Hawa ndio wababe wa CAF

Muktasari:

Droo ya robo fainali imepangwa kufanyika Jumatano, jijini Cairo yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kiutaratibu timu nne zilizoongoza makundi zitapangwa kucheza dhidi ya timu nne zilizoshika nafasi ya pili.

SIMBA imeingia kwenye vitabu vya rekodi vya michuano ya CAF baada ya juzi Jumamosi kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuilaza 2-1 AS Vita kwenye Uwanja wa Taifa.

Mabingwa hao wa Tanzania waliiungana na vigogo wengine saba kupenya hatua hiyo na sasa wanasubiri keshokutwa Jumatano kujua watavaana na nani katika mechi zao za kuwania kutinga nusu fainali ambapo watazidi kutunisha mfuko wao wa hazina.

Ukiondoa Simba na Al Ahly zilizofuzu kutokea Kundi D, timu nyingine sita ambazo zimepenya ni CS Wydad Casablanca ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini zilizokuwa kundi A, Horoya ya Guinea na Esperance ya Tunisia zote za kundi B, TP Mazembe ya DR Congo na CS Constantine ya Algeria zilipenya kupitia Kundi C.

Droo ya robo fainali imepangwa kufanyika Jumatano, jijini Cairo yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kiutaratibu timu nne zilizoongoza makundi zitapangwa kucheza dhidi ya timu nne zilizoshika nafasi ya pili.

Kwa maana hiyo Wydad Casablanca, TP Mazembe, Al Ahly na Esperance zitawekwa katika chungu cha kwanza na Simba, Constantine ya Algeria, Mamelodi na Horoya zitakuwa chungu cha pili.

Hata hivyo hakuna uwezekano wa Simba kupangwa na Al Ahly kwenye robo fainali kwa sababu walikuwa kundi moja na hivyo wawakilishi hao wa Tanzania wanaweza kukutana na timu mojawapo kati ya Esperance, Wydad Casablanca au TP Mazembe.

ESPERANCE

Ndio watetezi wa taji hilo wakilitwaa msimu uliopita kwa kuichapa Al Ahly kwa ushindi ushindi wa jumla wa mabao 4-3 ikipoteza kwa mabao 3-1 ugenini kabla ya kushinda mabao 3-0 nyumbani.

Espérance Sportive de Tunis ilianzishwa Januari 15 1919 zaidi ya miaka 100 iliyobaki na uwanja wao wa nyumbani ni Olympique de Radès wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 kama Uwanja wa Taifa.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Hamdi Meddeb amempa kibarua cha kukinoa kikosi hiko kocha Moïne Chaâbani.

Thamani ya klabu hiyo kwa sasa inafikia (Euro 14.76milioni).

WYDAD CASABLANCA

Silaha kubwa ya Wydad Casablanca ni uwanja wao wa nyumbani ambao wamekuwa wakiutumia vyema kupata matokeo ambayo yamekuwa yakiwavusha kwenda hatua zinazofuata lakini wamekuwa hawatishi sana ugenini.

Ilianzishwa Mei 6, 1937 uwanja wake wa nyumbani ni Stade Mohammed V, Casablanca wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 45,891, Rais wao Said Naciri ambaye amempa kazi ya kukinoa kikosi hiko kocha Faouzi Benzarti.

Rekodi zao zinaonesha katika Ligi ya Mabingwa Afrika mbali ya kuwa wanashiriki mara kwa mara na kuweka rekodi nyingi wamechukua ubingwa mara mbili katika miaka ya 1992 na 2017 huku msimu uliopita wakiishia katika hatua ya nusu fainali.

Wydad Casablanca katika mtandao wa Transfer Markert inaonesha kuwa na thamani ya (Euro 13.21 milioni) ambayo kwa mujibu wa mtandao wa Oanda inaonesha kuwa klabu hiyo inafika thamani ya zaidi ya Sh 41 Bilioni.

