Hatma ya Stars AFCON ipo mikononi mwa Cape Verde leo

Tuesday October 16 2018

 

By Angetile Osiah

Dar es Salaam. Baada ya kufungwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza mjini Praia, matumaini ya wengi ni kwamba Taifa Stars haiwezi kufurukuta mbele ya Cape Verde hata katika mechi ya leo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Wengi wanaelezea nafasi ya Cape Verde katika orodha ya ubora wa Fifa, ushindi mkubwa walioupata nyumbani kwao na ukaribu wao na Ureno na mataifa mengine ya Ulaya kama sababu nzito za wenyeji kutoweza kulipiza kisasi na hatimaye kujiweka katika nafasi nzuri katika Kundi L la michuano ya awali ya Mataifa ya Afrika.

Lakini mpira wa miguu ni mchezo wa maajabu na hata viwango vya Fifa hubadilika kutokana na matokeo, ambayo wakati mwingine ni tofauti na matarajio yanayotokana na rekodi za kwenye karatasi.

Na kwa kujua hilo, Fifa wameweka pointi nyingi kwa timu iliyo katika nafasi za chini za viwango vya ubora wa Fifa iwapo itaishinda timu iliyo juu katika orodha hiyo.

Hilo ndilo jambo linalotoa changamoto kwa timu nyingi kutaka kufanya "upsets" inapokutana na timu kubwa na ndivyo ilivyokuwa na itakavyokuwa kwa Taifa Stars leo itakapopata nafasi ya kujirekebisha jijini Dar es Salaam.

Cape Verde, ambayo inashika nafasi ya 67 kwa ubora na ambayo mwaka 2014 ilikuwa katika nafasi ya 27, ilitawala mchezo wa kwanza wakati Stars ikihangaika kutuliza timu na kupata uhakika japo wa kupiga pasi tatu mwanzoni mwa mchezo.

Ni katika kipindi hicho cha takriban dakika 22 wenyeji walifunga mabao mawili yaliyotokana na makosa ya mabeki yaliyosababishwa na uondoaji mpira vibaya golini na sehemu ya kiungo kutofanya vyema kazi ya kuiunganisha timu, kuituliza na kupeleka mpira mbele kwa haraka kila walipoupokonya.

Himid Mao, ambaye alishika kiungo akicheza mbele ya mabeki na ambaye mechi ya kwanza alianzia benchi kumpisha Frank Domayo, hakuweza kumeza "presha" ya wenyeji waliotumia mwanya huo kupitisha mipira mingi upande wa kulia.

Lakini mabadiliko ya kumtoa Gadiel Michael, aliyecheza kama kiungo wa kushoto, na kumuingiza Shomari Kapombe kumsaidia Mao katikati kulituliza timu ambayo ilianza kupata uhai na kuchangamka kipindi cha pili, ikiwa imetengeneza nafasi tatu za wazi, lakini Thomas Ulimwengu na John Bocco walishindwa kuzimalizia.

Ukosefu wa umakini, uliosababisha wachezaji kupoteza mipira mingi bila ya sababu, ulikuwa sababu kubwa ya Stars kuruhusu wenyeji wawashambulie kila wakati na hivyo ngome kufanya kazi ya ziada.

Kocha Emmanuel Amunike, ambaye alizungumzia tatizo hilo la umakini, atakuwa amefanyia kazi suala hilo baada ya kushuhudia vijana wake wakishindwa kurudia kiwango walichokionyesha mbele ya Uganda katika mechi iliyotangulia.

Bila ya shaka, Mbwana Samatta ataongoza tena safu ya ushambuliaji, akisaidiwa na Thomas Ulimwengu, ambaye alikosa mabao mawili baada ya kupata krosi safi kutoka kwa Abdi Banda.

Samatta alitumia muda mwingi wa mechi iliyopita kuchezesha wenzake hasa baada ya kocha kumtoa Gadiel aliyeanza kama winga wa kushoto, na kumuingiza Kapombe kwa lengo la kuimarisha kiungo.

Samatta alilazimika kukimbia umbali mrefu kujaribu kufika karibu na goli ili ajaribu shuti, lakini alikumbana na madaruga mengi yaliyomfanya afanikiwe kupiga kiki tatu bila ya kuwa katika nafasi nzuri.

Amunike atamlazimisha arudi katika nafasi yake ya kusubiri pasi za mwisho iwapo atakuwa ametatua tatizo la kiungo.

Kiwango kilichoonyeshwa na Bocco katika dakika 12 za mwisho, kinaweza kumfikirisha kocha kufanya uamuzi mgumu kati ya Ulimwengu na Bocco au kutumia washambuliaji wote watatu, wakisaidiwa na viungo watatu; Simon Msuva, Mudathir Yahya na Kapombe, aliyeonyesha uwezo mkubwa katika kiungo.

David Mwantika hakuwa katika kiwango cha kawaida na alishindwa kuupiga mpira mbali katika kipindi cha kwanza na kumpa nafasi Gomes Ricardo kufunga bao la kwanza. Ricardo pia alifunga bao la pili baada ya Mao kushindwa kumzuia Garry Rodriguez upande wa kushoto na mchezaji huyo kutoa krosi 'yenye macho' na ya chini iliyomkuta mfungaji.

Mwantika alibadilishwa katika dakika ya 73 na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Mtoni, ambaye alicheza upande wa kushoto na Banda kuhamia katikati. Lakini mchezaji huyo wa Lipuli hatarajiwi kuanza kikosi cha leo, badala yake Erasto Nyoni anaweza kuanza ili kuongeza uzoefu katikati ya ngome ya Stars.

Nyoni pia anaweza kupangwa sehemu ya kiungo iliyoongozwa na Mao na ambayo ilionyesha udhaifu mwanzoni.

Lakini mabadiliko ya wachezaji hayatakuwa na maana iwapo wachezaji wataingia uwanjani wakiwa hawajashughulikia suala la upotevu wa umakini ambalo lilikuwa tatizo kubwa, hasa mwanzoni mwa mchezo.

Ni dhahiri kuwa Cape Verde wasingepata mabao yaliyotokana na makosa ya mabeki mwanzoni mwa mchezo, wasingeweza kuendeleza "presha" na hivyo kuwapa fursa Stars kuamka na kwenda mbele kuwayumbisha wenyeji hadi waruhusu bao.

"Tatizo kubwa ni ukosefu wa umakini wa wachezaji wetu," alisema Amunike baada ya mchezo.

"Tutarudi nyumbani kushughulikia na tunatumaini tutatatua."

Cape Verde iliongozwa vyema na nahodha wake,Elvis Macedo aliyeituliza timu na kuiunganisha vyema, akipiga pasi za mbali zilizoiyumbisha ngome ya Stars.

Kiungo huyo anajivunia washambuliaji wake hatari na wazoefu, Ricardo Garry Rodriguez, ambao wana uwezo mkubwa wa kukaa na mpira, kupiga chenga na ujanja wa kutoroka mabeki.

 

 

Advertisement