Harmonize ameshamaliza kuhesabu Sh 500 milioni za kumlipa Diamond?

LEO hapa kuna mjadala mkubwa kuhusu nafasi ya mameneja, Taletale, Sallam na Mkubwa Fella pale WCB. Nani meneja na yupi mzigo? Hivi Harmonize hajamaliza kuhesabu hizo Sh500 milioni amlipe Diamond? Wabunge wa kitaa, Luqman Maloto na Dk Levy wapo kwenye mimbari!

LEVY: Imefika wakati ndugu yangu umekuwa kama Man United. Lukaku kaondolewa na Sanchez kachomolewa, na mamilioni ya pesa za usajili unapewa lakini bado unafanya upuuzi. Au unataka watu waanze kusema “Bring Back our Sir Alex Ferguson?”

LUQMAN: Kama kakuudhi Mmasai wetu wa Norway, Ole Gunnar Solskjaer usinifananishe naye.

LEVY: Sawa sikufananishi naye lakini nalazimika kukufananisha naye kwa hulka siyo mwili wala rangi.

LUQMAN: Kosa langu nini ndugu daktari? Kwani mimi ndiye King wa Mpapaso, Masau Bwire aliyewapapasa Yanga na Ruvu Shooting yake?

LEVY: Yanga wananihusu nini mimi? Acha kunikumbusha kamba za Zahera. Yule Mkongo ndiye binadamu bingwa wa sababu.

LUQMAN: Zahera wewe anakuhusu nini kama Yanga haikuhusu?

LEVY: Napenda uongo wake tu. Zahera fundi wa sababu za uongo kuliko wabunge. Anawadanganya Yanga mpaka anageuka mfalme.

LUQMAN: Mimi Zahera hajawahi kunidanganya. Aliniahidi kuwatoa Township Rollers na kawatoa. Aliniambia Yanga ingeshiriki Klabu Bingwa Afrika hata ikimaliza nafasi ya pili na kweli imeshiriki. Pengine masikio yako yanageuza ukweli wake kuwa uongo wako.

LEVY: Kama ambavyo alisema Yanga itafungwa mechi ya kwanza na kweli ilifungwa. Kama ambavyo alimsajili Kindonki na Molinga na kuahidi ni wachezaji wazuri ni kweli. Zahera ni mkweli.

LUQMAN: Unajua Zahera amekaa sana Ulaya ndio maana humwelewi. Ingekuwa aliishi Marekani angekuwa mshkaji wako. Kwani kosa la Zahera kwako ni kuitwa Mwinyi?

LEVY: Hapana kosa lake kuu ni kuvaa vipensi. Ujue jamaa umri umeenda sana, lakini vipensi vinafanya aonekane kama Ali Kiba.

LUQMAN: Kwa hiyo Zahera role model wake ni Ali Kiba. Kumbe Zahera sio timu Diamond wala Konde Gang.

LEVY: Zahera ni Timu Zahera. Ndo wale viumbe hawafananishwi hata kwa bahati mbaya. Zahera ni kocha wa Yanga, kocha wa Congo DRC, msemaji wa Yanga na dalali wa wachezaji. Makambo ndo jibu sahihi la udalali wake.

LUQMAN: Achana na mutu ya kazi Zahera. Hivi Prof Jay ulimwelewa? Na jibu la Majani ulilisoma vyema?

LEVY: Wa Mitulinga nilimwelewa, alikuwa anawajibu COSOTA na kumpiga dongo Majani kiaina. Majani alielewa Mti Mkavu amempiga dongo ndo maana alijibu kimhemko. Elewa tu wale watu wanajuana kinyumenyume.

LUQMAN: Una akili kubwa. Sasa Jay alilalamika nini ikiwa Majani alikomaa na kesi peke yake yeye akapotezea? Isitoshe yale ni malipo ya instrumental, sio wimbo. Aliyetengeneza instrumental ni Majani sio Jay.

LEVY: Pro Jay hana haki na ile kazi. Hana haki na yale malipo. Hana haki na Cosota. Wala hana haki na haki ya haki. Anachotakiwa kufanya ni kumshukuru na kumpongeza Majani kwa kupata haki yake.

LUQMAN: Nasikia WCB wamemtoza Harmonize Sh500 milioni kama fidia ya kuvunja mkataba.

LEVY: Wacha bana. Mi sina hiyo taarifa. Ila akipata wakili msomi mzuri kama Kibatala, hawezi kulipa kiasi hicho na zaidi WCB ndo wanaweza kumlipa Harmonize. Hasa akikomalia suala la wale vibonge watatu kulipwa pesa wasiostahili. Hivi Said Fella ana kazi gani? Babu Tale ana kazi gani?

LUQMAN: Nasikia na Harmonize ameridhia kuwalipa WCB Sh500 milioni ili awe huru. Nasikia Harmonize hataki kabisa ugomvi na Diamond, ndio maana amekubali kulipa.

LEVY: Harmonize ana akili kuliko Diamond. Ana akili kuliko Sallam. Ana akili kuliko zile njemba mbili ambazo hazieleweki ni ‘menejazi’ au ni wapambe.

LUQMAN: Unawaita Mkubwa Fella na ndugu yangu Hamis Taletale njemba? Wale nasikia ndio ma’Don wa huu muziki baada ya Scofield Ruge Mutahaba!

