Havertz aivulia kofia EPL

LONDON, ENGLAND. KIUNGO wa Chelsea, Kai Havertz amesema Ligi Kuu England ni ngumu na inachokesha sana tofauti na ilivyo Bundesliga ambayo aina ya uchezaji wa timu zao ni za taratibu ukilianganisha na England ambazo zinahitaji mchezaji awe na nguvu na kasi sana.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alijiunga na Chelsea katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi akitokea Bayer Leverkusen na mpaka sasa amecheza mechi tano chini ya kocha Frank Lampard.

Havertz alionekana kuwa kwenye kiwango kibovu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuud dhidi ya Brighton lakini katika mchezo wa pili dhidi ya Barnsley alifunga ‘hat-trick’ kwenye ushindi wa mabao 6-0 katika michuano ya Carabao Cup.

Mchezaji huyo amethibitisha kwamba anahitaji kupata muda mrefu zaidi wa kuzoea mazingira na aina ya soka la England ili kuonyesha kiwango ambacho mashabiki wengi wa Chelsea wanakitarajia kutoka kwake. “Nimeanza kwa kiwango cha chini kwa sababu ligi hii ni tofauti kabisa na ile niliyotoka, hii ni kati ya ligi ambazo zinakuhitaji mchezaji utumie nguvu zaidi na akili ili kuweza kufanikiwa na hilo nimeligundua katika hii michezo michache ambayo nimebahatika kucheza,” alisema.

“Simaanishi kwamba Bundesliga ni ligi mbaya ama rahisi sana, lakini nimeona utofauti hapa, unapokutana na timu yeyote huwezi kusema ina wachezaji wa kawaida ama wenye viwango vya chini, wote wanaonekana kuwa na viwango vya juu na usipoangalia unaigharimu timu.”