi ya nane.

Katika mechi 30 za msimu mzima, Azam FC ilishinda mechi 14, ikapoteza 6 na kuambulia sare mara 10. Jumla walimaliza ligi wakiwa na alama 52.

Msimu uliofuata baada ya kuondoka kwao, Azam FC ilimaliza katika nafasi ya pili, ikishinda michezo 16 na kupoteza miwili. Ikatoka sare mara 10 na kuvuna pointi 58.

Hii ilikuwa na maana kwamba, timu hiyo iliimarika bila wachezaji wale. Walishinda mechi mbili zaidi ya zile walizoshinda msimu uliotangulia. Walipoteza mechi nne pungufu ya zile walizopoteza msimu uliotangulia, na walivuna alama sita zaidi ya zile walizovuna katika msimu uliotangulia.
Haya yote yalipatikana baada ya wachezaji wale kuondoka.
Msimu huu, katika mechi 12 za mwanzo, Azam FC imeshinda mechi 9 na kutoa sare 3 na haijapoteza.
Haya yote yana maana kwamba Azam FC walifanya maamuzi sahihi kwa faida yao na kadri wakati unavyozidi kusonga, ukweli huu utazidi kujidhihirisha.
Hoja hapa siyo wachezaji wale wanafanya nini huko waliko, bali Azam FC inafanya nini bila wao.
Tuliona kilichowatokea Simba baada ya kuondokewa na wachezaji wake muhimu msimu wa 2011/12.
Haruna Moshi, Kelvin Yondani, Felix Sunzu na Patrice Mafisango (RIP) kuwataja kwa uchache.
Licha ya kuanza msimu kama mabingwa watetezi, walijikuta wakimaliza ligi katika nafasi ya tatu. Na waliendelea kuporomoka hadi kumaliza nafasi ya 4 msimu uliofuata.
Nani kasahau kilichowakuta Tukuyu Stars 1987? Waliuanza msimu kama mabingwa watetezi lakini wakashuka daraja baada ya kuondokewa na wachezaji wao muhimu.
Hata Yanga wanayajua madhala ya kuondokewa na wachezaji muhimu. 1977 walikutana na kipigo cha fedheza cha mabao 6-0 kutoka kwa Simba baada ya kuondokewa na wachezaji muhimu.
Lakini hiyo haipo kwa Azam FC. Badala ya kukutwa na balaa, ndiyo wapo kwenye neema zaidi.
Hii ni kwa sababu, walijua wanachokifanya na sasa wanavuna walichokipanda.
Namba huwa haziongopi. Kwa namba hizi za Azam FC, ni wazi kwamba klabu ilijua ilichokuwa ikikifanya ilipoamua kuwaruhusu wachezaji wale wakatafute maisha mapya kwingine.
Yule hakimu ‘wakati’ ambaye Azam FC walisubiri aje aamue kesi yao, ameshaanza safari yake na muda si mrefu majibu yatatoka.