LEVY: Hapana wangekuwa hivyo kina Tunda Man, Chege na Temba, Z Anto, Kassim Mganga na wengineo wengi wakuwa wasanii ooosh sorry, wanamuziki wakubwa sana.

LUQMAN: Kwa hiyo kati ya Tale, Fella na Sallam nani Don wa huu muziki?

LEVY: Hakuna Don wa ‘gem’ hapo. Mzee mbona unadhalilisha muziki. Sasa kama hao ni ma’Don mbona wanamuziki wengine wanaowasimamia hawakimbizi kama Dangote? Hao madalali kama madalali wa viwanja, vyumba, magari nk. Huyo Sallam pia ni meneja wa AY na Fid Q, unafahamu? Tale kawaacha wapi Tip Top? Saidi Fella kawasusa Chege na Temba. Sasa wanakuaje ma’Don watu wa hivyo? Hao wote Dangote akiwamwaga wanakufa njaa. Nikusimulie kitu?

LUQMAN: Nisimulie daktari. Nisimulie na usiache kitu mwanamume.

LEVY: Kuna wachungaji watatu (kama Fella, Tale, Sallam). Siku moja waliamua kwenda mapumzikoni.

Wakiwa huko mmoja akawambia wenzake: “Jamani leo mimi naongea ukweli ili mniombee... Nina tatizo la kuchukua sadaka waumini wangu wanapotoa. Zamani nilikua naiba kidogo kidogo lakini siku hizi nimezidisha sana... Naomba mniombee.”

Mchungaji mwingine akadakia fasta: “Kabla ya kukuombea na mimi nina jambo nataka kulisema. Nina tatizo la kuchukua wanawake kanisani kwangu, nilianza na wasioolewa lakini siku hizi mpaka wake za watu. Niombeeni wenzangu.”

Mchungaji wa tatu yeye akawaambia wenzake: “Kabla hatujaombeana mimi pia nina tatizo. Kila nikisikia neno lazima niwaambie watu. Siwezi kutunza siri kabisa, hata haya mliyoongea tayari hilo tatizo limekuja. Siwezi kukaa nayo moyoni. Bora niongee ili nimalize hili tatizo!”

LUQMAN: Kwani hao wachungaji walikuwa mameneja wa kwaya ya Kanisa au? Mbona sioni link ya kuwainganisha na akina Taletale, Sallam na Fella ambao ni mameneja wa muziki?

LEVY: Nimeamua tu kuwaunga kama ambavyo nao wameamua tu kujiita mameneja wakati ni madalali. Siamini katika wao aiseee. Na nashangaa nao wakawa wanamshangaa Marehemu Ruge wakati wao ndo wanayaishi wayasemayo.

LUQMAN: Kwani ukiambiwa uchague kati ya Fella, Taletale na Sallam, mmoja awe meneja wako, nani ana afadhali?

LEVY: Sallam ndo binadamu mwenye nafuu ya kujiita meneja. Hao wengine ni kama washikaji wanaoishi kwa mashemeji zao halafu wanashikilia rimoti ya tivii muda wote...

LUQMAN: Huo ni mtazamo wako, wale Taletale na Fella ni mameneja wakubwa, si unaona walipomfikisha Diamond Platinum? Hata Konde Boy alipo leo, ni matunda ya Fella na Taletale.

LEVY: Wote hao wamemkuta Diamond yupo vizuri. Kama ni mameneja wazuri na wamemfikisha hapo Diamond. Wameshindwaje kwa Chege Temba au Madee? Acha kusifia ujinga ndugu yangu. Hao ni kupe waliorundikana kwenye damu nyingi ya ng’ombe.

LUQMAN: Ni hivi, tufanye kila mtu aamini anachokiamini. Mimi naamini Taletale na Fella ni ma’Don wa huu muziki, wewe unaamini Sallam ndio Don. Tusilazimishane!

LEVY: Siwezi kukushangaa kwa maana mko wengi wa aina yako. Ndo nyinyi ambao mnashabikia tu mambo instagram huko bila kutafakari. Ngoja nikusimulie kitu kingine. Kuna msela mmoja alikuwa geto anavuta bangi. Mara baada ya bangi kukolea ghafla akaona mtu kasimama mbele yake. Kwa hofu jamaa akauliza; “Nani wewe?”

Akajibiwa: “Mimi ni Malaika mtoa roho.”

Msela: “Dah aiseee umenishitua kinoma nilidhani polisi. Basi poa mwanangu.”

LUQMAN: Au wewe unamhusudu Chambuso, yule meneja wa Aslay?

LEVY: Hiki kikao kingekuwa kinaruhusu kucheka ningekucheka sana. Bongo hakuna mameneja wa wanamuziki. Na wanamuziki wa Bongo walivyo hawajui kitu, eti mameneja wanawaita mabosi. Yaani Christian Rinaldo amuite Mendez bosi? Ulishasahi kusikia Neymar anamuita bosi wakala au meneja wake? Bongo hakuna meneja kuna wapigaji tu. Mwanamuziki kumuita meneja bosi, haina tofauti na Haji Manara kuwa muongeaji kuliko benchi la ufundi la Simba. Ushasikia msemaji wa Man City anaongelea ufundi wa Pep Guardiola? Sasa Manara anaongelea mpaka nani atapangwa na nani atakaa benchi. Bongo kila kitu tunafanya kinyume chake. Tumerogwa.

LUQMAN: Umerogwa mwenyewe, mimi sijarogwa.