Hawa Simba Queens washindwe tu wenyewe

Tuesday March 12 2019

 

By Olipa Assa

JKT Queens ni kama imewapa dili Simba Queens namna ya kujipatia pointi tatu dhidi ya Evergreen, watakapokutana kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam.

Kilichomshtua Kocha wa Simba, Omary Mbweze ni baada ya kuona Evergreen imefungwa mabao 5-0 na JKT Queens tofauti na mzunguko wa kwanza walipigwa mabao 9-0 na hilo limekuwa kama ishara kwake kujua mechi yao itakuwa sio lele mama.

Mbweze alisema raundi ya kwanza waliwafunga Evergreen mabao 6-0 na kudai anaamini awamu hii watakuja kivingine kutokana na usajili wa dirisha dogo walioufanya.

“Evergreen kwa sasa ina mabadiliko makubwa ndio maana unaona wanapunguza idadi ya mabao tofauti na mwanzo waliruhusu mengi, tunacheza nao Jumatano na tunajua tutakuwa na kazi ngumu.

“Malengo yetu ya kuchukua ubingwa yapo pale pale haijalishi JKT Queens hawajafungwa mchezo hata mmoja, tunachoangalia sisi ni kushinda mechi zilizopo mbele yetu, tunaungwa mkono na viongozi wa juu wa Simba,” alisema.

Amina Ramadhani ambaye kwa sasa amefikisha idadi ya mabao 11 ndani ya kikosi hicho, alisema lengo lao ni kuhakikisha wanapambana kadri wanavyoweza ili kuweza kuchukua ubingwa.

“Tunaamini timu ya wanaume inaweza kutetea ubingwa, hivyo na sisi tunapambana kadri tunavyoweza ili tusiwe nyuma kupeleka taji la Ligi Kuu msimu huu, inawezekana na sio miujiza,” alisema.

Ligi ya msimu huu imekuwa ngumu hasa mzunguko huu wa pili huku kila timu ikipambana kuhakikisha inamaliza salama.

Advertisement