Hawa kusepa dirisha dogo

Friday November 9 2018

 

By SADDAM SADICK,MWANZA

KANDA ya Ziwa msimu huu mambo yalikuwa safi baada ya kufanikiwa kuwa na idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara huku zikionyesha ushindani kwa timu kubwa kama Simba,Yanga na Azam.
Licha ya kwamba ligi ya msimu huu imekosa udhamini na kusababisha timu kushiriki michuano hiyo katika mazingira magumu, lakini wachezaji wameamua kujitolea na kufanya kazi yao bila kujali.
Kanda ya Kanda ya Ziwa inawakilishwa na timu za Mbao FC na Alliance(Mwanza),Stand United na Mwadui FC (Shinyanga),Biashara United (Mara) na Kagera Sugar ya mkoani Kagera.
Licha ya kupambana lakini zipo timu ambazo bado hali yake ni tete kwenye msimamo wa Ligi Kuu, lakini wachezaji wake wamekuwa watamu na zipo dalili za kuweza kuzihama kipindi cha dirisha dogo linalotarajia kufunguliwa Novemba 15.
Mwanaspoti imeziangalia timu hizo za Ukanda wa Ziwa kwa mchezaji mmoja mmoja na kubaini kuwa upo uwezekano wa Klabu hizo kuwakosa nyota wake pindi dirisha dogo litakapofunguliwa kutokana na uwezo waliouonyesha.

SAID KHAMIS- MBAO FC
Uhai wa Klabu hii yenye maskani yake Wilayani Ilemela Jijini Mwanza umechagizwa na nyota huyu ambaye kwa kiasi kikubwa ameisaidia timu hiyo kuwa katika nafasi nzuri kwenye msimamo.
Mabao yake matano aliyoyaweka nyavuni yanamfanya Straika huyu chipukizi kuwatoa mate timu kubwa ikiwemo Simba na Yanga na kuna uwezekano dirisha dogo akavaa uzi mpya.
Hadi sasa nyota huyo amekuwa katika ushindani na nyota wa klabu kubwa kama, Emauel Okwi na Meddie Kagere (Simba) na kuweka vita ya kupambana kusaka kiatu cha mfungaji Bora msimu huu.

EVALIGESTUS MUJWAHUKI- MBAO FC
Mshambuliaji huyu hadi sasa ameshaweka hazina ya mabao matatu katika mechi alizocheza na kuweza kujizolea mashabiki kutokana na mchango wake ndani ya klabu hiyo ya jijini Mwanza.
Nyota huyu ambaye amesajiliwa kutoka Mwadui, amekuwa ni ‘Super Sub’ kwani licha ya kutoanza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza lakini ameonyesha uwezo wake katika mechi ambazo zilikuwa ngumu.
Mujwahuki ambaye awali alikipiga hapo kabla ya kujiunga na Mwadui, amerejea kikosini na kuonyesha mchango ,kwani mechi ya ufunguzi wakicheza dhidi ya Alliance FC akitokea benchi aliweza kuifungia bao ambalo liliipa ushindi Mbao.
Lakini kama haitoshi wakati wanacheza dhidi ya Mbeya City wakiwa tayari wameshalala mabao 2-0, nyota huyo akitokea benchi aliweza kusawazisha yote na kumfanya kuwa mchezaji mwenye uwezo binafsi na huenda akavaa uzi mpya dirisha dogo.

HANS MASOUD- ALLIANCE FC
Licha ya kuwa mara yao ya kwanza timu hii kushiriki Ligi Kuu na kuwa katika nafasi za chini, lakini Kinda huyu ameonyesha uwezo wake kwa kuwadhibiti washambuliaji katika mechi zao.
Pamoja na kwamba uzoefu umekuwa tatizo kwao, lakini kwa namna moja au nyingine, Masoud amekuwa mhimiri mkubwa kwenye kikosi chake na tetesi zinasema kuwa huenda akatimkia KMC ambao tayari wameonyesha nia ya kumuhitaji.
Katika kutambua ubora wa kijana huyu, ameweza kufanikiwa kuitwa kwenye timu ya Taifa Vijana (U-23).