TP MAZEMBE

Ikiwa itapangwa kukutana, haitokuwa mara ya kwanza kwani kabla ya hapo walishawahi kukutana mwaka 2011 kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa na Simba ikatolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 6-3 lakini baadaye Mazembe waliadhibiwa na kutupwa nje kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakuwa halali.

Rekodi inaonesha TP Mazembe mbali ya kucheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika mfululizo ameweza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano huku ikicheza fainali mbili.

TP Mazembe yenye zaidi ya thamani (Euro 3.49 milioni) kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Markert pesa hiyo ni sawa na Sh 10.85 Bilioni kwa pesa ya Tanzania kwa mujibu wa mtandao wa Oanda ambao unaonesha usawa na thamani ya pesa wa kila nchi, amechukua ubingwa katika miaka ya 1967, 1968, 2009, 2010 na 2015 huku pia akicheza fainali 1969 na 1870.

Mwaka 1939 ndio ilianzishwa TP Mazembe wakati huo ikiitwa FC Saint-Georges, uwanja wake wa nyumbani ni Stade TP Mazembe, ambao upo Lubumbashi unauwezo wa kubeba mashabiki 18,500 huku Rais wa klabu hiyo ni Moïse Katumbi ambaye amempa kibarua ya kukinoa kikosi hiko Kocha Mihayo Kazembe.

MAMELODI SUNDOWNS

Mamelodi Sundowns katika msimu uliopita waliishia katika hatua ya makundi lakini wamechukua ubingwa mara moja mwaka 2016 na kucheza fainali moja 2001.

Mamelodi inatumia uwanja wa nyumbani wa Masterpieces Moripe, uliopo Pretoria ambao una uwezo wa kuchukua wataazamaji 51,762 mmiliki wa timu hiyo ni Patrice Motsepe na ipo chini ya kocha Pitso Mosimane.

Klabu hii kongwe nchini Misri inaonesha kuwa na thamani ya (Euro 19,28 milioni) ambayo kwa pesa ya Kitanzania inaonesha kuwa ni zaidi ya Sh 59 Bilioni.

HOROYA

Mafanikio makubwa ambayo Horoya imeyapata katika mashindano haya ya Ligi ya Mabingwa ni msimu uliopita waliishia katika hatua ya robo fainali kama iliyotinga wakati huu.

Horoya ilianzishwa 1975, uwanja wao wa nyumbani unatambulika kama 28, Septembre, Conakry wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 25,000 huku Rais wake akiwa Antonio Souaré huku kocha mkuu akiwa Patrice Neveu.

Thamani ya klabu hii inaonesha kuwa ni (Euro 525) kwa pesa ya Kibongo inakuwa Sh 16 Bilioni.

CS CONSTANTINE

Timu ya Sportif Constantinois ilianzishwa Juni 26, 1898 na uwanja wao wa nyumbani ni Mohamed Hamlaoui wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 40,000 Rais wa klabu hiyo Tarek Arama huku kocha akiwa Denis Lavagne.

Katika Ligi ya mabingwa Afrika hawana rekodi ya kutisha kwani wameshiriki mara mbili mara ya kwanza ilikuwa 1998 ambapo iliishia katika mzunguko wa kwanza na msimu huu ndio kwao una mafanikio makubwa katika mashindano hayo.

Thamani yake (Euro 7,93) kwa pesa ya Tanzania ni zaidi ya Sh 24 Bilioni.

AL AHLY

Katika hatua ya robo fainali hawataweza kukutana na Simba kwani walishacheza katika hatua ya makundi na kama watakutana basi ni katika mechi ya hatua ya nusu fainali lakini timu zote ziwe zimepata matokeo ya kuwafikisha hapo.

Al Ahly ilianzishwa Aprili 24, 1907 zaidi ya miaka 111, walifika fainali msimu uliopita, uwanja wao wa nyumbani ni Cairo International Stadium wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 75,000 ingawa muda mwingine hubadilishwa katika matumizi ya mashindano haya.

Kocha Martín Lasarte ndio anakinoa kikosi cha Al Ahly. Kwenye soka hakuana kisichowezekana hongera Simba.