Hata kwa Wasafi mambo sio kama unavyodhani

Muktasari:

 Kando na usimamizi wa wasanii pia inamiliki redio na runinga. Lebo hiyo imewatengeneza wasanii wake na kuwafanya mastaa wakubwa kwa mfano Rayvanny, Lavalava, Mbosso Khan, Harmonize, Queen Darlin miongoni mwa wengine.

Nairobi, Kenya. KATIKA tasnia ya muziki suala la usimamizi sio kitu kidogo. Zipo lebo za kiusimamizi, zipo za kurekodi muziki tu na pia zipo zinazofanya kazi zote hizo.

Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, kwa kipindi cha mwongo mmoja uliopita, zimeibuka lebo nyingi za usimamizi. Huu ni mukhutasari wa misukosuko iliyoshuhudiwa kwenye lebo tajika katika ukanda huu.

Just In Love Music

Ni lebo aliyoanzisha msanii Otile Brown mwezi uliopita na msanii wa kwanza kusainiwa pale akiwa kichuna Jovial. Hata kabla ya wiki mbili kuisha, Otile alitibuana na Jovial na kuuvunja mkataba huo. Kwa sasa lebo hiyo kama kweli ipo, ina msanii mmoja tu ambaye ni yeye Otile.

Candy & Candy

Mwanzilishi wa lebo hii Joe Kariuki katoka jela ya Tanzania hivi majuzi baada ya miaka miwili akihudumia kifungo cha utapeli.

Kariuki alianzisha lebo hiyo 2012 baada ya kutoka zake majuu. Lebo hiyo aliianzisha Mombasa kabla ya kuhamishia afisi zake Nairobi.

Lengo la Kariuki ilikuwa ni kuwafufua wasanii wa zamani waliotisha sana ila wakafifia. Hivyo alianza kwa kufanya usajili mkubwa wa wasanii hao waliobuma akimchukua Fat S wa Mombasa, Top C, Baby Madaha, Hussein Machozi na Mr Nice.

Ikiwa lebo ya kiusimamizi, aliwapa wasanii hao mikataba mikubwa ya kurekodi, kuwaandalia shoo pamoja na kuwasakia dili zinginezo za kimatangazo.

Hata hivyo, baada ya miaka mitatu lebo hiyo haikuweza kuvutia biashara na kumplekea Kariuki kuifunga na kuhamia kwenye biashara za ujenzi na usafiri wa ndege.

Katika maneno yake hivi majuzi Kariuki alisema, “Lebo ya Candy & Candy ilipata umaarufu kutokana na uhusiano wake na muziki ila haikutengeneza faida na ndio sababu nimeonelea niwekeze kwenye majengo.”

Baada ya kuanguka nchini Kenya, Candy alihamia Tanzania 2017 ambapo lebo hiyo sasa inajihusisha na biashara ya ujenzi na umiliki majengo.

EMB Records

Takriban miaka mitatu iliyopita, msanii wa Injili, Kevin Bahati alianzisha lebo yake ya EMB Records na kuwasaini wanamuziki Mr Seed, Wizdom, David Wonder na Rebecca Soki.

Hata hivyo, baada ya kuwekeza zaidi ya Sh6 milioni, EMB  licha ya kuachia hiti kadhaa kupitia wasanii hao ilishindwa kutengeneza faida na mwishoni mwa mwaka jana ilisambaratika. Bahati alimruhusu kila msanii aondoke kujitafutia maisha kwingine.

Kwenye mahojiano niliyofanya naye miezi michache iliyopita, Bahati alisema sababu za shughuli ya lebo hiyo kusita ni kutoweza kuimarika kibiashara licha yake kuwekeza zaidi ya Sh6 milioni kwenye usimamizi wa wasanii hao. Baada ya wasanii hao kuondoka, wapo waliojengeana bifu naye mpaka sasa.

Aprili mwaka huu Bahati aliifufua tena lebo hii safari hii akimsaini msanii mmoja pekee Danny Gift. Hata hivyo, taarifa tulizozinasa ni kwa mba kuna msukosuko kati ya Danny Gift na Bahati na huenda naye akajitoa.

 

Grand Pa Records

Kwa zaidi ya mwongo Grand Pa inayomilikiwa na rapa wa zamani produsa Reffigah ilifanya kazi kubwa ya kuibua vipaji vya wasanii, kuwakuza kisanaa na kuwafanya mastaa.

Hiti nyingi zilitengenezwa chini ya lebo hii. Wasanii kama vile Kenrazy, Sosoun, Majirani, Dufla Dilgon, Visita, DNA, Kiddis, Gin Ideal ni baadhi tu ya waliojitengenezea majina chini ya Grand Pa ambayo kando na kuwa lebo ya kurekodi ilikuwa pia ya kiusimamizi.

Hata hivyo baada ya miaka mingi, mpasuko mkubwa ulitokea miaka miwili mitatu iliyopita na wasanii wote wakubwa wakagura. Japo Reffigah kasisitiza mara si moja kwamba wasanii hao waliondoka baada ya mikataba yao kuisha, wanamuziki hao wamekuwa wakimshtumu kwa unyanyasaji. Lakini pia kinachoibua maswali zaidi ni kwa nini idadi kubwa ya wasanii iligura wakati mmoja. Grand Pa ikafa.

Mapema mwaka huu baada ya ukimya wa zaidi ya miaka miwili, Reffigah alifufua tena lebo hiyo kwa kutangaza usajili wa wasanii wawili chipukizi Mistony na Thomas Niweti.

Kaka Empire

Rapa King Kaka ndiye mwanzilishi wa lebo hii. Baada ya kuanzisha yapata miaka mitano iliyopita, alifanikiwa kuwasanii wasanii wakubwa kama vile Rich Mavoko kutoka Bongo, Arrow Bowy, Avril, Timmy Tdat na Owago Onyiro.

Na japo shughuli za lebo hiyo zinaendelea, wasanii wote hao watajika wameshagura na Kaka Empire kwa sasa imejitosa kwenye usimamizi wa wasanii chipukizi wanfahamika kama Empire’s Gold.

Japo King Kaka kasisitiza kuwa wasanii hao waliondoka baada ya mikataba yao kuisha, tetesi zilizopo kitaa zinaelezea stori tofauti. Wasanii hao wamekuwa waungwana kuficha ukweli wa kiini kilichowatoa pale, ila kwa mujibu wa tetesi ni kwamba waligura kutokana na kupunjwa kwenye mapato yao.

Wasafi Records

Kwa sasa ndio lebo inayoonekana kuwa na uhai katika ukanda huu. Ikiwa inamilikiwa na staa Diamond Platinumz akisaidiwa na mameneja watatu Babu Tale, Sallam Mendez na Said Fella, Wasafi imefika mbali kiusimamizi na kibiashara.

Kando na usimamizi wa wasanii pia inamiliki redio na runinga. Lebo hiyo imewatengeneza wasanii wake na kuwafanya mastaa wakubwa kwa mfano Rayvanny, Lavalava, Mbosso Khan, Harmonize, Queen Darlin miongoni mwa wengine.

Hata hivyo, lebo hiyo pia imekumbwa na misukosuko kibao. Msanii Rich Mavoko aling’oka baada ya miaka miwili tu akidai kuwa mkataba wake ulikuwa wa unyanyasaji. Mavoko aliikacha Kaka Empire na kusaini na Wasafi kwa mkataba wa miaka 10. Hakutimiza hata nusu yake.

Wengine waliogura ni meneja wa zamani wa Harmonize, Mr Puaz na wa Mbosso, Sandra Brown wakilalamikia mazingara mabaya ya kikazi na mshahara mdogo.