Hawa mastaa wamesapraizi kinoma Ligi Kuu

Muktasari:

Wachezaji ambao wamesapraizi katika ligi kwa namna ambavyo matokeo yamekuwa ni ya kushangaza katika msimu huu.

LIGI Kuu Tanzania Bara ilimalizika Jumapili na kinachosubiliwa ni kuona tiomu zinazopambana kubaki Ligi Kuu kwani bingwa tayari amepatikana, bali kwenye vita ya kushuka ni Singida, Lipuli, Ndanda na Alliance ndizo zimeshuka moja kwa moja.

Wakati hayo yakitokea wapo wachezaji ambao wamesapraizi katika ligi hiyo kwa namna ambavyo matokeo yamekuwa ni ya kushangaza katika msimu huu.

Mwanaspoti linaangazia wachezaji ambao wamesapraizi kwa matukio ambayo wameyafanya msimu huu, licha ya kwamba walikuwa wamepata nafasi katika ligi, lakini wakaondoka katika klabu kwa matatizo mbalimbali, huku wengine wakirudi nyumbani pamoja na kwamba walishatoka.

HARUNA NIYONZIMA

Kiungo huyu alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza 2011 akitokea APR ya Rwanda na kukaa Jangwani hadi 2017.

Baadaye Niyonzima alijiunga na Simba ambako alidumu kwa miaka miwili (2018/19) kisha akarejea zake AS Kigali ambapo alicheza kwa muda mfupi mwaka huu kabla ya kurejea tena Yanga.

Kurejea kwa Niyonzima klabuni Yanga kuligeuka kuwa sapraizi kwa mashabiki wa Jangwani ambao wakati anaondoka kwenda Simba walifikia hatua ya kuchoma jezi ya namba nane aliyokuwa anavaa Yanga.

Lakini msimu huu baada ya kurejea amekata kiu yao kutokana na kiwango ambacho anakionyesha na kugeuka kuwa mhimili katika eneo la kiungo.

ABDALLAH SHAIBU ‘NINJA’

Wengi walibariki kitendo cha kuondoka na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Picha zake akiwa na mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahamovic akiwa LA Galaxy nchini Marekani ziliwafanya mashabiki waamini kwamba mchezaji huyo anazidi kupasua anga, lakini baadaye amekuja kuonekana akiwa mazoezini Yanga.

Mwenyewe anadai kwamba fedha ambazo alikuwa anapata hazikuwa zinamsaidia katika mambo yake, hivyo akaona bora arejee nchini kuja kuanza kupambania maisha yake mengine.

Hii ni kama sapraizi kwa waTanzania kwani wengi walitarajia kumuona akisonga mbele zaidi baada ya kutoka nchini. Hata kama alikutana na misukosuko, basi aalipaswa kuendelea kusikilizia ofa zingine akiwa hukohuko, lakini sio kurejea Yanga kwa kuwa ni kama amerudi chini zaidi na bora angeendelea kupambana kupata timu nyingine hukohuko Ulaya.

SHIZA KICHUYA

Winga huyu mtoto wa Morogoro alikuwa amejitengenezea jina katika kikosi cha Simba kutokana na umahiri wake uwanjani mpaka kufikia hatua ya kutimkia nchini Misri katika klabu ya Pharco.

Kichuya alitumia muda mwingi kuwa Tanzania kuliko Misri, jambo ambalo baadhi ya watu walijua kabisa wepesi wa yeye kurejea nchini ni rahisi kwa kuwa mwenyewe alishaanza kujiweka mbali na timu.

Msimu huu katika dirisha dogo, Kichuya alisaini mkataba wa miezi sita kuitumikia Simba, lakini tangu ajiunge nayo hajawa mchezaji anayepata nafasi katika kikosi cha kwanza. Kurejea kwake nchini kuliwashtua watu kimtindo kwani wenzake Himid Mao na Yahya Zaiid wameendelea kupambana hukohuko Misri.

IBRAHIM AJIBU/BENO KAKOLANYA

Habari kubwa ilikuwa kwa Ibrahim Ajibu kurejea tena Simba, licha ya kwamba alikuwa amepewa unahodha katika kikosi cha Yanga.

Aliyekuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera aliamua kumtuliza Ajibu kwa kumpa unahodha, lakini pia alikuwa akimpa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Mashabiki wa Yanga wengi walikuwa wanaamini kwamba msimu huu wangeendelea kuwa naye, lakini aliwapiga sapraizi baada ya kwenda kufuata ‘minoti’ ambayo aliwekewa mezani na Simba na muda huu hapati hata nafasi ya kuanza kikosini Msimbazi.

Kwa Beno Kakolanya, naye wengi walitarajia kumuona akienda katika klabu ambayo angepata nafasi ya kucheza moja kwa moja kikosini, lakini haijawa hivyo badala yake aliamua kwenda kugombea namba na Aishi Manula ambaye ameaminiwa katika kikosi hicho.

Hata hivyo kinachombeba kipa huyu ni uwezo wake tu uwanjani kwani hata akipewa muda wa kucheza bado anafanya kazi yake kwa ufasaha na ustadi wa hali ya juu.

GADIEL MICHAEL

Beki huyu alikuwa ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha timu ya Taifa waliokuwa nchini Misri katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Inaelezwa kwamba alipata dili la kucheza moja ya timu nchini Misri, lakini alilipotezea na badala yake alirejea nchini na kusaini Simba.

Licha ya kupotezea dili la nje bado alikuwa na ofa ya kuendelea kusalia katika kikosi cha Yanga, lakini inaelezwa alizima simu na kumpotezea meneja wake na kusaini kimyakimya Simba na kuwasapraizi mashabiki wa Yanga ambao walikuwa na imani kwamba mchezaji huyo ataendelea kusalia katika kikosi chao. Hivi sasa yupo zake benchi akicheza kama chaguo la pili mbele ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amekuwa mhimili mzuri katika upande wa beki ya kushoto kwenye kikosi cha Simba.

BERNARD MORRISON

Winga huyu kutoka Ghana anaingia katika orodha hii kutokana na kufanya tukio kubwa ambalo limeacha maswali mengi kwa mashabiki wa Yanga.

Katika mchezo wa Yanga dhidi ya Simba uliomalizika kwa wana Jangwani kuchezea kichapo cha mabao 4-1, Morrison alipofanyiwa marekebisho na nafasi yake kuchukuliwa na Patrick Sibomana, mchezaji huyo alionyesha kuchukia na badala yake kutoka na kwenda moja kwa moja vyumbani jambo ambalo ni nadra kuonekana katika soka.

Morrison baada ya kuingia vyumbani alibadilisha nguo kisha akaondoka zake na usafiri wa bajaji. Hili ni tukio ambalo liliwafanya mashabiki wa soka nchini kubaki midomo wazi.

LUIS MIQUISSONE

Hii nayo ni sapraizi katika soka la Bongo. Haina ubishi kwa sababu mashabiki wa Yanga walikuwa na imani kubwa kwamba mchezaji huyo anatua kwao, lakini baadaye mabosi wa Simba wakatibua mipango yote.

Simba walivyomtambulisha mchezaji huyo viongozi wa Yanga walibaki midomo wazi wakiwa hawaamini.Hivi sasa Miquissone amegeuka kuwa nyota katika kikosi cha Simba kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira pamoja na chenga za kukera huku akiwa mtupiaji mzuri nyavuni wa mashuti ya mbali.

Yanga wamekosa mtu wa namna yake kwani Patrick Sibomana licha ya kuanza kwa makeke mengi, lakini alipotea ghafla.