Hatima ya Yanga, Morrison yaiva

Muktasari:

Kiungo huyo mshambuliaji wa Yanga aliishitaki klabu hiyo kwa TFF akidai kuwa saini yake imeghushi katika mkataba wa miaka miwili

Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema hukumu ya madai ya kughushi saini ya mchezaji Bernard Morrison itatolewa Agosti 10 baada ya kazi ya uchunguzi iliyofanywa na Jeshi la Polisi kumalizika.

Kiungo huyo mshambuliaji wa Yanga aliishitaki klabu hiyo kwa TFF akidai kuwa saini yake imeghushi katika mkataba wa miaka miwili, ambao klabu hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani imeuwasilisha TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za uchunguzi wa suala hilo na hawana haja ya kuwa na papara ili kupata majibu sahihi.

Mwanjala alisema awali walipanga kutoa uamuzi wa suala hilo mwishoni mwa Julai na baadaye kupeleka mwanzoni mwa mwezi huu, lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao.

Alisema wamewasiliana na polisi na kupata majibu kuwa wanamalizia uchunguzi na mwishoni mwa wiki hii watawasilisha TFF kwa mujibu wa taratibu.

“Siyo suala la kukaa dakika au saa kadhaa na kutoa uamuzi. Jambo hili linahitaji umakini wa hali ya juu ili kupata majibu sahihi. Tumewasiliana na Jeshi la Polisi na kuambiwa kuwa kazi imekwisha na sasa wanaweka sawa taarifa za kiuchunguzi ili kutangazwa na TFF,” alisema Mwanjala.

Kuhusiana na suala la fedha alizopewa Morrison kurejeshwa Yanga, Mwanjala alisema hakuna taarifa hiyo hadi sasa zaidi ya kusubiri uchunguzi kukamilika.

Mbali ya Morrison kuishitaki Yanga, mabingwa hao wa kihistoria pia wameishitaki klabu ya Simba ikidai kuwa inaingilia mkataba wake na mchezaji huyo kinyume na utaratibu.

“Kwa kifupi masuala yote haya tutayatolea uamuzi wake siku hiyo. Tutakuwa na masuala mengi, ambayo yatatolewa uamuzi, kuna suala la wachezaji kudai mishahara yao, masuala ya mikataba na kesi mbalimbali,” aliongeza ofisa huyo.

Awali, Yanga ilimsajili Morrison kwa mkataba wa miezi sita kwa lengo la kuangalia kiwango chake na iliporidhishwa kuwa ana uwezo wake, ilidai kumuongezea mkataba wa miaka miwili ambao unamalizika katikati ya 2022.

Yanga ilisema mkataba huo ulisajiliwa TFF na Shirikisho la Kandanda Duniani (Fifa) kwa mujibu wa taratibu.