Harry Kane kuzua balaa jipya

LONDON,ENGLAND. GARETH Southgate amepanga kumtibua zaidi kocha Jose Mourinho baada ya kudai kwamba atamwanzisha straika Harry Kane dhidi ya Denmark.

Kocha huyo wa England, Southgate alisisitiza “kila kitu kipo sawa” Kane kuanzishwa kwenye mchezo huo wa leo Jumatatu baada ya wiki iliyopita mchezaji huyo kufanyiwa vipimo vya paja.

Jambo hilo litawaingiza makocha hao wawili, Southgate na Mourinho kwenye mzozo mkubwa juu ya afya ya mchezaji huyo huku klabu yake na timu ya taifa zote zikihitaji acheze mechi zao.

Kocha wa Tottenham Hotspur, Mourinho alimwambia Southgate hadharani kwamba asimtumie Kane atamuumiza zaidi, huku straika huyo akicheza mechi 11 msimu huu, akianzishwa mara nane na Jumapili iliyopita alikuwa sub kwenye ushindi dhidi ya Ubelgiji kwa sababu hakuwa fiti kiasi cha kutosha.

Tayari kumekuwa na mjadala baina ya madaktari wa chama cha soka cha England na wale wa Spurs kuhusiana na ufiti wa mshambuliaji huyo kama uchovu unaweza kumsababishia kuwa majeruhi.

Kane alikosa miezi kibao msimu uliopita baada ya kusumbuliwa na maumivu ya misuli aliyopata kwenye mchezo wa Southampton kutokana na uchovu kitu ambacho kinawatia shaka kwa awamu hii.

Southgate alisema: “Nadhani atakuwa na uhakika zaidi baada ya kucheza dhidi ya Ubelgiji na kwa kusema hivyo, tunatumai ataanza Jumatano.”