Hawa hapa mastaa waliowahi kutekwa

Muktasari:

  • Hadi sasa bado hali ya hewa haijatulia baada ya kutekwa kwa Bilionea, Mohammed Dewji (43) lililotokea juzi Alhamisi alfajiri Dar es Salaam katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Osterbay.

SINTOFAHAMU imetanda juu ya tukio la kutekwa kwa Mfanyabiashara Mohammed Dewji (43) lililotokea juzi Alfajiri Dar es Salaam katika Hoteli ya Colosseum iliyopo Osterbay.

Dewji ambaye ni mshindi wa zabuni ya uwekezaji wa 49% za hisa kwenye klabu ya Simba ambayo sasa inaendeshwa kwa mfumo wa kampuni ikiwa ni matokeo ya wazo la bilionea huyo, alitekwa hotelini hapo wakati alipofika kwa ajili kwenda kufanya mazoezi.

Kutekwa kwa Dewji ni kama mwendelezo wa matukio ya aina hiyo, ambayo yamekuwa yakiwatokea wanamichezo katika nchi mbalimbali duniani katika miaka na nyakati tofauti.

Mara kwa mara, matukio ya utekaji wanamichezo yamekuwa yakiendana na madai ya fedha ambayo watekaji huyatoa ili kuwaachia mateka hao.

Ukiondoa tukio la kutekwa kwa Mohammed Dewji, ifuatayo ni orodha ya wanamichezo na wasanii wenye majina makubwa ambao walikutana na matukio ya utekwaji katika maeneo tofauti duniani.

Alfredo Di Stefano-1963

Gwiji wa zamani wa soka wa Real Madrid na Argentina, Alfredo Di Stefano alijikuta akiingia mikononi mwa genge la watekaji, Agosti 24,1963 nchini Venezuela ambako klabu yake ilikwenda kuweka kambi ya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Hispania. Watekaji hao ambao walitumia silaha za moto, walimteka Di Stefano katika Hoteli ya Potomac jijini Caracas ambako Real Madrid ilifikia huku wakiweka sharti la kulipwa fedha.

Hata hivyo, siku mbili baadaye, Di Stefano alikutwa kwenye Ubalozi wa Hispania nchini Venezuela baada ya kuachiwa na watekaji hao ambao kwa mujibu wa nyota huyo, hawakumdhuru katika kipindi chote walichomshikilia huku wakiwa hawajalipwa chochote.

Ruben Omar Romano-2005

Nyota wa zamani wa Argentina, Ruben Omar Romano, naye alikumbwa na balaa la kutekwa nyara ambalo alikutana nalo Julai 19,2005 na kukaa mikononi mwa genge la watekaji hao kwa takribani siku 65 kabla ya kuokolewa na maofisa wa idara ya upelelezi usiku wa Septemba 21, 2005.

Victoria Beckham-2000

Mwaka 2000, idara ya usalama wa Taifa ya Scotland ‘Scotland Yard’ lilifanya kazi ya ziada kumwokoa mwanamuziki Victoria Caroline Adams ‘Victoria Beckham’ ambaye ni mke wa nyota wa zamani wa Manchester United na timu ya Taifa ya England, David Beckham kutoka mikononi mwa genge la watekaji.

Victoria alizungukwa na kundi la watekaji hao lakni ndani ya muda mfupi, Scotland Yards waliwahi kufika eneo la tukio na kumnusuru yeye na familia yake.

Jeremy London-2010

Mwigizaji Jeremy London aliyewahi kutamba na filamu Mallrats na Party of Five alitekwa akiwa katika mizunguko jijini London na watekaji walihitaji fungu la fedha. Baada ya kuhisi watakosa walichohitaji, watekaji hao walimpora gari mwigizaji huyo ingawa baadaye walikamatwa.

WENGINE NDUGU ZAO WATEKWA

Mbali na mastaa hao ambao walitekwa, kuna ambao tukio la utekaji liliwakuta ndugu na jamaa zao;

Baba wa Michael Jordan-1993

Mchezaji wa mpira wa kikapu maarufu, Michael Jordan, baba yake alitekwa na kuuliwa mwaka 1993 na watekaji ambao walikuwa wanalazimisha staa huyo awape fungu kubwa la fedha.

Baba wa Carlos Tevez-2014

Nyota wa zamani wa Argentina, Manchester United, Manchester City na West Ham, Carlos Tevez naye alionja shubiri ya watekaji baada ya baba yake kutekwa huko Argentina ingawa baadaye aliachiwa.

Baba wa Romario-1994

Matukio ya utekaji wa ndugu wa mastaa au watu maarufu Barani Amerika Kaskazini na Kusini ni kama utamaduni uliozoeleka. Mwaka 1994, watekaji walimtia mikononi baba wa mwanasoka wa zamani wa nchi hiyo, Romarioa lakini siku moja baadaye aliokolewa na Polisi.

Baba wa Jorge Campos-1999

Kipa wa zamani wa Mexico, Jorge Campos naye alikutana na makucha ya genge la watekaji mwaka 1999 ambao walimteka baba yake na kumshikilia kwa siku 10 kabla ya baadaye kumwachia.

Baba wa Diego na Gabriel Milito-2002

Mwaka 2002, wateka nyara walimshikilia baba wa wanasoka wawili maarufu, Diego na Gabriel Milito nchini Argentina na kisha kumuachia baada ya wanasoka hao kuwalipa kiasi kikubwa cha fedha.

Kaka wa Juan Roman Riquelme

Nyota wa zamani Argentina aliyewahi kuzichezea Boca Juniors na Villareal, Juan Roman Riquelme naye alilazimika kulipa kitita kikubwa cha fedha ili kumnusuru kaka yake ambaye alitekwa nyara huko Argentina.