Haya ndio maisha ya Burundi

Muktasari:

Gazeti hili linakuletea orodha ya mambo manane (8) kuhusu nchi ya Burundi ambayo yanaweza kumpa taswira halisi Mtanzania kuhusu majirani zao hao.

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilikuwa nchini Burundi kuumana na timu ya taifa ya nchi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Intwari (Mashujaa), juzi Jumatano, Septemba 4.

Mwanaspoti lilikuwa ni miongoni mwa vyombo vya habari ambavyo vilifunga safari kutoka Tanzania hadi Burundi kwa ajili ya kuripoti mchezo huo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 zitakazofanyika Qatar.

Zaidi ya waandishi 30 walisafiri kutoka Tanzania hadi Burundi kwa kutumia usafiri wa basi.

Ukiondoa kile kilichojiri ndani ya uwanja, yapo mambo ya nje ya uwanja ambayo pengine Mtanzania wa kawaida anaweza kutofahamu kuhusu nchi ya Burundi.

Gazeti hili linakuletea orodha ya mambo manane (8) kuhusu nchi ya Burundi ambayo yanaweza kumpa taswira halisi Mtanzania kuhusu majirani zao hao.

Mishikaki dili

Moja ya biashara ambazo zina mwitikio mkubwa wa wateja ni ile ya nyama za kuchoma ambazo hukatwa vipande vipande na kuchomekwa kwenye vijiti maarufu kama mishikaki.

Kama ilivyo Tanzania ambako kuna maeneo ambayo watu hukusanyika kununua nyama ya kuchoma au kukaanga ndivyo ilivyo Burundi ambako sio jambo la kushangaza kuona baa au eneo wanalouza mishikaki tu.

Baadhi ya maeneo, hutoa ofa ya ndizi moja bure kwa kila mshikaki mmoja ambao mteja ananunua.

Filimbi kuongoza msafara

Imezoeleka kwenye nchi mbalimbali misafara ya viongozi, timu au wageni wa kimataifa kuongozwa na magari au pikipiki za Jeshi la Polisi kama ishara ya kutaka watumiaji wengine wa barabara kupisha wakati msafara unapopita.

Hata hivyo ni tofauti na Burundi ambako msafara licha ya kuongozwa na gari la askari, wenyewe hawatumii ving’ora bali filimbi ambayo inapulizwa na askari ili kuwapa wengine ishara ya kukaa pembeni.

Bunduki kila kona

Pengine kutokana na matatizo na migogoro ya kisiasa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo Burundi wamepitia, suala la usalama limekuwa likichukuliwa kwa uzito mkubwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hiyo.

Kutokana na hilo, sio jambo la kushangaza kuona askari wakiwa na mitutu ya bunduki hata katika kumbi za starehe, mitaani na kwenye maeneo mengine.

Lugha jipange

Warundi wanazungumza Kifaransa, Kiswahili na lugha ya kwao na wengi hawafahamu vyema Kiingereza.

Lakini pamoja na kuzungumza Kiswahili, unaweza kupata wakati mgumu kuwaelewa au kuwaelezea jambo pindi unapozungumza nao kwani hawaifahamu kiundani kama ilivyo kwa Watanzania.

Dawa bei nafuu

Moja ya mambo yanayoshangaza kuhusu Burundi ni unafuu wa bei za madawa ya binadamu katika maduka yanayofanya biashara hiyo kulinganisha na nyumbani Tanzania.

Mfano tembe moja ya dawa za minyoo hapa Tanzania unaweza kuinunua kuanzia Sh 2000 lakini kwa Burundi dawa hiyohiyo unaweza kununua tembe tatu kwa Sh 700.

Vitunguu kwenye upishi

Burundi wanapenda sana kutumia vitunguu pindi wanapopika vyakula vyao na ukifika usishangae kuona hata samaki wa kukaangwa wamejazwa vitunguu huku nyanya na viungo vingine vikiwa vichache.

Barabara

Ukiingia Burundi kwa usafiri wa barabara unapaswa kuwa makini kwenye uendeshaji wa chombo hicho cha usafiri kwani wenyewe gari zao zinatembea upande wa kulia na sio kushoto tofauti na nyumbani Tanzania ambako zinatembea upande wa kushoto wa barabara.

Soda sukari kiduchu

Aina nyingi ya kinywaji aina ya soda huwa haziwekwi kiwango kikubwa cha sukari na wanapendeleza zaidi zile ambazo hazina sukari ambazo ndizo zinanunulika kwa wingi.