Hawa hapa wanaume wenye historia Afcon

Muktasari:

Makala hii inakuletea orodha ya mataifa matano ambayo yamefanikiwa zaidi kwenye fainali za AFCON, ama kwa kutwaa ubingwa, kumaliza kwenye nafasi ya pili au ya tatu au hata ile ya nne.

SIKU 28 zimebaki kabla ya kuanza kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) huko Misri ambazo zitaanza Juni 21 na kuhitimishwa Julai 19 zikichezwa katika viwanja sita tofauti ambavyo vipo kwenye majiji manne ambayo ni Cairo, Suez, Ismailia na Alexandria nchini humo.

Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, ni miongoni mwa nchi 24 zitakazoshiriki fainali hizo, ikifanya hivyo kwa mara ya pili, baada ya mwanzo kushiriki fainali za mwaka 1980 zilizofanyika Nigeria na kutolewa kwenye hatua ya makundi.

Kimsingi Stars inaenda kwenye mashindano hayo ikiwa haina historia yoyote kubwa ya kujivunia zaidi ya kushiriki lakini sio yenyewe peke yake kwani kuna idadi kubwa ya nchi ambazo zimeshindwa kutwaa taji hilo licha ya kushiriki mara nyingi kuzidi hata Taifa Stars.

Kuna timu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye mashindano hayo ambayo mwaka huu itakuwa ni awamu ya 32 kufanyika tangu yalipoanza kuchezwa mwaka 1957.

Makala hii inakuletea orodha ya mataifa matano ambayo yamefanikiwa zaidi kwenye fainali za AFCON, ama kwa kutwaa ubingwa, kumaliza kwenye nafasi ya pili au ya tatu au hata ile ya nne.

Misri

Wenyeji wa mashindano hayo mwaka huu, Misri wanaingia kama timu iliyofanikiwa zaidi kulinganisha na nyingine kuanzia kwenye ushiriki hadi mafanikio ambayo wamepata kwenye fainali za AFCON.

Misri ambayo jina lake la utani ni ‘Mafarao’ na ambayo kwa sasa inanolewa na kocha raia wa Mexico, Javier Aguirre, inaongoza kwa kutwaa taji la mashindano hayo ikiwa imefanya hivyo mara saba (7) ambazo ni mwaka 1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010.

Imemaliza kwenye nafasi ya pili mara mbili baada ya kufungwa mechi ya hatua ya fainali mwaka 1962 na 2017.

Nafasi ya tatu imeshika mara tatu ambazo ni mwaka 1963, 1970 na 1974 huku mara tatu ikimaliza kwenye nafasi ya nne katika fainali zilizofanyika mwaka 1976, 1980 na 1984.

Ghana

Inajulikana kwa jila la utani la ‘Black Stars’ na inanolewa na kocha Kwesi Appiah ambaye ni mzawa aliyewahi kuichezea timu hiyo miaka ya nyuma.

Ghana ni miongoni mwa timu ambazo zimetamba kwenye mashindano hayo kwani imetwaa ubingwa mara nne ambazo ni kwenye fainali zilizochezwa mwaka 1963, 1965, 1978 na 1982 na imemaliza kwenye nafasi ya pili mara tano ambazo ni mwaka 1968, 1970, 1992, 2010 na 2015.

Imemaliza ikiwa nafasi ya tatu mara moja ambapo ilikuwa ni mwaka 2008 na nafasi ya nne imeshika mara nne napo ni mwaka 1996, 2012, 2013 na 2017.

Nigeria

Ni moja ya nchi zinazoogopeka na kupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye Fainali za AFCON mwaka huu huko Misri na wengine wanaamini kuwa inaweza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kufanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 2013.

Inaingia kwenye fainali hizo ikiwa na rekodi ya kutwaa taji mara tatu, 1980, 1994 na 2013.

Imemaliza ikiwa nafasi ya pili mara nne nazo ilikuwa ni mwaka 1984, 1988, 1990 na 2000 huku mara saba ikishika nafasi ya tatu kwenye fainali za mwaka 1976, 1978, 1992, 2002, 2004, 2006 na 2010.

Ivory Coast

‘Tembo wa Pwani ya Afrika Magharibi’ ndio jina la utani la Ivory Coast ambayo nayo imekuwa ikitikisa kwenye Fainali za AFCON kwa kumaliza kwenye nafasi za juu mara kwa mara pindi inaposhiriki.

Imewahi kutwaa ubingwa wa AFCON mara mbili nazo ni mwaka 1992 na 2015 lakini imeshika nafasi ya pili mara mbili, mwaka 2006, 2012 na mara nne imeshika nafasi ya tatu nazo ni mwaka 1965, 1968, 1986 na 1994 huku mwaka 1970 na 2008 ikiwa imemaliza kwenye nafasi ya nne.

Cameroon

Fainali za mwaka huu wataingia wakiwa mabingwa watetezi baada ya kutwaa taji hilo kwenye awamu iliyopita mwaka juzi, katika fainali zilizofanyika Gabon wakiifunga Misri mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali.

Cameroon ni timu ambayo huwa haina mzaha pindi inapoingia hatua ya nusu fainali kwani mara saba ilivuka na kutinga fainali na mara mbili tu ndio ilishindwa kupenya kwa kuishia kugombea nafasi ya mshindi wa tatu.

Katika mara saba ambazo wametinga fainali ya mashindano hayo, wametwaa ubingwa mara tano ambapo ni miaka ya 1984, 1988, 2000, 2002, 2017 na imeshika nafasi ya pili mara mbili nazo ni mwaka 1986 na 2008.

Mara moja wamemaliza wakiwa nafasi ya tatu nayo ni mwaka 1972 na mara moja walishika nafasi ya nne katika fainali za michuano hiyo za mwaka 1992.