Haya haya! Solskjaer kapewa 200mil huko

Muktasari:

  • Kocha huyo amepanga kunasa makinda wenye uzoefu ili kukifanya kikosi chake kuwa moto uwanjani huku mabosi wake wakifurahishwa na kiwango chake kwenye timu hiyo baada ya kupunguza pengo la pointi baina ya timu hiyo na Liverpool na Manchester City kwenye Ligi Kuu England.

MANCHESTER, ENGLAND.NAKWAMBIA wapinzani wa Ole Gunnar Solskjaer mbona kazi mnayo msimu ujao! Ni hivi, kocha huyo mpya wa Manchester United amekabidhiwa mkwanja mnene, usipungua Pauni 200 milioni kwa ajili ya kufanya usajili wa mastaa wapya katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Ripoti za kutoka Old Trafford zinafichua kwamba Ole amekabidhiwa pochi nene la kuhakikisha anairudisha Man United katika makali yake na kuwa timu inayoshindania ubingwa kwenye michuano mbalimbali na si kama inavyobahatisha kwa sasa.

Kocha huyo amepanga kunasa makinda wenye uzoefu ili kukifanya kikosi chake kuwa moto uwanjani huku mabosi wake wakifurahishwa na kiwango chake kwenye timu hiyo baada ya kupunguza pengo la pointi baina ya timu hiyo na Liverpool na Manchester City kwenye Ligi Kuu England.

Wakati makinda Jadon Sancho, Callum Hudson-Odoi, Declan Rice na Aaron Wan-Bissaka wakiwa kwenye mpango, Solskjaer amemwambia makamu mwenyekiti wa Manchester United, Ed Woodward anahitaji pia wachezaji walio tayari kwa ajili ya mechi kubwa kama vile mabeki wa kati, Kalidou Koulibaly na Raphael Varane ili kuja kuongeza nguvu kwenye kikosi chake.