Hawa wapinzani Afcon kundi C: Stars ina kazi na vifaa hivi huko Misri

Muktasari:

  • Makala haya inakuletea kikosi cha mastaa 11 ambao wanaotamba kwenye klabu mbaimbali barani Ulaya ambao nyota wa Stars watakabiliana nao huko Misri.

BAADA ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kuondolewa kwa aibu kwenye Fainali za Afrika kwa Vijana chini ya umri huo (AFCON U17) zinazoendelea nchini, jicho la Watanzania sasa limeelekezwa kwenye timu ya taifa ya wakubwa ‘Taifa Stars’ ambayo itashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu zitakazofanyika Misri.

Katika fainali hizo zitakazochezwa kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, Stars imepangwa kundi C pamoja na timu za Senegal, Algeria na Kenya.

Ni wazi Stars ina kazi kubwa ya kufanya ii iweze kutinga hatua zinazofuata za mashindano hayo kwani wapinzani wake hao watatu wana timu zenye ubora wa hali ya juu na zenye wachezaji wanaofanya vizuri kwenye klabu mbalimbali wanazochezea.

Mbaya zaidi timu hizo zina vikosi vinavyojumuisha wachezaji wenye majina makubwa wanaocheza na kutamba kwenye klabu tofauti barani Ulaya ambao ni wazi kwamba kama wachezaji wa Stars wasipowadhibiti kwa umakini, wanaweza kutuadhibu.

Makala haya inakuletea kikosi cha mastaa 11 ambao wanaotamba kwenye klabu mbaimbali barani Ulaya ambao nyota wa Stars watakabiliana nao huko Misri.

1. Alfred Gomis-Senegal

Bahati nzuri kwa Stars ni kuwa watakutana na timu ambazo hazina makipa wanaochezea klabu zenye majina barani ulaya kulinganisha na wachezaji wa nafasi za ndani kwenye vikosi vya wapinzani wao.

Hata hivyo ukipima makipa wa timu hizo zote tatu, kidogo jina la mlinda mlango wa Senegal anayedakia SPAL inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia, Alfred Gomis linaweza kuleta angalau chembe ya mshtuko.

Kipa huyo mwenye thamani ya Euro 3 milioni, msimu huu ameidakia SPAL jumla ya mechi 19, akiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26 huku akicheza mechi sita (6) bila kuruhusu bao. Ameichezea timu ya Taifa ya Senegal mechi tano na ameruhusu mabao matano.

2. Youssouf

Sabaly- Senegal

Nyota atakayecheza nafasi ya winga wa kushoto wa Stars anaweza kupata urahisi kidogo dhidi ya Kenya na Algeria lakini anapaswa kujiandaa vilivyo kukabiliana na beki wa kulia wa Senegal anayechezea Girondins Bordeux inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.

Sabaly aliyeanza kuichezea Senegal tangu mwaka 2017 hadi sasa amecheza jumla ya mechi 12 za timu yake hiyo ya taifa na ana thamani ya Euro 10 milioni akiwa na umri wa miaka 26.

3. Ramy Bensebaini-Algeria

Unakumbuka mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 ya mashindano ya Europa League ambao Arsenal ilichapwa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Stade Rennais ya Ufaransa?

Basi kuna beki mmoja wa kushoto mwenye umri wa miaka 24 raia wa Algeria, Ramy Bensebaini ambaye aliwaficha vilivyo washambuliaji wa Arsenal na kama atakuwa mzima hadi wakati wa AFCON, basi mastraika wa Stars wanapaswa kujiandaa kukabiliana na beki huyo mwenye thamani ya Euro 8 milioni

4. Kalidou Koulibaly-Senegal

Anatajwa kama mmoja wa mabeki bora wa kati duniani kwa sasa na kuna ofa nyingi timu yake ya Napoli imekuwa ikizipokea kutoka timu mbalimbali ambazo zina majina makubwa kama Barcelona na Manchester United kwa ajili ya kumnasa Koulibaly mwenye thamani ya Euro 70 milioni.

Huenda ndiye akapewa jukumu la kumdhibiti Mbwana Samatta kwenye mashindano ya AFCON 2019.

5. Salif Sane - Senegal

Nyota huyo wa kati wa Senegal mwenye thamani ya Euro 15 milioni, anachezea klabu ya Schalke 04 inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani na anatarajiwa kutengeneza pacha sambamba na Koulibaly kama ambavyo wamekuwa wakicheza mara kwa mara.

6. Victor Wanyama- Kenya

Mmoja wa nyota wanaofanya vizuri na wenye majina makubwa ndani ya kikosi cha Tottenham Hotspurs kinachoshiriki Ligi Kuu England ni kiungo Victor Wanyama ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya.

Ndiye mchezaji ambaye bila shaka atafuatiliwa na kutazamwa kwa ukaribu na timu pinzani kwenye mashindano hayo. Kutokana na kile anachokifanya kwenye klabu yake.

7. Yacine Brahim- Algeria

Mwaka 2015 alikuwa gumzo nchini baada ya kuiongoza Algeria kuichapa Stars kwa mabao 7-0 kwenye mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia ambao walicheza uwanja wa nyumbani.

Bado Brahimi mwenye umri wa miaka 29 na thamani ya Euro 25 milioni ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa Algeria na kuelekea kwenye Fainali za AFCON, mabeki wa Taifa Stars wanapaswa kujiandaa kukabiliana naye.

8. Idrissa Gueye-Senegal

Ni mchezaji tegemeo na anayefanya vizuri kwenye kikosi cha kwanza cha Everton kutokana na uwezo wake wa kupora mipira kutoka kwa timu pinzani, kuituliza na kuichezesha timu pamoja na kuiunganisha timu

Thamani yake kwa sasa ni Euro 20 milioni.

9. Sadio Mane- Senegal

Mafanikio ya Liverpool ambayo kwa sasa inanyemelea ubingwa wa Ligi Kuu ya England lakini pia Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na juhudi za mshambuliaji Sadio Mane katika kupika na kufunga mabao.

Mane mwenye umri wa miaka 27 na thamani ya Euro 85 milioni, hadi sasa ameifungia Liverpool mabao 18 katika mechi 33 na atakuwa miongoni mwa nyota tutakaokabiliana nao kule Misri.

10. RIyad Mahrez- Algeria

Thamani yake ni Euro 60 milioni na hiyo imechangiwa na kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha kwenye mechi mbalimbali za mashindano ambayo Manchester City inashiriki na hapana shaka ni miongoni mwa wachezaji tishio sio tu kwa kundi bali mashindano hayo.

11. Keita Balde- Senegal

Ana umri wa miaka 24 na thamani yake sokoni ni Euro 24 milioni akiwa anaichezea Inter Milan inayoshiriki Ligi Kuu ya Italia.

Ni miongoni mwa nyota wa Senegal waliong’aa kwenye Fainali zilizopita za Kombe la Dunia na kama asipopata majeraha, hapana shaka kuwa sura yake itaonekana AFCON mwaka huu.