Haya ndio maajabu ya Robben Ulaya

Muktasari:

Kocha wake wa zamani wa timu ya vijana ya Groningen, Barend Beltman anasema anakumbuka mchezo wa Mei 13, 2000 hadi mapumziko, Robben alikuwa amefunga mabao sita peke yake.

Wakati akiifundisha Bayern Munich, Pep Guardiola ambaye kwa sasa anainoa Manchester City, yaliwahi kumtoka maneno kuwa awapo na mpira, Arjen Robben ni rahisi kwa mabeki kufanya makosa.

Robben ambaye ameamua kutangaza kutundika daluga amekuwa akitajwa kama ni mmoja wa mawinga bora kuwahi kutokea muongo huu kutokana na makubwa aliyofanya akiwa na vigogo mbalimbali wa soka la Ulaya.

Guardiola aliwahi kukaririwa kipindi hicho akiwa Bayern akisema washambuliaji wake, Thomas Müller na Robert Lewandowski walikuwa bora kwa sababu ya uwepo wa Robben.

“Kila anapokuwa uwanjani tena anapomiliki mpira ni rahisi mabeki kufanya makosa, ilikuwa ni faida kwa washambuliaji hao,” hayo yalikuwa ni maneno ya Guardiola.

Kutokana na makubwa aliyofanya, Robben katika uchezaji wake soka, kocha wa zamani wa Uholanzi, Bert van Marwijk anasema angepata nafasi ya kuchagua kati ya mchezaji huyo na mastaa wengine kama vile Lionel Messi na Cristiano Ronaldo asingepepesa macho.

“Kama kocha nadhani Robben angekuwa chaguo langu ni mchezaji aliyekamilika,” anasema.

Kocha wake wa zamani wa timu ya vijana ya Groningen, Barend Beltman anasema anakumbuka mchezo wa Mei 13, 2000 hadi mapumziko, Robben alikuwa amefunga mabao sita peke yake.

“Tukiwa tumekwenda mapumziko akanifuata na kusema kocha, ujue sijawahi kufunga mabao 10 katika mchezo mmoja, nikamwambia nenda utafanya hivyo.

“Aliporejea kipindi cha pili alifikisha mabao tisa,akiwa kwenye nafasi ya kufunga la 10, aliamua kumpa pasi mwenzake ambaye hakuwahi kufunga bao, si mbinafsi hata kidogo,” anasema Barend.

Robben alianza kutamba akiwa na timu ya vijana ya Groningen ya nchini kwao Uholanzi kwenye miaka ya 1996 hadi 2000 ambapo alipandishwa na kuanza kucheza kikosi cha kwanza.

Nyota huyo aliyestaafu soka akiwa na miaka 35, alicheza kwa miaka miwili Groningen na baada ya hapo alisajiliwa na vigogo wa soka la nchi hiyo, PSV ambao na wenyewe ni kama walikuwa daraja kwake la kujiunga na matajiri wa London, Chelsea.

Alicheza Chelsea kwa mafanikio kabla ya kutimkia Hispania ambako alijiunga na Real Madrid na baadaye akaenda kumalizia soka lake Ujerumani ambako alicheza kwa miaka 10.

Katika uchezaji wake wa soka, Robben ambaye ni fundi wa kutumia mguu wake wa kushoto ametwaa karibu kila aina ya makombe lakini hakuwa na bahati ya kubeba ubingwa wa kombe la dunia.

Akiwa na PSV ya nchini kwao Uholanzi alitwaa makombe mawili, ambayo ni Ligi Kuu nchini humo ‘ Eredivisie’ msimu wa 2002–2003 na kombe la mfunguzi wa msimu ambapo lilipewa jina la marehemu Johan Cruyff alipostaafu.

Nchini England alibeba makombe sita ambayo ni Ligi Kuu mara mbili kwenye misimu ya 2004–2005, 2005–2006, kombe la FA, 2006–2007, Kombe la Ligi pia mara mbili, 2004–2005, 2006–2007 na mara moja ngao ya jamii, 2005.

Moto wa kutwaa mataji haukuzimika alipotua Real Madrid alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Hispania msimu wa 2007–2008 na Ngao ya Jamii ‘Supercopa de Espana’, 2008.

Kilele cha mafanikio yake alikifikia akiwa na miamba ya soka la Ujerumani, Bayern Munich ambao alijiunga nao, mwaka 2009 alicheza kwa kiwango cha juu na kutwaa kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, 2012-13.

Robben alifanya makubwa katika mchezo wa fainali dhidi ya Borussia Dortmund iliyokuwa chini ya kocha wa sasa wa Liverpool, Jürgen Klopp kwa kuiwezesha Bayern kutoa dozi ya mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Wembley, England.

Dortmund ilikuwa imesheheni kwa kuwa na mastaa kama vile Mats Hummels, Sokratis Papastathopoulos, Llkay GundoGan, Nuri Sahin, Pierre-Emerick Aubameyang ambaye hakuwa na namba mbele ya Robert Lewandowski.

Robben aliisumbua sana ngome ya Dortmund na ndiye aliyehusika na mabao yote mawili ya Bayern, alianza kwa kutengeza lile lililofungwa na Mario Mandzukic dakika ya 60.

Japo Dortmund walilisawazisha dakika ya 68 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Gundogan, Robben akiwa na jezi nambari 10 mgongoni aliipa ubingwa huo, Bayern kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 89.

Mbali na ubingwa huo wa Ligi ya Mabingwa, katika orodha yake ya mataji aliyotwaa akiwa ni Ujerumani ni pamoja na manane ya Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’.

Kama unakumbuka, Robben akiwa na timu yake ya taifa ya Uholanzi nchini Afrika Kusini, 2010 lilipofanyika kwa mara ya kwanza kombe la dunia, alishindwa akiwa na wakina, Mark van Bommel, Nigel de Jong,Wesley Sneijder, Dirk Kuyt na Robin van Persie kufua dafu mbele ya Hispania.

Robben na Uholanzi yake walishindwa kutwaa kombe hilo katika mchezo wa fainali baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, lakini aliambuliwa medali baada ya Uholanzi nafasi ya pili.