Haya hapa ulikuwa huyajui kwa nyota hawa

Wednesday May 15 2019

 

MADRID, HISPANIA.KWENYE viwanja vya soka, hakuna asiyewajua na kukubali uwezo wao. Hata hivyo, zaidi ya kuona chenga na mabao yao bora kila mwisho wa wiki timu zao zinapokuwa uwanjani. Kuna mambo mengi sana yametokea kwa wanasoka ambayo kwa hakika, yanasisimua. Iwe ni ndani au nje ya viunga vya soka.

Ni wazi, sio wote wanaoyafahamu mambo hayo na makala haya bila ajizi inakuwekea machache kutoka kwa baadhi ya nyota wa soka ambayo ulikuwa huyafahamu.

Juan Mata

Mhispania huyu kutokea kunako klabu ya soka ya Manchester United ambaye anacheza katika nafasi ya kiungo mshambuliaji, anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika Ligi Kuu England kuhama kutoka Chelsea kwenda Manchester United. Alijiunga na Chelsea akitokea katika Valencia kwa dau la Euro 26.70 milioni na baadae kutoka Chelsea na kujiunga na Manchester united kwa kiasi cha Euro 44.73 milioni na kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya ligi hiyo kutoka Chelsea na kujiunga na Manchester United.

Xavi Hernandez

Kiungo mwingine wa Kihispania akiwa ni zao la klabu ya Barcelona ya nchini humo, Xavi anakumbukwa na mashabiki wa soka duniani kwa pasi zake zenye macho na zenye udambwiudambwi akiwa na klabu hiyo. Hata hivyo, usilolijua kuhusu kiungo huyu fundi wa soka ni hivi, akiwa na umri wa miaka 19 alikaribia kusaini katika klabu AC Milan ya Italia na alipata ruhusa kutoka kwa baba yake, lakini mama yake alisema “Kama Xavi atajiunga na AC Milan na kuiacha Barcelona” basi ataitaji talaka kuachana na baba yake Xavi. Hapo ndipo mchezaji huyo alipoamua kuchezea Barcelona ili kuleta furaha katika familia yake.

Ryan Giggs

Giggs amewahi kutamba na Manchester United na timu ya taifa ya Wales. Pia amewahi kuifundisha klabu hiyo kama kocha wa muda kumaliza msimu wa Ligi Kuu. Usichokijua kwa nyota huyu, anashikilia rekodi ya Ligi Kuu England ya kuwa mchezaji pekee aliyeifikisha mabao 100 bila ya kufunga (hat-trick), yaani mabao matatu ndani ya mechi moja tangu anze kuichezea klabu hiyo.kwa sasa Giggs anaifundisha timu ya taifa lake ya Wales.

Christiano Ronaldo na LIonel Messi

Tuwaite wafalme wa soka wa kizazi cha sasa. Hii ni kwa sababu ya ufundi wao na makubwa waliyoyafanya na kuteka hisia za watu. Leo ukiamka Messi kafanya jambo, kabla hujalala unasikia Ronaldo kafanya yake. Wachambuzi wengi wa soka wanadhani hakuna wanasoka wengine watakaotokea kama wao.

Ambalo hulijui kuhuso nyota hawa wawili ni utofauti wa miaka yao, Ronaldo aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1985 na Messi aliyezaliwa Juni 24, mwaka 1987 ni siku 869 sawa na miaka miwili. Kinachovutia zaidi ni, utofauti wao ni sawa na utofauti wa miaka ya watoto wao wa kwanza Christiano Ronaldo Jr aliyezaliwa June 2010 na Thiago Messi alizaliwa Novemba 2011.

Zinedine Zidane

Fundi wa kulisakata kabumbu anayetumia akili na vile anavyotaka na kuwapa wapinzani kazi kubwa ya kumkaba. Mfaransa huyu mwenye asili ya Kialgeria, Zizzou anashikilia rekodi ya aina yake. Enzi zake za kucheza soka kabla hajageukia ukocha, alikuwa anacheza nafasi ya kiungo mshambuiaji. Sasa unaambiwa kwa kipindi chote cha soka lake katika nafasi hiyo, Zizzou hajawahi kuwa katika eneo la uviziaji mipira (Off-side). Aliwahi kutamba na klabu za Juventus na Real Madrid kabla ya kuteuliwa kuwa kocha wa Madrid na kujiwekea rekodi nyingine ya kuwa kocha mwenye mafanikio baada ya kuinua vikombe vitatu mfululizo vya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kabu hiyo.

James Rodriguez na Nicklas Bendtner

James Rodriguez ambaye ni staa wa soka kutokea Real Madrid anayekipiga kwa mkopo Bayern Munich, wakati aliposajiliwa na Real Madrid, ilifanya mauzo ya jezi 50, 000 za James kwa muda wa siku moja. Kwa upande wa Nicklas Bendtner, Juventus ilimchukua kwa mkopo staa huyo wa zamani wa Arsenal akitokea Wolfsburg ya Ujerumani na kutokufanya mauzo ya jezi hata moja ya mchezaji huyo kwa msimu mzima. Bendtner kwa sasa anakipiga katika klabu ya Roseburg ya Norway.

Arthur Wharton

Huyu ni mchezaji wa zamani aliyetamba kunako miaka ya 1885 huko England akitamba na klabu za Darlington, Preston North End na Sheffield United zingine kibao. Kama hujui tu, Wharton ndiye mchezaji wa kwanza mwenye asili ya weusi kucheza soka la kulipwa. Alikuwa akicheza kama kipa winga.

Advertisement