MTU WA PWANI : Hata Kagera Sugar wamemsahau George Kavila?

Muktasari:

Nilitegemea kuona TFF ikimpa Kavila, tuzo fulani ya heshima kama mtu aliyeitumikia Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa muda mrefu lakini imeshindwa kufanya hivyo.

GEORGE Kavila amestaafu rasmi kucheza soka la ushindani baada ya kutumikia zaidi ya klabu tatu tofauti za Ligi Kuu.

Hii ni baada ya kucheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa takribani miaka 20 mfululizo tangu alipokuwa kijana mdogo mwishoni mwa miaka ya 90.

Hata hivyo, hakuna anayejali rekodi hii ya Kavila kucheza Ligi Kuu kwa takribani miaka 20 mfululizo, ambayo sidhani kama kuna mchezaji mwingine aliwahi kuiweka wala kuifikia hapa nchini.

Sio Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lililoonyesha kujali na kuheshimu rekodi hiyo ya Kavila, sio Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) na hata klabu yake ya Kagera Sugar aliyoonyesha kuithamini rekodi ya mkongwe huyo anayecheza nafasi ya kiungo.

Mwisho wa siku Kavila amestaafu kimyakimya kama ilivyo asili yake yeye mwenyewe ya upole na ukimya nje na ndani ya uwanja.

Ni muendelezo wa soka letu kutotoa heshima kwa watu waliolitumikia kwa mafanikio au kuweka rekodi mbalimbali ambazo zingeweza kutumika kuvutia vizazi vinavyofuata katika soka kucheza kwa bidii ili kuzivunja ama kuzifikia.

Lakini watu kama hao wanapoenziwa, inazidi kuhamasisha vijana wadogo kuvutika na kuhamasika na mchezo wa soka wakiamini kuwa siku moja nao watapata heshima baada ya kufanya mambo fulani makubwa kama ambayo akina Kavila wameyafanya.

Nilitegemea kuona TFF ikimpa Kavila, tuzo fulani ya heshima kama mtu aliyeitumikia Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa muda mrefu lakini imeshindwa kufanya hivyo.

Nilifikiria Bodi ya Ligi kwa vile wao ndio wenye ligi yao, wangelipa uzito mkubwa tukio la Kavila kustaafu baada ya kucheza Ligi Kuu kwa miaka zaidi ya 20, kwa kulifanya kuwa ajenda kubwa ambayo ingeongeza thamani ya Ligi yetu na kuvutia kundi kubwa la watu kuifuatilia zaidi.

Lakini hakuna taasisi yoyote kati ya hizo mbili ambayo imeona kuwa Kavila amefanya kitu kikubwa na badala yake zimemuacha ajiendee zake.

Kana kwamba haitoshi, hata klabu yake Kagera Sugar imeshindwa kuona fahari kuwa na mchezaji aliyefanya jambo kubwa na la kihistoria kwa kucheza Ligi Kuu kwa muda mrefu na ikamuacha katika namna ambayo haipendezi.

Ilipaswa Kagera Sugar kumtambulisha na kumtangaza Kavila kama shujaa wao kwa kufanikiwa kuweka rekodi kubwa na ya kipekee kama hiyo akiwa mchezaji wa klabu yao lakini hawakuona faida ya hiyo.

Kwa bahati mbaya tabia hiyo ya kuwapa heshima na thamani watu waliofanya vizuri inaonekana sio utamaduni wetu hasa kwenye mchezo wa soka jambo linalofanya watu kama kina Kavila wasionekane kama kuna cha maana walichokifanya.

Kwa wenzetu nchi zilizopiga hatua kisoka, jambo lililofanywa na Kavila lingekuwa ndio habari ya mjini na lingetengeneza historia kubwa ambayo ingedumu vizazi hadi vizazi.

Lakini bado inaonekana ni utamaduni mgumu kuiga na watu hawana mpango wa kufanya jambo hilo kama ambavyo tumeshuhudia kupitia Kavila.

Itafika kipindi, vizazi vijavyo vitashindwa kufahamu kuwa Abdi Kassim ‘Babi’ ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa sababu hakuna lolote lililofanyika kutambulisha tukio hilo.

Hapo baadaye haitajulikana kuwa kuna marefa kama marehemu Hafidh Ally Tahir na Omar Abdulkadir, waliwahi kuchezesha mashindano makubwa ya soka duniani kwa sababu historia zao hazikupewa thamani na heshima stahiki.

Nani baadaye atajua kuwa refa kama Israel Nkongo amechezesha Ligi Kuu Tanzania Bara kwa zaidi ya miaka 15, wakati alipostaafu, hakukufanyika tukio lolote la kumtambulisha kwa hicho alichokifanya?

Je tutakuja kukumbuka kuwa Erasto Nyoni ni mchezaji aliyeitumikia timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa muda mrefu zaidi wakati hatuko tayari kuhifadhi na kuthamini rekodi yake hiyo aliyoiweka?

Hatuwezi kukumbuka kwa sababu hatuko tayari kubadilika na tunaona kama ni jambo gumu kulifanya pasipo kujua athari yake kwa vizazi vijavyo.

Inashangaza kuona watu waliofanya vizuri kwenye mpira wetu na kuweka rekodi mbalimbali hawapewi kile wanachostahili na badala yake wanaachwa wapotee na hizo rekodi au historia zao.

Tumeamua kuishi kizamani na ndio maana sio jambo la kushangaza kuona watu kama kina George Kavila wanaondoka kimyakimya.