DICKSON AMBUNDO- ALLIANCE FC
Winga huyu ambaye ndio mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu lakini mchango wake  umekuwa mkubwa sana kwa kuweza kutengeneza nafasi nyingi.
Ambundo ambaye kwenye msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza aliibuka mfungaji bora kwa kupachika mabao 14,ndiye ‘ijini’ ya Alliance hadi sasa na juzi wakati wakiilaza Mtibwa Sugar, nyota huyo alionyesha uwezo wa juu.

ALEX KITENGE- STAND UNITED
Straika huyu raia wa Burundi alianza kwa kasi licha ya kwamba kwa sasa mambo yamekwama,lakini huenda dirisha likafunguliwa anaondoka kutokana na uwezo alionao kwenye kabumbu.
Mrundi huyu ambaye ameitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Burundi chini ya miaka 23,alionyesha umahili wake wakati Stand United ikipepetana na Yanga na kuweza kupiga ‘Hat-triki’ ya kwanza kwenye Ligi Kuu.
Tayari timu ya KMC imeshaonyesha nia ya kumuhitaji nyota huyo kuitumikia mzunguko wa pili ili kutibu tatizo la umaliziaji kwenye kikosi chao kinachoongozwa na Mrundi Ettiene Ndayiragije.

RAMADHAN KAPERA - KAGERA SUGAR
Nyota huyu aliyesajiliwa kutoka Majimaji iliyoshuka Daraja msimu uliopita hakuwa katika ubora wake baada ya kupata majeruhi na kucheza mechi chache kabla ya Kocha, Mecky Mexime kumuona na kumuita kikosini.
Kwa sasa Mshambuliaji huyu amekuwa moto katika timu hiyo baada ya kuisaidia Kagera Sugar kuifungia mabao matatu na kama ataamua kusaka timu mpya katika dirisha dogo huenda asikwame.

IBRAHIM NASSER -MWADUI FC
Licha ya kwamba Klabu hii imekuwa katika hali ngumu kwa kushindwa kupata matokeo mazuri na kujikita katika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi, lakini Straika huyu raia wa Burundi amekuwa msaada mkubwa ndani ya timu hiyo.
Mwadui katika mechi zake 12 walizocheza hadi sasa wameshinda miwili, ambapo katika ushindi huo, nyota huyo amehusika kwani awali aliifungia wakiwa mkoani Mara dhidi ya Biashara United kisha kufunga la pili dhidi ya Stand United.
Ni wazi kuwa kama timu yoyote itamuhitaji anaweza akafanya makubwa na tayari taarifa za ndani zinasema kuwa Mrundi huyo huenda asibaki wakati wa dirisha dogo akatimkia zake nchini Kenya kati ya timu ya AFC Leopard au Sofapaka FC.

GEORGE WILLIAM- BIASHARA UNITED
Licha ya Klabu yake kuwa mkiani kwenye msimamo lakini Straika huyu ambaye ndiye msimu wake kukipiga Ligi Kuu ameonyesha kiwango bora na hakuna shaka huenda Dirisha dogo likaenda naye timu nyingine.
Hadi sasa kati ya mabao matatu waliyofunga timu nzima,Straika huyo aliyesajiliwa kutoka Pamba ndiye alifunga mawili hivyo kubaki kuwa chaguo namba moja katika safu ya ushambuliaji ya Kocha,Hitimana Thiery.
Hivyo kama ataamua kuondoka huenda rekodi yake ikambeba kwa timu yoyote na akaweza kufanya vizuri kulingana na mfumo wa Kocha atakayekuwa naye.

Wasikie viongozi Stand United
WASIKIE V
Kuotokana na tetesi za kwamba straika wao,Alex Kitenge kuhitajika na KMC,Uongozi wa Klabu hiyo unaeleza kuwa hadi sasa hawajapokea taarifa kutoka Klabu yoyote kuhitaji mchezaji wao na kufafanua kuwa wao hawamkatazi mchezaji kujiunga na timu iwapo ataipenda.
Meneja wa timu hiyo,Freddy Masai anasema kuwa uongozi unathamini maisha ya mchezaji ,hivyo hata mikataba yao haizuii mchezaji kujiunga na timu yoyote iwapo pande zote wataafikiana.
“Hadi sasa bado hatujapata taarifa yoyote ya kuhitajika kwa mchezaji wetu,lakini kama kuna timu inauhitaji waje tuzungumze sisi hatumzibi mchezaji kujiunga na timu yoyote isipokuwa makubaliano”anasema Masai.

Advertisement