Hatimaye wachezaji Simba wakabidhiwa bodaboda zao

Muktasari:

Wachezaji na benchi la ufundi wa Simba, leo Alhamisi walikabidhiwa zawadi za pikipiki aina ya Boxer, rice cooker na simu ndogo baada ya kufanya vizuri msimu uliopita.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed Dewji ameitimiza ahadi yake ya kuwakabidhi wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi pikipiki aina ya Boxer, simu ndogo pamoja na Rice Cooker.

Mo Dewji alitoa ahadi ya kuwapa bodaboda wachezaji wote wa Simba baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Waliokabidhiwa zawadi hizo ni wachezaji wote na viongozi wote wa benchi la ufundi walikuwepo kwenye timu hiyo msimu uliopita.

Hata hivyo, wakati wa makabidhiano hayo, Mo Dewji hakuwepo bali aliwakirishwa na watu wake mkurugenzi wa masoko, Fatuma Dewji.

Fatuma alisema, anasikia furaha na kutembea kifua mbele kutokana na namna Simba inavyofanya vizuri.

"Mo Dewji ametoa zawadi hiyo kwa sababu ya mapenzi yake na Simba baada ya kufanya vizuri katika kipindi cha msimu uliopita kama kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuchukua ubingwa,"alisema Fatuma.

Akizungumzia tukio hilo nahodha wa Simba, John Bocco alisema: "Tunashukuru ile siku ya ahadi leo hii imetimia, tunamshukuru Mo kwani zawadi hiyo inaongeza morali kwetu kuona tunapambana na kufanya vizuri katika mashindano yote yaliyo mbele yetu."

"Pia, tunawashukuru mashabiki wetu wote maana wamekuwa pamoja nasi muda wote,"alisema Bocco.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Masingiza alisema, anamshukuru Mo Dewji kwa hatua hiyo kwa sababu zawadi alizotoa ni kwa mapenzi yake ni nzuri kwa sababu itaongeza morali.

"Pikipiki hizi zikalete matokeo mazuri kwenu si kwa leo tu iwe faida hata ya miaka mitano hadi 10 mbele," alisema Mazingisa.