Hatujui kama Liverpool watamfukuza mdudu wao

Muktasari:

Ligi bado mbichi lakini Pep Guardiola aliwahi kusema kwamba unaweza kukosa ubingwa au kuupata ndani ya mechi nane za mwanzo.

LIVERPOOL inaongoza kwa tofauti pointi nane. Maisha yanataka nini zaidi kwao? Suala la ubingwa lipo katika mikono yao. Lakini kadiri ambavyo Liverpool inavyoukaribia ubingwa ndivyo ambavyo inajivunja moyo zaidi.

Iko hivi. Kama Liverpool itachukua ubingwa msimu huu basi itachukua mara nyingi zaidi. Ile imani kwamba inaweza kuchukua ubingwa wa England itarudi. Nyakati hizi ikiwa inaongoza kwa tofauti ya point nane, wengi wao bado hawaamini kama itachukua kwa sababu ya jinamizi la msimu uliopita.

Lakini pia hawaamini kama watachukua pindi wakikumbuka jinsi Steven Gerrard alivyoteleza katika pambano la Chelsea miaka michache iliyopita na kuuacha ubingwa kizembe. Wanahisi wana nuksi fulani hivi.

Nahofia kwamba kama Liverpool haitachakua ubingwa baada ya kuongoza kwa pointi nane mpaka sasa, basi haitachukua tena kwa muda mrefu. kila inapoukosa, jinamizi la kuamini kwamba haiwezi kuchukua ndivyo linavyoongezeka zaidi.

Ligi bado mbichi lakini Pep Guardiola aliwahi kusema kwamba unaweza kukosa ubingwa au kuupata ndani ya mechi nane za mwanzo.

Kama ligi ingekuwa inaongozwa kwa tofauti ya pointi nane na Wolves tusingewapa presha ya kuwapa ubingwa. Lakini hii ni Liverpool yenye Sadio Mane, Mo Salah na Roberto Firmino huku ikiwa inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi nane.

Kwa mstari wake wa mbele ukijumlisha uwepo wa kina Virgil van Dijk lazima useme Liverpool kombe lipo katika mikono yake. Kama isipochukua msimu huu, kama ikipoteza uongozi wa pointi nane mkononi, basi mwisho wa msimu itajumlisha jinsi misimu hii miwili ilivyokwenda na nadhani kuna kitu kitazidi kuimarika katika mioyo yao kwamba haiwezi kuchukua ubingwa wa England tena.

Hili litakuwa jambo baya zaidi. Hakuna kitu kibaya au kizuri kama kutengeneza imani katika moyo.

Ni kitu kama hiki ndicho huwa kinaipa Liverpool ubingwa wa Ulaya. Kule huwa inaamini kwamba taji ni lake na inaweza kulichukua wakati wowote. Kwa England, imani hii imetoweka tangu mwaka 1990.

Hata inapokaribia bado huwa haiamini.

Sijui kama Liverpool itamfukuza mdudu huyu anayewanyima imani ya ubingwa wa England, wakati huu ikiongoza kwa tofauti ya pointi nane. Sijui. Ikifanikiwa, basi itachukua ubingwa mara nyingi tu.