Harrier yageuka ‘ambulance’ CCM Kirumba

Muktasari:

  • Mchezaji wa Coastal Union, Adeyum Salehe ameshindwa kuendelea na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao baada ya kuanguka ghafla akiwa uwanjani CCM Kirumba Mwanza.

Mwanza.Maisha ya wachezaji Tanzania yapo shakani, baada ya kukosekana kwa gari la wagonjwa kwenye Uwanja CCM Kirumba na kulazimika gari aina Harrier kumtoa uwanjani beki wa Coastal Union, Adeyum Saleh baada ya kudondoka ghafla na kupoteza fahamu wakati wa mechi ya Ligi Kuu dhidi Mbao.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika dakika 45, wakati beki huyo Saleh alipoanguka ghalfa uwanjani baada ya kupatiwa matibabu alitakiwa kubebwa na gari la kubebea wagonjwa ‘Ambulance’ lakini halikuwepo ndipo ilipolazimika kutumika gari aina ya Harrier kuingia uwanjani ili kumchukua.

Hata hivyo, kabla kuingizwa kwenye Harrier kwa ajili ya kukimbizwa hospitali beki Saleh alizinduka na kutolewa na kwenda kukaa jukwaanini.

Daktari wa Coastal Union, Kitambi Mganga amesema kuwa sababu ya mchezaji wao Salehe kuanguka uwanjani imesababishwa na kukosa maji mwilini kwani wamecheza wakati wa jua kali.

Mganga amesema kuwa hata hivyo tatizo hilo halitamfanya nyota huyo kukosa mechi zinazofuata kwani ni tatizo la muda.

"Tatizo amepungukiwa na maji mwilini, kutokana na jua kali, hili si tatizo kwa wachezaji tu hata kwa watu wengine wa kawaida, ila ni tatizo la muda ataendelea kucheza" amesema Kitambi.

Gari la wagonjwa liliingia kipindi cha pili dakika ya 61 wakati mchezo ukiendelea na hata hivyo hakuna tukio lingine lililojitokeza tena licha ya wachezaji kulala lala kila mara.

Fifa imetoa utaratibu wa mechi zinazochezwa wakati wa jua kali, kwa waamuzi kutoa muda kidogo kwa wachezaji kunywa maji, leo hapakuwepo jambo hilo haswa kwa dakika 45 za kwanza.

Katika mchezo huo Coastal Union ikiwa ugenini ilifanikiwa kuondoka na pointi tatu kwa kuichapa Mbao FC bao 1-0, shukrani kwa bao pekee la Raizin Hafidh aliyefunga katika dakika ya 59.