Hatima ya Morrison Oktoba 12

Sakata la mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison limeisukuma Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukutana Oktoba 12 ili kumjadili.

Sakata hilo limeibuka upya baada ya Yanga kuonyesha mkataba ambao wanadai ni wa mchezaji huyo na Simba, lakini ukiwa na saini ya mchezaji bila kuwa na saini ya klabu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Elias Mwanjala alisema jana kuwa watakutana siku hiyo ili kulijadili suala hilo. “Kamati yetu itakutana Oktoba 12 kwa ajili ya kupitia upya ishu ya mkataba wa Morrison na Simba,” alisema Mwanjala.

Alipoulizwa kama mkataba ambao Yanga wanauonyesha kuwa wa Morrison na Simba na una upungufu, Mwanjala alisema hajauona zaidi ya kuusikia.

“Oktoba 12 baada ya kikao ndiyo nitakuwa na majibu sahihi kuhusu mkataba wa Morrison na Simba, kwa sasa nimekuwa nikiusikia tu.”

Licha ya kuwepo taarifa kwamba TFF wamewarejeshea Simba mkataba huo ili waufanyie marekebisho, Mwanjala alisema hajui chochote na kuhoji ni lini ulirudishwa katika klabu hiyo. “Kama wamewarudishia basi ni jambo jema, ila sijui lolote hadi Oktoba 12 baada ya kikao ndipo nitazungumzia suala hilo,” alisema.

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema suala la Morrison wanalifuatilia na watakapokamilisha watalitolea taarifa.

“Sina kingine cha kuzungumza kuhusu Morrison, TFF tulishasema tunalifuatilia, tukikamilisha tutasema,” alisema Karia.

Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alidai mkataba huo una upungufu, huku akihoji uhalali wa Morrison kuidhinishwa na TFF kuichezea Simba kwa kutumia mkataba huo.

Awali, Yanga ambayo ilidai kumuongezea mkataba wa miaka miwili Morrison iliingia kwenye mgogoro na mchezaji huyo ambaye alidai hakuongeza mkataba na klabu hiyo baada ya ule wa awali wa miezi sita kumalizika.

Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF ilidai mkataba wa Yanga na Morrison ulikuwa na upungufu, hivyo kumtamka kuwa Morrison hana mkataba na klabu hiyo.