Hawa buti za Eden Hazard wanavaa tu

Muktasari:

  • Real Madrid tangu kuondoka kwa Ronaldo wamekuwa wakihaha kusaka mchezaji wa kuziba pengo lake na mara kadhaa wamehusishwa na kumtaka Hazard na Neymar.

LONDON, ENGLAND. Vigogo Real Madrid hawaishi kuhusishwa na mpango wa kumnasa supastaa wa Chelsea, Eden Hazard ili kwenda kuziba pengo la Cristiano Ronaldo huko Bernabeu.

Dili hilo lilishindwa kukamilika kwenye uhamisho wa dirisha la kiangazi miezi michache iliyopita, lakini sasa presha imekuwa kubwa na huenda mambo yakawekwa sawa kama si kwenye uhamisho wa Januari basi utakuwa ule wa mwisho wa msimu.

Licha ya kwamba jambo hilo bado halijakamilika, hawa hapa ndio mastaa ambao wanaweza kuja kurithi buti za Hazard kama atang’oka kweli Stamford Bridge.

 

Aleksandr Golovin (CSKA Moscow)

Kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi huko Ulaya, Chelsea ilihusishwa sana na mpango wa kumsajili staa huyo wa Russia. Shida moja iliyokuja kutibua dili hilo ni Chelsea wenyewe kuchelewa kumtangaza Maurizio Sarri kuwa kocha wao mpya. Chelsea haitakuwa imefanya kosa kama itamfuata Golovin ili kupata huduma yake kufidia pengo litakaloachwa na Hazard kwenye kikosi chao.

 

Gareth Bale (Real Madrid)

Supastaa, Gareth Bale haonekani kuwa na uwezo wa kuziba pengo la Ronaldo huko kwenye kikosi cha Los Blancos na ndio maana wababe hao wa Bernabeu wanamtaka Hazard. Lakini, Chelsea wanaweza kufanya biashara moja ya kuwaambia Real Madrid wamchukua Hazard na wao wapewe Bale. Itakuwa biashara nzuri kwa sababu kila mmoja atakwenda kuziba pengo lililopo huko atakakokwenda. Bale atawasaidia Chelsea, lakini Hazard atakuwa staa mkubwa pia Madrid.

 

Dries Mertens (Napoli)

Mertens ni Mbelgiji kama alivyo Hazard. Staili yao ya kisoka kwa namna fulani inataka kufanana, hivyo Chelsea watakuwa wamefanya usajili mzuri tu kama wataamua kumchukua Mertens kuja kuziba pengo la Hazard atakapoamua kwenda kujiunga na Real Madrid. Huduma ya Mertens huko Napoli si ya mchezo na hakika ni mchezaji ambaye hatakuwa mgeni kwa kocha Maurizio Sarri kwa sababu waliwahi kuwa pamoja kwenye kikosi cha Napoli.

 

Anthony Martial (Man United)

Kitu ambacho Martial anakitaka ni kuaminiwa tu. Winga huyo wa Kifaransa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana. Maisha yake huko Manchester United yamekuwa na mapito mengi kwa sababu kocha Jose Mourinho haonekani kumwaamini jambo linalomfanya Martial kushindwa kuonyesha uwezo wake halisi aliokuwa nao. Chelsea kama itapeleka ofa kuhitaji huduma yake na kisha ikamwambia kwamba amekuja kuziba pengo la Hazard ni wazi Martial atalitendea haki jambo hilo. Martial ni kipaji.

 

Nabil Fekir (Lyon)

Liverpool walishindwa kumnasa Nabil Fekir kwenye dirisha lililopita kutokana na vipimo vyao vya afya. Lakini, kiungo huyo wa ushambuliaji ni staa wa maana huko Lyon na timu ya taifa ya Ufaransa. Panga pangua anapata namba kwenye vikosi hivyo, hivyo Chelsea watakuwa kwenye mikono salama kama wataichukua huduma yake kumbadili Hazard atakapochukua uamuzi wa kwenda kujiunga na Real Madrid ambayo mwenyewe anaamini ni timu ya ndoto zake.

 

Leon Bailey (Bayer Leverkusen)

Kinda mwingine matata kabisa anayefanya kweli kwenye Bundesliga akiwa na kikosi cha Bayer Leverkusen. Bailey ameelezwa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana na anatajwa akija kwenye Ligi Kuu England atatikisa kweli kweli kutokana na staili yake ya kiuchezaji. Chelsea itakuwa imepata mtu wa kurithi mikoba ya Hazard kama watafanikiwa kumnasa staa huyo wa Leverkusen, Bailey. Kwenye dirisha lililopita kinda huyo alisakwa sana na timu za Ligi Kuu England.

 

Wilfried Zaha (Crystal Palace)

Kwenye kikosi cha Crystal Palace, Zaha ni mchezaji mkubwa sana, ambaye mashabiki wa timu hiyo hawatakuelewa kama utakwenda kumsajili. Lakini, winga huyo aliwahi kupata nafasi ya kucheza kwenye klabu kubwa ya Ligi Kuu England, Manchester United. Hata hivyo, alipokuwa Old Trafford, Zaha hakuwa na kitu cha maana alichokifanya jambo linalozifanya klabu nyingine kubwa kufikiria mara mbili kunasa saini yake kwa sababu ameonekana kama ni mchezaji wa timu ndogo. Lakini, Chelsea wanaweza kuwa na mtu anayekaribia ubora wao kwenye kikosi kama watamchukua Zaha akarithi mikoba ya Hazard.